Passenger 57
| Passenger 57 | |
|---|---|
| Imeongozwa na | Kevin Hooks |
| Imetayarishwa na | Dan Paulson Lee Rich Dylan Sellers |
| Imetungwa na | David Loughery Dan Gordon |
| Nyota | |
| Muziki na | Stanley Clarke |
| Imehaririwa na | Richard Nord |
| Imesambazwa na | Warner Bros. |
| Imetolewa tar. | Novemba 6, 1992 |
| Ina muda wa dk. | Dakika 84 |
| Nchi | Marekani |
| Lugha | Kiingereza |
| Bajeti ya filamu | Dola milioni 15[1] |
| Mapato yote ya filamu | Dola milioni 66.5 |
Passenger 57 ni filamu ya mapigano na kusisimua iliyotoka mwaka 1992 kutoka nchini Marekani. Filamu iliongozwa na Kevin Hooks. Filamu hii imechezwa na Wesley Snipes na Bruce Payne, ambapo Snipes anaigiza kama mtaalamu wa usalama John Cutter ambaye analazimika kukwamisha mpango wa kundi la kigaidi la kutaka kumwokoa gaidi hatari Charles Rane aliyekamatwa, wakati wakiwa kwenye ndege ya abiria. Maoni ya wakosoaji wa filamu yaligawanyika, lakini filamu hiyo ilipata mafanikio makubwa sokoni na kumfanya Snipes kuwa kielezo maarufu kama shujaa wa filamu za mapigano.
Hadithi
[hariri | hariri chanzo]Gaidi wa kimataifa kutoka Uingereza na bosi wa dawa za kulevya Charles Rane, ambaye uhalifu wake umepewa jina la "The Rane of Terror" (Utawala wa Kigaidi wa Rane) na vyombo vya habari, anakamatwa na FBI na mamlaka za usalama huko Miami, akiwa katika hatua ya kufanyiwa upasuaji wa kubadilisha sura ili kukwepa mkono wa sheria. FBI wanafanya mipango ya kumrudisha Rane jijini Los Angeles ili akabiliwe na mashtaka.
John Cutter ni askari mkongwe aliyefiwa na mke wake, akiwa na historia ya utumishi wa heshima kama polisi mwenye sifa nzuri, mwanajeshi aliyetunukiwa nishani, na wakala wa kuaminika wa Idara ya Usalama wa Rais anayejulikana kwa msimamo wake mkali dhidi ya uhalifu mkubwa. Akisumbuliwa kila wakati na kumbukumbu za kifo cha mkewe aliyeuawa kwa kupigwa risasi wakati wa ujambazi kwenye duka la mahitaji ya nyumbani, Cutter amezindua mafunzo maalum ya kuwafundisha hudumu wa ndege mbinu za kujihami. Baada ya darasa moja, Cutter anafuatwa na rafiki yake wa zamani, Sly Delvecchio, ambaye anamwomba kuwa Makamu wa Rais wa kitengo kipya cha kupambana na ugaidi kwenye kampuni yao ya ndege ya Atlantic International Airlines. Cutter anasita mwanzoni, lakini Delvecchio na rais wa kampuni hiyo, Stuart Ramsey, hatimaye wanamshawishi kukubali nafasi hiyo.
Cutter anapanda ndege kama abiria wa 57 kwenye usafiri wa Atlantic International kuelekea Los Angeles (ndege ya Lockheed L-1011 TriStar), ambapo mmoja wa wanafunzi wake, Marti Slayton, anafanya kazi humo kama mhudumu. Rane na mawakala wawili wa FBI wanaomshindikiza, Manning na Duncan, nao wamo ndani ya ndege hiyo. Baada ya ndege kupaa, wafuasi kadhaa wa Rane waliokuwa wamejifanya kama wahudumu wa ndege na abiria, wanawauwa mawakala Manning na Duncan, wanamfungua Rane, na kuiteka ndege kwa kumwua rubani mkuu pia. Cutter, ambaye alikuwa chooni wakati tukio hilo linaanza, anafanikiwa kutumia simu ya ndani ya ndege kumwonya Delvecchio kuhusu hali hiyo, lakini punde si punde anakamatwa na Allen, mmoja wa watu wa Rane.
Cutter anamzidi nguvu Allen na kumnyang'anya silaha yake; kisha anamtumia (kwa kumkaba koo) kama ngao ya kumkabili Rane, lakini Rane anaonyesha ukatili wake kwa kuwapiga risasi na kuwauwa baridi abiria mmoja anaitwa Douglas pamoja na mfuasi wake Allen. Cutter anatambua kuwa amezidiwa nguvu na kutoroka na Marti kuelekea sehemu ya chini ya mizigo na vifaa. Cutter anamwua mtu mwingine wa Rane aitwaye Vincent, aliyekuwa amejifanya mhudumu wa chakula. Cutter anaharibu mifumo ya umeme ili kumwaga mafuta ya ndege, hatua inayomlazimisha Rane kuwaamuru marubani waliobaki hai kutua kwenye uwanja mdogo wa ndege huko Louisiana. Wakati Cutter na Marti wakijiandaa kuruka nje mara baada ya ndege kutua, Marti anakamatwa na gaidi mmoja aitwaye Forget, na Forget anampiga teke Cutter na kumtupa nje ya ndege. Cutter anakamatwa na sheriff wa eneo hilo, Leonard Biggs, ambaye anadhani yeye ni gaidi, na kumpeleka kwenye jengo la uwanja wa ndege.
Rane anasiliana na mnara wa kuongozea ndege na kudai kuwekewa mafuta, akiahidi kuwa nusu ya abiria wataachiwa huru. Kwa kila dakika tatu za kuchelewa au kusuasua, ataamuru abiria watano wauawe. Rane pia anadanganya kuwa Cutter ni mmoja wa watu wake aliyewageuka. Biggs anaruhusu ndege iwekewe mafuta, na abiria wanapoanza kuachiliwa, Rane na baadhi ya watu wake wanatoroka kutoka kwenye ndege. Cutter anatambua kuwa kuachiwa kwa abiria ni mbinu ya kuwazuga, hivyo anajitorosha kutoka kwa Biggs na kumfukuza Rane na watu wake hadi kwenye tamasha la wilaya hiyo, ambapo anafanikiwa kumwua Matthew, mmoja wa watu wa Rane. Wakati Cutter akipambana na Rane, polisi wanawasili na kumkamata Rane, huku mawakala wa FBI wakifika na kumthibitishia Biggs utambulisho halisi wa Cutter. Rane anatishia kuwa asipowasiliana na ndege na kuruhusu iondoke, watu wake waliobaki ndani wameelekezwa kuwauwa mateka waliobaki. Mawakala wa FBI wanafanya mpango wa kumrudisha Rane kwenye ndege akisindikizwa na mawakala wawili, wakiwa na mpango wa kumtumia mdungaji riasasi kumtungua Rane na kuruhusu kikosi kuvamia ndege kuwaokoa mateka. Hata hivyo, mdungaji huyo anageuka kuwa Vincent (ambaye alidhaniwa kufa), na anawauwa mawakala wale, lakini yeye pia anapigwa risasi na kuuawa na Cutter, huku Rane akifanikiwa kuingia ndani ya ndege salama. Rane anawaamuru marubani kupaa, wakati Cutter, kwa msaada wa Biggs, anafanikiwa kuruka kutoka kwenye gari lililokuwa kwenye kasi kubwa na kuning'inia kwenye magurudumu ya mbele ya ndege kabla haijapaa kabisa.
Akiwa ndani, Cutter anapambana na wasaidizi wengine wa Rane kabla ya kuingia kwenye mapambano ya ana kwa ana na Rane yenyewe. Risasi inapiga na kuvunja moja ya madirisha ya ndege na kusababisha hewa kupungua kwa kasi kubwa, na mlango mmoja unajifungua kwa kishindo. Cutter anafanikiwa kumsukuma Rane karibu na mlango ulio wazi na kumpiga teke la nguvu akamfanya aanguke kutoka kwenye ndege hadi chini ambapo anakufa. Ndege inarudi kwenye uwanja wa ndege, ambapo mawakala wa FBI wanamdhibiti Sabrina Ritchie, gaidi pekee wa Rane aliyebaki, na mateka waliobaki wanaachiwa huru. Katikati ya pongezi na sherehe, Marti na Cutter wanaondoka zao wakiwa wameshika mikono, lakini si kabla ya Mkuu wa Polisi Biggs kuwapa ofa ya kuwapeleka kwa gari lake.
Washiriki
[hariri | hariri chanzo]- Wesley Snipes kama Mkuu John Cutter, ofisa mkongwe wa usalama aliyebadilika na kuwa mtaalamu wa usalama wa usafiri wa anga, anayesumbuliwa na kumbukumbu za kifo cha mkewe.
- Bruce Payne kama Charles Rane, kiongozi mkatili wa genge la kigaidi la kimataifa na muuza madawa ya kulevya aliyeteka ndege ili kutoroka ulinzi.
- Tom Sizemore kama Sly Delvecchio, rafiki wa zamani wa Cutter ambaye anampa kazi ya ngazi ya juu.
- Alex Datcher kama Marti Slayton, mhudumu wa ndege na mpenzi wa Cutter.
- Bruce Greenwood kama Stuart Ramsey, rais wa kampuni ya ndege ya Atlantic International Airlines.
- Robert Hooks kama Dwight Henderson, wakala wa FBI.
- Elizabeth Hurley kama Sabrina Ritchie, msaidizi mkuu wa Rane na mwanamke pekee kwenye genge lake aliyejifanya mhudumu wa ndege.
- Michael Horse kama Forgét, mfuasi wa Rane.
- Marc Macaulay kama Vincent, mfuasi wa Rane.
- Ernie Lively kama Mkuu Leonard Biggs, sheriff wa eneo hilo.
- Duchess Tomasello kama Bibi Edwards
- William Edward Roberts kama Matthew, mfuasi wa Rane.
- James Short kama Allen
- Joel Fogel kama Dkt. Bauman
- Jane McPherson kama Muuguzi
- Elena Ayala kama Lisa Cutter
- Michael Moss kama Wakala Manning
- Jim McDonald kama Wakala Duncan
- Frank Causey kama Kapteni Whitehurst
- Dennis Letts kama Frank Allen
- Gary Rorman kama Douglas
- Brett Rice kama Polisi
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Gerosa, Melina (1992-11-06). "Fly Hard". Entertainment Weekly. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Mei 19, 2007. Iliwekwa mnamo 2013-02-21.
{{cite magazine}}: CS1 maint: date auto-translated (link)