Nenda kwa yaliyomo

Papa Leo XIV

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Papa Leo XIV
Papa Leo XIV mwaka 2025
AmezaliwaRobert Francis Prevost
14 Septemba 1955
Chicago, Marekani
Elimu
  • Chuo Kikuu cha Villanova
  • Umoja wa Kikatoliki wa Taasisi ya Teolojia
  • Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thomaso wa Aquinas
Kazi yakePapa wa Kanisa Katoliki
AliyemtanguliaPapa Fransisko
DiniUkristo
DhehebuUkatoliki
NdoaHakuna (alifuata useja wa kipadre)
WatotoHakuna
WazaziLouis Marius Prevost
Mildred Martinez
Saini
NemboNembo ya Papa Leo XIV

Papa Leo XIV, O.S.A. (jina la kuzaliwa: Robert Francis Prevost, alizaliwa 14 Septemba 1955) ni kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki na Mtawala wa Mji wa Vatikani. Alichaguliwa kuwa Papa tarehe 8 Mei 2025 kufuatia kifo cha Papa Fransisko. Ndiye Papa wa kwanza kutoka Marekani na Amerika ya Kaskazini kwa ujumla[1]. Akiwa mtawa wa Shirika la Mtakatifu Augustino (O.S.A.), aliwahi kuhudumu katika nyadhifa za juu ndani ya shirika hilo na ndani ya ofisi kuu za Kanisa, zikiwemo Mkuu wa Idara ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa Amerika ya Kilatini.[2]

Kabla ya uchaguzi wake, alijulikana kama kiongozi mwenye busara na msimamo wa wastani, aliyesisitiza malezi ya maaskofu, nidhamu kadiri ya sheria za Kanisa, na utume wa kichungaji. Uchaguzi wake ulionekana kuendeleza mwelekeo wa mageuzi wa Papa Fransisko, hasa kuhusu uteuzi wa viongozi wa Kanisa duniani na kuwapa maeneo uhuru wa kichungaji.

Mbali na Kiingereza, anazungumza Kihispania, Kiitalia, Kifaransa na Kireno, pamoja na kuweza kusoma Kilatini na Kijerumani.

Maisha ya awali na elimu

[hariri | hariri chanzo]

Robert Francis Prevost alizaliwa tarehe 14 Septemba 1955, katika Hospitali ya Mercy iliyoko mtaa wa Bronzeville, Chicago, Illinois, kwa Mildred Martínez, ambaye alikuwa mkutubi, na Louis Marius Prevost, mwanajeshi mstaafu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani aliyeshiriki Vita Kuu ya Pili ya Dunia na msimamizi wa Wilaya ya Shule ya Brookwood 167 huko Glenwood, Illinois. Baba yake alikuwa na asili ya Italia na Ufaransa. Mama yake alikuwa na wazazi wa kichotara kutoka Louisiana, Joseph Martínez kutoka Santo Domingo, Jamhuri ya Dominika-Haiti, na Louise Baquié kutoka New Orleans, ambao walikuwa na asili ya Afrika, Ufaransa, na Hispania. Martínez alikuwa na asili mchanganyiko ya Ki-afrika na Haiti, na Baquié alikuwa mchanganyiko wa Krioli mwenye asili ya Kiafrika. Prevost ana kaka wawili, Louis na John.

Alilelewa huko Dolton, Illinois, kitongoji kilichoko karibu na upande wa kusini wa jiji la Chicago, Prevost alikua katika parokia ya Mtakatifu Maria wa Kupalizwa Mbinguni ambapo alisoma, akaimba kwenye kwaya, na pia aliwahi kuwa mtumishi wa altare. Kaka yake Prevost, John, alieleza kuwa alitamani kuwa padri tangu akiwa mdogo. Alikamilisha elimu ya sekondari katika Seminari ya Upili ya Mtakatifu Augustino, seminari ya awali, iliyoko katika Jumba la Felt huko Holland, Michigan, mwaka wa 1973, ambapo alipata Barua ya Pongezi kwa ubora wa kitaaluma, akiwa mara kwa mara kwenye orodha ya heshima, na pia alihudumu kama mhariri mkuu wa kitabu cha mwaka, katibu wa Baraza la Wanafunzi, na mwanachama wa Jumuiya ya Kitaifa ya Heshima. Pia alishiriki kwenye hotuba na midahalo.

Prevost alipata Shahada ya Sayansi katika Hisabati pamoja na diploma katika Falsafa kutoka Chuo Kikuu cha Villanova huko Philadelphia, Pennsylvania, kilichoanzishwa na watawa Waaugustino, mwaka 1977. Mwaka wa kwanza wa Prevost kama mwana wa shirika la Mt. Agostino, kanda ya Mama wa Shauri Jema, ujulikanao kama mwaka wa unovisi, ulifanyika katika kanisa la Immaculate Conception huko St. Louis, Missouri, kuanzia tarehe 1 Septemba 1977. Aliweka nadhiri zake za kwanza mnamo Septemba 1978 na nadhiri za daima mnamo Agosti 1981. Alipata Shahada ya Uzamili ya Divinity kutoka Catholic Theological Union huko Chicago (1982), na mnamo Juni 19 alifanywa na Askofu Mkuu Jean Jadot kuwa kasisi katika Kanisa la Mt. Monika huko Roma.

Prevost alihudumu kama mwalimu wa fizikia na hisabati katika Shule ya Upili ya Mtakatifu Rita wa Cascia huko Chicago wakati akisoma katika Catholic Theological Union hadi kupata Shahada ya Uzamili katika Sheria za Kanisa (1984).

Mnamo 1985 alitumwa katika misheni ya Waaugustino huko Peru alipohudumu kama Katibu mkuu wa jimbo la Chulucanas na paroko wa kanisa kuu la Familia Takatifu ya Nazareti huko Chulucanas hadi mwaka 1986. Mnamo 1987 alipata kwa maksi za juu (magna cum laude) Shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa kutoka Chuo Kikuu cha Kipapa "San Tommaso d'Aquino" huko Roma na tasnifu yenye kichwa: "Jukumu la priori wa kanda katika Shirika la Mtakatifu Augustino". Miaka 1987 - 1988 alikuwa mhamasishaji wa miito na mkurugenzi wa misheni ya kanda yake.

Mnamo 1988 alikuwa tena Peru, ambapo alitumia miaka kumi akiongoza seminari ya Waaugustino huko Trujillo, akifundisha Sheria za Kanisa, Patrolojia na Maadili katika seminari ya jimbo "San Carlo na San Marcello". Katika kipindi hichohicho pia alikuwa mkuu wa masomo ya seminari ya jimbo, mkurugenzi wake kwa mwaka mmoja, jaji wa mahakama ya Kanisa ya mkoa, mwanachama wa baraza la washauri wa Jimbo Kuu la Trujillo, akitoa huduma za kichungaji katika maeneo ya pembezoni mwa jiji hilo kama mwanzilishi wa parokia ya Mama wa Kanisa, leo parokia ya Mt. Rita wa Cascia, kutoka 1988 hadi 1999 na msimamizi wa parokia ya Mama wa Mungu wa Montserrat kutoka mwaka 1992 hadi 1999. Pia alikuwa priori wa jamii kutoka 1988 hadi 1992.

Mnamo 1998, Prevost alichaguliwa kuwa priori wa kanda wa Shirika la Mtakatifu Augustino kwa Jimbo la Mama Yetu wa Ushauri Mwema lililoko Chicago, na alianza rasmi kazi hiyo tarehe 8 Machi 1999. Mnamo mwaka 2000, aliruhusu padri Mwaugustino James Ray, ambaye alisimamishwa kushiriki huduma ya hadharani tangu 1991 kwa tuhuma za kuaminika za unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto, kuishi katika nyumba ya watawa ya St. John Stone huko Chicago chini ya uangalizi, baada ya makazi ya awali kukataliwa na bodi ya mapitio ya dayosisi kwa sababu ya ukaribu wake na shule ya parokia ya Mtakatifu Thomas Mtume. Ray alihamishwa mwaka 2002 kufuatia utekelezaji wa sheria kali zaidi zilizowekwa na maaskofu wa Marekani.

Mnamo 14 Septemba 2001 alichaguliwa kuwa mkuu wa Shirika la Mt. Augustino duniani, jukumu ambalo alilichukua kwa miaka 12, hadi tarehe 4 Septemba 4. Katika jukumu hilo pia alikuwa msimamizi mkuu wa Taasisi ya Patrolojia Augustinianum ya Roma. Baadaye aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa mafunzo katika nyumba ya watawa ya Mtakatifu Augustino huko Chicago, na pia mshauri wa kwanza na makamu wa mkuu wa kanda ya Mama wa Shauri Jema. Chuo Kikuu cha Villanova kilimtunuku Shahada ya Heshima ya Uzamivu wa Binadamu mwaka 2014.

Askofu na Kardinali

[hariri | hariri chanzo]

Tarehe 3 Novemba 2014 Papa Fransisko alimteua kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo la Chiclayo na Askofu wa jimbojina la Sufar. Tarehe 7 mwezi huohuo alichukua umiliki wa dayosisi hiyo mbele ya Balozi wa Papa nchini Peru, James Patrick Green, na chuo cha washauri.

Alipokea daraja ya uaskofu tarehe 12 Desemba katika Kanisa Kuu la Santa Maria huko Chiclayo kutoka kwa Askofu Mkuu Green, akiwa na askofu mstaafu wa Chiclayo, Jesús Moliné Labarta, na askofu mkuu wa Ayacucho, Salvador Piñeiro García-Calderón, kama wawekaji wakfu wenza. Kama kauli mbiu yake ya kiaskofu alichagua maneno ya Kilatini yaliyotamkwa na Mtakatifu Augustino katika mahubiri ya Ufafanuzi wa Zaburi 127: In Illo Uno Unum ("Ndani Yake [Kristo, sisi] tu mmoja"). Mnamo Agosti 2015 alipata rasmi uraia wa Peru.

Kuanzia Machi 2018 hadi Januari 2023 alikuwa makamu wa pili wa rais wa Baraza la Maaskofu la Peru. Ndani ya chombo hicho alikuwa pia rais wa tume ya utamaduni na elimu na mjumbe wa baraza la uchumi.

Tarehe 15 Aprili 2020 Papa Fransisko pia alimteua kuwa msimamizi wa kitume wa jimbo la Callao, jukumu aliloshikilia hadi tarehe 26 Mei 2021. Huko Vatikani alikuwa mshiriki wa Idara ya Makasisi tangu 13 Julai 2019 na wa Idara ya Maaskofu tangu 20 Novemba 2021.

Tarehe 30 Januari 2023, Papa Fransisko alimteua kuwa Mkuu wa Idara ya Maaskofu na Rais wa Tume ya Kipapa kwa Amerika ya Kilatini, wakati huohuo akimpa hadhi ya Askofu Mstaafu wa Chiclayo. Akaanza kushikilia nyadhifa zote mbili tarehe 12 Aprili 2023, akimrithi Kardinali Marc Ouellet, ambaye alijiuzulu baada ya kufikia kikomo cha umri.

Prevost alichaguliwa kuwa Papa tarehe 8 Mei 2025 katika mkutano wa uchaguzi wa Kipapa wa mwaka 2025, na hivyo kuwa Papa wa kwanza kutoka Marekani na Peru. Alizingatiwa kuwa mgombea wa kushangaza akilinganishwa na wagombea maarufu zaidi, na pia alikuwa mshirika wa Papa Fransisko na mtu ambaye angeweza kuwa chaguo la maridhiano. Wafuasi wake walidai kuwa alisimamia "msimamo wa kati wenye heshima." Baada ya kukubali kuchaguliwa kwake, ambayo ilifanyika katika duru ya nne ya upigaji kura, Prevost aliwakumbatia makardinali alipokuwa akitoka katika Kikanisa cha Sisto IV.

Dominique Mamberti, Kardinali shemasi mzee, alitangaza Habemus Papam kutoka kwenye roshani kuu ya Basilika la Mt. Petro, akitangaza jina la Prevost na jina lake la Kipapa kuwa Leo wa Kumi na Nne (Leo XIV). Prevost alionekana akiwa amevaa vazi la Papa la jadi la stola nyekundu juu ya mozzetta, mavazi ambayo hayakuvaliwa na Papa Fransisko alipoteuliwa mwaka 2013. Kisha alitoa hotuba yake ya kwanza kwa Kiitalia na Kihispania, na kutoa baraka Urbi et Orbi kwa Kilatini. Vatikani ilimtambulisha kama Papa wa kwanza kutoka Shirika la Mtakatifu Augustino na Papa wa pili kutoka Amerika (baada ya Papa Fransisko). Prevost pia ni Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kaskazini, Papa wa kwanza aliyezaliwa Marekani, raia wa kwanza wa Peru na Marekani (kupitia uraia wa nchi mbili), Papa wa kwanza kutoka nchi inayozungumza Kiingereza tangu Adrian IV katika karne ya 12, Papa wa kwanza kuitwa Leo tangu Leo XIII (18781903), wa kwanza kuzaliwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, na Papa wa 267 kwa jumla.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]
  1. Christian; Lauren; Olivia; Maureen. "First American Pope". www.edition.cnn.com (kwa Kiingereza). CNN. Iliwekwa mnamo 2025-05-09.
  2. "Biography of Pope Leo XIV, born Robert Francis Prevost". www.vaticannews.va (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2025-05-09.