Panya-nyasi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Panya-nyasi
Panya-nyasi wa Neumann (Arvicanthis neumanni)
Panya-nyasi wa Neumann (Arvicanthis neumanni)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Chordata (Wanyama wenye ugwe wa neva mgongoni)
Ngeli: Mamalia (Wanyama wenye viwele wanaonyonyesha wadogo wao)
Oda: Rodentia (Wanyama wagugunaji)
Nusuoda: Myomorpha (Wanyama kama panya)
Familia: Muridae (Wanyama walio na mnasaba na panya)
Nusufamilia: Murinae (Wanyama wanaofanan na vipanya-miiba)
Jenasi: Arvicanthis
Lesson, 1842
Ngazi za chini

Spishi 7:

Panya-nyasi ni wanyama wagugunaji wa jenasi Arvicanthis katika nusufamilia Murinae ya familia Muridae ambao wanatokea Afrika kusini kwa Sahara katika nyika na savana mpaka nyanda za juu.

Maelezo[hariri | hariri chanzo]

Panya-nyasi ni wakubwa kiasi. Urefu wa mwili ni sm 9-21 na wa mkia ni sm 22-32. Uzito ni g 48-130. Manyoya ni kahawia, hudhurungi au kijivu. Tumbo lina rangi isiyoiva kuliko mgongo. Mara nyingi kuna mlia mgongoni. Panya hao wana meno laini ya mbele na magego ya ajabu, kama mawe ya kusagia.

Makazi[hariri | hariri chanzo]

Wanaishi katika nyika, savana na makazi yanayohusiana. Wanapatikana sana katika Bonde la Naili, lakini hawapo katika maeneo ya misitu. Huko Ethiopia hufikia hadi urefu wa m 3700. Hula mbegu, majani, nyasi na pengine wadudu na hukiakia wakati wa mchana. Wanaishi katika vishimo vilivyojengwa chini ya mizizi ya miti, vichaka au mawe makubwa au katika vichuguu.

Ekolojia[hariri | hariri chanzo]

Wakati mwingine wanyama hao wana milipuko ya idadi (inayojulikana kwa lemingi). Mwanzoni mwa miaka ya 1970 kulikuwa na panya-nyasi wengi katika Hifadhi ya Serengeti mpaka mtu hangeweza kusonga bila kukanyaga mnyama. Wanyama walio hai walijilisha kwa waliokufa. Mnamo 1976-1977 kulikuwa na hali kama hiyo huko Saheli. Uwepo wao mkubwa unawafanya wanyama muhimu wa kuwinda: katika sehemu kadhaa za Afrika wako karibu 25% ya mawindo ya bundi-mabanda. Pia huliwa na nguchiro, mbweha, nyoka na shakivale.

Spishi hizo ni wanyama wa kijamii. Huishi katika vikundi vyenye madume na majike kadhaa. Jozi kadhaa zinaweza kuzaa wachanga kwa wakati mmoja katika kikundi. Wakati wa hali nzuri wachanga wanaweza kuzaliwa mwaka mzima, ingawa wachanga hawazaliwi wakati wa kiangazi kwa kawaida. Kwa wastani wachanga watano huzaliwa kwa wakati mmoja. Hunyonya muda wa wiki tatu na huwa na uwezo wa kupandana baada ya miezi mitatu. Majike hukaa katika kikundi chao, huku madume wakiondoka katika kikundi chao kwa kawaida. Ingawa panya-nyasi mmoja aliye kifungoni alifikia umri wa miaka sita na nusu, porini kwa kawaida hufikia tu miezi kumi hadi miezi ishirini kwa kiasi juu kabisa.

Katika eneo la msambao wao panya hao huchukuliwa kuwa hatari kwa uchumi. Wakati wa mlipuko wa idadi wanaweza kusababisha hasara kubwa. Labda pia ni waambukizaji wa magonjwa na waliambukiza tauni huko Misri kwa mfano.

Spishi[hariri | hariri chanzo]

Picha[hariri | hariri chanzo]