Nenda kwa yaliyomo

Nzige mwekundu

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nzige mwekundu
Nzige mwekundu
Nzige mwekundu
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Orthoptera (Wadudu wenye mabawa nyofu)
Nusuoda: Caelifera (Wadudu kama panzi)
Familia: Acrididae (Panzi)
Nusufamilia: Cyrtacanthacridinae
Jenasi: Nomadacris
Uvarov, 1923
Spishi: N. septemfasciata
(Audinet-Serville, 1839)

Nzige wekundu ni wadudu wa familia ya panzi inayoitwa Acrididae katika oda Orthoptera ambao wana mabawa ya nyuma yaliyo mekundu kwa msingi wao. Wakiwa wachache wanaishi kama panzi wakubwa, lakini wakiwa wengi sana hujikusanya katika makundi makubwa na kusafiri mbali ndefu hadi km 30 kwa siku. Tauni za nzige wekundu zinatishia uzalishaji wa kilimo katika sehemu za Afrika, k.m. Madagaska, Tanzania na nchi zinazoizunguka, na zamani pia delta ya ndani ya Mto Niger nchini Mali. Sikuhizi tauni za nzige huyu zimepungua.

Mzunguko wa maisha

[hariri | hariri chanzo]

Mzunguko wa maisha wa nzige wekundu una hatua nane au tisa: yai, hatua 6 (au 7 katika awamu ya upweke) za tunutu, wanaojulikana kama warukaji, na mpevu mwenye mabawa. Kupandana hufanyika wakati dume aliyekomaa anaporuka juu ya mgongo wa jike aliyekomaa na kumbokora mwili wake kwa miguu. Manii huhama kutoka ncha ya fumbatio ya dume kwenda ncha ya ile ya jike, ambapo huhifadhiwa. Mchakato huo unachukua masaa kadhaa na uingizwaji mmoja wa manii unatosha kwa idadi ya vibumba vya mayai.

Kisha jike hutafuta udongo laini unaofaa kwa kutaga mayai yake. Lazima uwe na joto sahihi na kiwango kizuri cha unyevu na kuwa karibu na majike wengine wanaotaga. Anachunguza udongo kwa fumbatio yake na kuchimba kishimo ambacho ndani chake anaweka kibumba cha mayai kilicho na mayai 50-200 kwa awamu ya upweke na 20-100 kwa awamu ya makundi. Kibumba cha mayai kina urefu wa sm 3 hadi 4 na ncha ya chini ni takriban sm 10 chini ya uso wa ardhi. Mayai yamezungukwa na povu na hii inakauka mpaka kuwa utando na kuziba kishimo juu ya kibumba cha mayai. Mayai huchukua unyevu kutoka kwa udongo unaozunguka. Kipindi cha kuatamia kabla ya kujiangua kwa mayai kinaweza kuwa siku 24-36 kulingana na nyuzijoto.

Baada ya kutoka kwenye yai tunutu mpya huanza kujilisha mara moja na, akiwa kwa awamu ya makundi, anavutiwa na tunutu wengine na wanajikusanya. Wakati wa ukuaji anahitaji kuambua ngozi (kuacha kiunzi-nje chake) mara kwa mara. Ganda lake gumu la nje linapasuka na mwili wake unatanuka wakati kiunzi-nje kipya bado ni chororo. Hatua kati ya maambuaji zinaitwa “instars” na tunutu wa nzige mwekundu hupitia maambuaji sita (au saba) kabla ya kuwa mpevu mwenye mabawa. Tunutu wa awamu ya kukaa pamoja huunda makundi yanayojilisha, kukota jua na kusonga mbele katika vikosi vinavyoshikamana, wakati wale wa awamu ya upweke hawaundi makundi.

Baada ya uambuaji wa sita au saba mdudu anasemekana kuwa mpevu lakini bado hajakomaa kabisa. Kwanza ana rangi ya nyekundu hafifu na hawezi kuzalisha mayai au manii. Kufikia ukomavu kunaweza kuchukua wiki mbili. Halafu kipindi cha pumziko la kukomaa (diapause) kinafuata ili kupitia msumo wa ukavu. Wakati huo rangi yao inaiva. Urefu wa mchana ukipungua nzige hukomaa kingono. Mwanzo wa msumo wa mvua wako tayari kupandana na kutaga mayai.

Ekolojia na kuunda makundi

[hariri | hariri chanzo]

Nzige wekundu wana awamu mbili: awamu ya upweke ("solitaria") na awamu ya makundi ("gregaria") (polyphenism). Imeonyeshwa kuwa tunutu na wapevu wa nzige wanaweza kutenda kama gregaria ndani ya masaa machache baada ya kuwekwa katika hali ya msongano, ingawa mabadiliko ya kimofolojia huchukua maambuaji kadhaa ili kuonekana. Nzige wa gregaria wanahitaji kizazi kimoja au zaidi ili kuwa solitaria wakikuzwa katika upweke.

Kuna tofauti katika mofolojia na mwenendo kati ya awamu hizo mbili. Katika awamu ya solitaria tunutu hawaundi makundi lakini huzunguka peke yao. Rangi yao kwanza ni kijani, lakini hatua zinazofuata zinaweza kuwa hudhurungi ikiwa uoto kijani huadimika au kukosekana. Wapevu wa solitaria huruka usiku na kuwa hudhurungi ili kufichika katika mazingira yao.

Katika awamu gregaria tunutu hujikusanya pamoja. Hatua ya kwanza ni nyeusi,lakini zile zinazofuata hupata rangi za njano na nyekundu pamoja na mabaka meusi. Wapevu wasiokomaa ni wekundu hafifu na waliokomaa ni kahawianyekundu iliyoiva. Wanaruka wakati wa mchana katika makundi mazito.

Kwa kawaida nzige wekundu huzaliana katika maeneo yenye nyasi ndefu yanayofurikwa kwa muda kila mwaka. Mayai yanatagwa mwanzo wa msumo wa mvua na tunutu hujitokeza kabla ya mafuriko. Maji yalipoingia hukaa juu ya mabua ya nyasi. Sasa, badiliko kutoka kwa panzi wa solitaria kwenda kwa nzige mlafi wa gregaria inatukia kwa kawaida wakati ambapo maji yanakauka na tunutu wanalazimishwa kukaa katika “visiwa” vya nyasi kijani. Kwa sababu ya msongano tunutu wanakutana na kugusana mara nyingi, ambayo husababisha mfululizo wa mabadiliko ya metaboliki na ya mwenendo. Wanaanza kutoa feromoni nyingine inayovutia wenzake na rangi inaanza kubadilika. Baada ya vizazi viwili ndani ya hali hizi panzi wamekuwa nzige kabisa.

Feromoni ya tunutu ni tofauti na ile ya wapevu. Wanapofunuliwa na feromoni ya wapevu, tunutu huchanganyikiwa na kufadhaika, kwa sababu inaonekana kwamba hawawezi kunusana, ingawa vichocheo vya kuona na kugusa vinabaki. Baada ya siku chache makundi ya tunutu hutengana na wale wanaotoroka umbuai huwa solitaria tena. Katika nzige-jangwa ni vilevile na kwa hivyo wanasayansi kadhaa wamejaribu kutumia sehemu kuu ya feromoni ya nzige huyu, benzyl cyanide, ili kusababisha tunutu wa gregaria wakuwe solitaria. Lakini matokeo ya majaribio uwandani walisikitikisha na kemikali hii ilizingitiwa kuwa sumu mbaya. Kwa hivyo mbinu huo wa udhibiti ulisuswa.

Wakati wa vipindi vya utulivu, vinavyoitwa vipindi vya mapungufu, nzige wekundu hutokea tu maeneo kadhaa ya nyasi ndefu, hasa Bonde la Rukwa, Ikuu-Katavi na Malagarasi nchini Tanzania, Bonde la Zambezi na Tambarare za Simalaha nchini Zambia, Tambarare ya Chilwa na Bonde la Shire nchini Malawi, Caprivi nchini Namibia, Mto Chobe nchini Botswana na kusini kwa Madagaska. Lakini baada ya miaka kadhaa ya hali nzuri za kuzaa na hali za kusongamanisha wapevu wanaunda makundi makubwa na kuondoka maeneo yao ya kuzaliana. Halafu wanaweza kuvamia maeneo yanayozunguka hadi nchi zinazopakana.

Makundi ya nzige wekundu huruka juu ya upepo kwa takriban kasi ya upepo. Yanaweza kupita km 20-30 kwa siku na yataruka hadi mamia ya m juu ya ardhi. Hawawezi kusafiri umbali kama nzige-jangwa na hakuna ripoti za kuvuka bahari kwa nzige wekundu, hata Mlangobahari wa Msumbiji. Walakini lazima waliuvuka zamani sana, kwa sababu wanapatikana Madagaska.

Makundi hayo si makubwa kama makundi ya nzige-jangwa, hata hivyo yanaweza kufunika makumi ya km² na kuwa na zaidi ya nzige milioni kwa km². Nzige wa kundi la km² 50 wana uzito wa karibu na tani 100. Kulingana na nzige-jangwa, nzige wekundu hupendelea nyasi, zile ndefu hasa, kama Echinochloa, Hyparrhenia na Cyperus. Lakini kwa awamu ya makundi hula mimea aina nyingi, pamoja na mazao mengi ya kilimo, kama nafaka, kabichi na miharagwe. Kama nzige-jangwa hula takriban uzito wake wa chakula (±2 g) kila siku.

Udhibiti

[hariri | hariri chanzo]

Kuonya mapema na kudhibiti ili kuzuia milipuko ni mkakati uliopitishwa na nchi zilizoathiriwa na nzige barani Afrika na Asia kujaribu kuzuia tauni za nzige kuendelea na kuenea. Mnamo miaka ya 1920-1930s, udhibiti wa nzige ulikuwa uwanja mkubwa wa ushirikiano wa kimataifa. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) ilitengeneza miradi kadhaa yenye lengo la kubadilishana data kuhusu nzige mwekundu na mikutano ya kimataifa ilifanyika. Milki za kikoloni zilihusika sana katika majaribio haya ya kudhibiti nzige wekundu wasumbufu ambao waliathiri sana sehemu za Afrika.

Nchi za Afrika ya Kusini-Mashariki ziliunda Shirika la Kimataifa la Udhibiti wa Nzige Wekundu la Afrika ya Kati na ya Kusini (IRLCO-CSA). Makao yake makuu ni huko Ndola, Zambia. Huduma zake ni pamoja na kufuatilia hali ya hewa, hali ya kiekolojia na hali ya nzige. Wanatoa jarida la habari la kila mwezi na barua za maonyo ikiwa ni lazima. Shirika lina helikopta moja ili kuchunguza maeneo ya mlipuko na kusaidia operesheni za udhibiti. Ndege hukodishwa kutoka Shirika la Udhibiti wa Nzige-jangwa la Afrika ya Mashariki (DLCO-EA) ili kunyunyizia makundi ya nzige.

Nzige wekundu ni rahisi kudhibiti kuliko nzige-jangwa, kwa sababu maeneo ya kuzaliana ni machache kiasi. Shida ni kwamba ufikiaji wa maeneo hayo yenye kinamasi ni mgumu. Kwa hivyo, kutathmini misongamano ya nzige wekundu si rahisi, lakini helikopta ya IRLCO inasaidia nayo. Hakuna matatizo ya usalama kama kwa nzige-jangwa, lakini rasilimali ya kifedha ya uchunguzi na udhibiti inakosa mara nyingi katika nchi zinazoathiria.

Kwa sasa njia kuu ya kudhibiti uvamizi wa nzige-jangwa ni kutumia viuawadudu, haswa fosfati ogania kama fenitrothion, malathion na chlorpyrifos. Hivi vinapulizwa kwa vipimo vidogo vya ukolevu wa juu kwa vyombo vya kupulizia vilivyopandishwa kwenye ndege kwa viwango vya matumizi vya mjao wa chini kabisa (ultra-low volume au ULV). Mdudu hupata kiuawadudu moja kwa moja au kupitia uokotaji wa sekondari (yaani kukanyaga au kula mabaki kwenye mimea). Udhibiti hufanywa na mashirika ya serikali katika nchi zilizoathirika pamoja na msaada wa IRLCO-CSA na DLCO-EA.

Nzige mwekundu ana maadui wa asili kama vile nyigu na nzi mbuai, nyigu vidusia, lava wa mbawakawa, ndege na watambaazi. Hao wanaweza kuwa na ufanisi katika kudhibiti idadi ya wadudu wa solitaria lakini wana athari ndogo dhidi ya nzige wekundu wa gregaria kwa sababu ya idadi kubwa sana ya wadudu katika makundi ya wapevu na ya tunutu.

Sikuhizi mashamba hayavamii na tunutu wa nzige mekwundu mara nyingi. Kwa hivyo, wakulima hawajaribu kuwadhibiti kwa kawaida. Kwa kisa cha makundi ya wapevu, wakulima hujaribu kuogofya nzige mbali na mashamba yao kwa kufanya kelele, kuchoma tairi au njia nyingine. Hii inaelekea kuhamisha shida kwenye mashamba jirani, na makundi ya nzige yanaweza kurudi tena kwa urahisi kwenye mashamba yaliyotembelewa hapo awali.

Dawa za kibiolojia

[hariri | hariri chanzo]

Dawa za kibiolojia zinajumuisha kuvu, bakteria, uto wa mbegu za mwarobaini na feromoni. Ufanisi wa dawa nyingi za kibiolojia ni sawa na ule wa dawa za kemikali za kawaida, lakini kuna tofauti. Kwa ujumla dawa za kibiolojia huchukua muda mrefu zaidi kuua wadudu, magonjwa ya mimea au magugu, kwa kawaida kati ya siku 2 na 10.

Kuna aina mbili za dawa za kibiolojia, biokemikali na vijidudu. Dawa za biokemikali ni sawa na kemikali zinazotokea kwa asili lakini zina sumu isiyo kali sana au hazina sumu, kama vile feromoni zinazotumiwa kupata wenzake wa jinsia nyingine. Dawa za kibiolojia zenye vijidudu zina bakteria, kuvu, miani au virusi ambayo inatokea kwa asili au imebadilishwa vinasaba. Kuvu viuawadudu hukandamiza wasumbufu kwa uambukizaji kwa ujumla: kusababisha ugonjwa ambao ni maalum kwa wadudu.

Bidhaa za udhibiti wa kibiolojia zimekuwa zikiendelewa tangu miaka ya mwisho ya tisini, haswa bidhaa zilizo na kuvu ya asili iliyo pathojeni wa wadudu (yaani kuvu inayoambukiza wadudu), Metarhizium acridum. Spishi za Metarhizium zinaenea duniani kote na zinaambukiza vikundi vingi vya wadudu, lakini zinaonyesha hatari ndogo kwa wanadamu, mamalia wengine na ndege. M. acridum inaambukiza tu panzi wenye vipapasio vifupi, kikundi ambacho nzige ni wana wake, na kwa hivyo imechaguliwa kama kiambato kiamilifu cha bidhaa hizo. Ni salama mno kwa sababu haitoi sumu kama hufanya spishi nyingine za Metarhizium.

Bidhaa inayopatikana sasa katika Afrika na Asia ya Kati, inaitwa NOVACRID, inayozalishwa nchini Maroko (tazama LUBILOSA). Bidhaa nyingine, Green Muscle, ilipatikana hapo zamani lakini ikatoweka kutoka soko, wakati leseni ya uuzaji ilipewa kampuni nyingine ambayo haikuwa na hamu. Bidhaa hiyo zinatumika kwa njia ile ile kama dawa za kikemikali, lakini haziui haraka kama zile. Kwa vipimo vilivyopendekezwa kuvu inaweza kuchukua wiki mbili hadi tatu kuua hadi 90% ya nzige. Kwa sababu hiyo inashauriwa kutumiwa hasa dhidi ya tunutu. Wale wa nzige mwekundu hupatikana zaidi katika maeneo ya nyasi ndefu, mbali na maeneo ya mazao, ambapo kuchelewesha kwa kifo hailetei uharibifu wa mazao. Faida ya bidhaa ni kwamba zinaathiri panzi na nzige tu, ambayo hufanya ziwe salama sana kuliko viuawadudu vya kikemikali. Hasa, inaruhusu maadui wa asili wa nzige na panzi kuendelea na kazi yao ya faida. Hao wanajumuisha ndege, nyigu vidusia na mbuai, nzi vidusia na spishi fulani za mbawakawa. Ingawa maadui wa asili hawawezi kuzuia tauni, wanaweza kupunguza marudio ya milipuko na kuchangia udhibiti wao. Dawa za kibiolojia zinapendekezwa hasa kutumika katika maeneo ya mazingira nyeti kama hifadhi za kitaifa au karibu na mito na miili mingine ya maji.