Nenda kwa yaliyomo

Nzige-miti

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nzige-miti
Nzige-miti wa Saheli
Nzige-miti wa Saheli
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Animalia (Wanyama)
Faila: Arthropoda (Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila: Hexapoda (Wanyama wenye miguu sita)
Ngeli: Insecta (Wadudu)
Ngeli ya chini: Pterygota (Wadudu wenye mabawa)
Oda: Orthoptera (Wadudu wenye mabawa nyofu)
Nusuoda: Caelifera (Wadudu kama panzi)
Familia: Acrididae (Panzi)
Nusufamilia: Cyrtacanthacridinae
Jenasi: Anacridium
Uvarov, 1923
Ngazi za chini

Spishi 12 na nususpishi 2:

Nzige-miti ni wadudu wa familia ya panzi inayoitwa Acrididae katika oda Orthoptera ambao hula majani ya miti, migunga na vikwata hasa, na wana mabawa yenye baka jeusi au mabawa (karibu na) meusi. Spishi nyingi ni panzi wakubwa tu, lakini kadhaa zinaweza kuwa nzige, k.m. Anacridium melanorhodon na A. rubrispinum. Wadudu wa spishi hizi wanaishi kama panzi wakubwa wakiwa wachache, lakini wakiwa wengi sana hujikusanya katika makundi makubwa kiasi na kusafiri umbali wa hadi km 50 kwa siku. Kinyume na nzige wengine wanaoruka mchana, nzige-miti huruka usiku. Hawasababishi tauni lakini wanaweza kuleta hasara kwa kiwango cha kikanda, k.m. katika ukanda wa sumughu nchini Sudani.

Mzunguko wa maisha

[hariri | hariri chanzo]

Mzunguko wa maisha wa nzige-miti una hatua nane hadi kumi kulingana na spishi: yai, hatua 6-8 za tunutu, wanaojulikana kama warukaji, na mpevu mwenye mabawa. Katika nzige-miti wa Misri madume wana hatua 6 kwa kawaida lakini majike wana 7 au 8, labda kwa sababu hawa ni wakubwa zaidi.

Baada ya kupandana jike hutaga mayai chini ya miti ambayo wanakula majani yao. Hivyo tunutu wakitoka katika mayai wako karibu na chakula chao. Lazima udongo uwe na joto sahihi na kiwango kizuri cha unyevu. Anachunguza mchanga kwa fumbatio yake na kuchimba kishimo ambacho ndani chake anaweka kibumba cha mayai kilicho na mayai 30-150 kulingana na spishi na hali ya afya ya jike. Kibumba cha mayai kina urefu wa sm 5 hadi 8.5 na ncha ya chini ni takriban sm 10 chini ya uso wa ardhi. Mayai yamezungukwa na povu na hii inakauka mpaka kuwa utando na kuziba kishimo juu ya kibumba cha mayai. Mayai huchukua unyevu kutoka kwa mchanga unaozunguka. Kipindi cha kuatamia kabla ya kujiangua kwa mayai kinaweza kuwa siku 15-65 kulingana na spishi na nyuzijoto. Kipindi hiki ni kirefu hasa katika nzige-miti wa Misri (siku 30-60), labda kwa sababu wanaishi katika eneo la nyuzijoto za chini kiasi. Kipindi ni kifupi kwa kulinganisha katika nzige-miti wa Saheli (15-25) na cha kati katika nzige-miti kusi (20-30).

Baada ya kutoka kwenye yai tunutu mpya hupanda miti ya kando na kujilisha mara moja na, akiwa kwa awamu ya makundi, anavutiwa na tunutu wengine na wanajikusanya. Wakati wa ukuaji anahitaji kuambua ngozi (kuacha kiunzi-nje chake) mara kwa mara. Ganda lake gumu la nje linapasuka na mwili wake unatanuka wakati kiunzi-nje kipya bado ni chororo. Hatua kati ya maambuaji zinaitwa “instars” na tunutu wa nzige-miti hupitia maambuaji sita hadi manane kabla ya kuwa mpevu mwenye mabawa. Tunutu wa awamu ya kukaa pamoja huunda makundi yanayojilisha, kukota jua na kusonga mbele katika vikosi vinavyoshikamana, wakati wale wa awamu ya upweke hawaundi makundi.

Baada ya uambuaji wa mwisho mdudu anasemekana kuwa mpevu lakini bado hajakomaa kabisa. Kufikia ukomavu kunaweza kuchukua wiki mbili au zaidi. Wapevu wa nzige-miti wa awamu wa makundi ni weusi kuliko wale wa awamu ya upweke ambao wana rangi na ruwaza zinazofanana na gome la miti ambayo wanakula majani yao. Kama nzige wengine wapevu wa nzige-miti wana kipindi cha pumziko (diapause) ili kupitia wakati wa ukame (wale wa Saheli) au baridi (wale wa Misri na wa kusi). Kichocheo cha kuingia kipindi hiki ni kufupisha kwa masaa ya mchana.

Ekolojia na kuunda makundi

[hariri | hariri chanzo]

Spishi kadhaa za nzige-miti wana awamu mbili: awamu ya upweke ("solitaria") na awamu ya makundi ("gregaria") (polyphenism). Imeonyeshwa kuwa tunutu na wapevu wa nzige wanaweza kutenda kama gregaria ndani ya masaa machache baada ya kuwekwa katika hali ya msongano, ingawa mabadiliko ya kimofolojia huchukua maambuaji kadhaa ili kuonekana. Nzige wa gregaria wanahitaji kizazi kimoja au zaidi ili kuwa solitaria wakikuzwa katika upweke.

Kuna tofauti katika mofolojia na mwenendo kati ya awamu hizo mbili. Katika awamu ya solitaria tunutu hawaundi makundi lakini huzunguka peke yao. Rangi yao kwanza ni kijani, lakini hatua zinazofuata zinaweza kuwa hudhurungi ikiwa uoto kijani huadimika au kukosekana. Wapevu wana rangi ya kamafleji na pronoto yao ni juu. Pia wana mabawa mafupi na miguu mirefu kwa kulinganisha. Huruka usiku peke yao.

Katika awamu ya gregaria tunutu hujikusanya pamoja. Hatua ya kwanza ni nyeusi, lakini zile zinazofuata hupata rangi ya manjano na madoa na mabaka meusi. Wapevu wana mabawa marefu zaidi na miguu mifupi zaidi na pronoto ni bapa. Hawa ni wembamba na wafupi kiasi. Huruka usiku katika makundi.

Nzige-miti hupatikana kwenye maeneo ambapo miti yao ya chakula ipo. Wanapandana juu ya miti hiyo na kutaga chini yao. Tunutu hula majani ya miti hiyo hiyo. Ikiwa majani mabichi ya miti hiyo imekuwa michache, tunutu husongana juu ya majani yanayobaki. Kwa sababu ya msongano huo tunutu wanakutana na kugusana mara nyingi, ambayo husababisha mfululizo wa mabadiliko ya metaboliki na ya mwenendo. Wanaanza kutoa feromoni nyingine inayovutia wenzake na rangi inaanza kubadilika. Baada ya vizazi viwili ndani ya hali hizi panzi wamekuwa nzige kabisa.

Wakati wa vipindi vya utulivu, vinavyoitwa vipindi vya mapungufu, nzige-miti hutawanyika kama panzi kwenye maeneo ya miti yao ya chakula. Lakini baada ya miaka kadhaa ya hali mbaya husongana kwenye miti iliyo bado na majani mabichi, mara nyingi miti ya migunda kama vikwata-sumughu, k.m. nchini Sudani. Hapo wanabadilika kuwa nzige wa kweli.

Makundi ya nzige-miti huruka usiku. Kwa sababu ya hiyo huitwa sari al-layl (ساري الليل) nchini Sudani. Wanaweza kusafiri km makumi hadi zaidi ya 100. Wakuzaji wa vikwata-sumughu wanaweza kulala usiku bila nzige na kuamka asubuhi kupata miti inayojaa nao. Nzige hawa hula majani ya miti, aina za vikwata na migunga hasa, kama kikwata-sumughu (Senegalia senegal) na mgunga mwekundu (Vachellia seyal). Wanaweza kuvamia migunda ya miti ya matunda, k.m. wakati wanaporuka kwa makundi, kama familia ya michungwa (Citrus spp.), familia ya mifyulisi (Prunus spp.), mitende (Phoenix dactylifera), miembe (Mangifera indica) na mipera (Psidium guajava). Hata mazao mengine hushambuliwa, kama mpamba (Gossypium spp.), mizabibu (Vitis spp.), mtama (Sorghum bicolor) na mwele (Cenchrus americanus).

Udhibiti

[hariri | hariri chanzo]

Nzige-miti hasababishi tauni lakini anaweza kuleta hasara kikanda. Shughuli kubwa za udhibiti hazifanywi mara nyingi. Nchini Sudani, nzige-miti wa Saheli mara kwa mara hudhibitiwa kwa ndege na nzige-miti Arabu pia katika eneo la Ziwa Turkana nchini Kenya. Kusini mwa Afrika, nzige-miti kusi wakati mwingine hudhibitiwa na nzige-miti wa Misri mara nyingi hudhibitiwa katika eneo la Mediteranea. Udhibiti unafanywa na mashirika ya serikali iwapo kuna uvamizi mkubwa wa mashamba ya kibiashara. Vinginevyo, wakuzaji wa miti wanapaswa kudhibiti nzige wenyewe.

Udhibiti wa nzige-miti ni mgumu kiasi, kwa sababu wadudu wapo juu kutoka ardhi. Kuwadhibiti kwa ndege au helikiopta ni bora, lakini ikiwa hizi hazipatikani inabidi watu watumie kipulizaji mgongoni chenye injini ili kupuliza dawa juu sana. Kwa sasa njia kuu ya kudhibiti uvamizi wa nzige-miti ni kutumia dawa za kikemikali, haswa fosfati ogania kama fenitrothion, malathion na chlorpyrifos. Hivi vinapulizwa kwa vipimo vidogo vya ukolevu wa juu kwa vyombo vya kupulizia vilivyopandishwa kwenye ndege kwa viwango vya matumizi vya mjao wa chini kabisa (ultra-low volume au ULV). Mdudu hupata kiuawadudu moja kwa moja au kupitia uokotaji wa sekondari (yaani kukanyaga au kula mabaki kwenye mimea).

Dawa za kibiolojia

[hariri | hariri chanzo]

Dawa za kibiolojia zinajumuisha kuvu, bakteria, uto wa mbegu za mwarobaini na feromoni. Ufanisi wa dawa nyingi za kibiolojia ni sawa na ule wa dawa za kemikali za kawaida, lakini kuna tofauti. Kwa ujumla dawa za kibiolojia huchukua muda mrefu zaidi kuua wadudu, magonjwa ya mimea au magugu, kwa kawaida kati ya siku 2 na 10. Bidhaa inayopatikana sasa katika Afrika na Asia ya Kati inaitwa NOVACRID na hiyo ina kuvu ya kipathojeni Metarhizium acridum ndani yake. Kuvu hii ilijaribiwa kwa mafanikio dhidi ya nzige wa miti. Kwa maelezo zaidi soma makala kuhusu nzige-jangwa.