Nyumba ya Sanaa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mlango wa kuingia Nyumba ya Sanaa

Nyumba ya Sanaa ni duka maalumu kwa ajili ya wasanii wa Tanzania kuonyesha na kuuza kazi zao za sanaa walizobuni wao wenyewe. Mwanzilishi wa Nyumba ya Sanaa ni Sr. Jean Pruitt ambaye ni Sista anayefanya kazi na shirika la Maryknoll sisters chini ya kanisa Katoliki nchini Tanzania.

Historia ya Nyumba ya Sanaa[hariri | hariri chanzo]

Nyumba ya Sanaa ilianzia shughuli zake mtaa wa Mansfield uliopo nyuma ya kanisa kuu la Mtakatifu Joseph. Sr. Jean Pruitt alianzisha Nyumba ya sanaa mwaka 1971 pale Mtaa wa Mansfield, baada ya kukusanya vijana na kuanza kufanya kazi za sanaa. Wazo hili la Sr. Jean lilizaa matunda na kazi za sanaa zilizokuwa zinafanywa na vijana kuonekana na jamii pamoja na Taifa. Baada ya kazi zilizokuwa zinafanywa na vijana chini ya Sr. Jean Puitt kuonekana zina manufaaa zaidi kwa Taifa la Tanzania, Nyumba ya Sanaa ilizinduliwa na Mwalimu J.K.Nyerere mwaka 1972 hapo hapo mtaa wa Mansfield. Katika harakati za kuipanua Nyumba ya Sanaa Sr. Jean Pruitt alisaidia kupatikana kwa wafadhili kwa ajili ya kujenga jengo ambalo lingeweza kuchukua wasanii wengi kwani ofisi ya mtaa wa Mansfield ilikuwa ndogo. Mwalimu J.K.Nyerere alitoa kiwanja kilichopo makutano ya barabara za Alli Hassani Mwinyi na Ohio na Nyumba ya Sanaa ikajengwa hapo. Jengo hili jipya la Nyumba ya Sanaa lilianza kujengwa mwaka 1981, na lilizinduliwa rasmi na Mwalimu J.K.Nyerere mwaka 1982. Na mwaka uliofuata 1 Mei 1983 wafanyakazi walihamia jengo hili jipya llilopo Upanga mtaa wa Ohio wakitokea mtaa wa Mansfield. Sr. Jean Pruitt alianzisha Nyumba ya Sanaa kama sehemu ambayo vijana wasanii watabuni na wataonyesha kazi zao za sanaa ili ziweze kutambulika kitaifa na kimataifa na kuziuza ili waweze kuondokana na umasikini. Ndani ya nyumba ya Sanaa maonyesho mbalimbali ya kitamaduni huonyeshwa na ni eneo muhimu ambapo unaweza kuona ngoma mbalimbali za kitamaduni za jamii mbalimbali za Tanzania.

Msanii Patrick Francis akimuonyesha Prince Charles wa Uingereza picha ambayo ni moja ya kazi alizofanya alipotembelea Nyumba ya Sanaa 1982

Wasanii Maarufu waliotokana na Nyumba ya Sanaa[hariri | hariri chanzo]

Nyumba ya Sanaa imeibua vipaji vya wasanii wengi sana kwa upande wa uchoraji na utengenezaji wa nguo za Batik. Miongoni mwa wasanii maarufu wajulikanao kitaifa na kimataifa walioibuliwa pale Nyumba ya Sanaa ni George Lilanga, Francis Patrick Imanjama, Augustino Malaba, Robino Ntila n.k.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Nyumba ya Sanaa