Nenda kwa yaliyomo

Nostra Aetate

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kutokana na mchanganyiko wa watu ambao siku hizi unaongezeka mahali pengi, Mtaguso wa pili wa Vatikano uliona haja ya kutoa tamko juu ya uhusiano wa Kanisa Katoliki na dini mbalimbali ili kujenga umoja kadiri ya mpango wa Mungu.

Hati hiyo ilitolewa tarehe 28 Oktoba 1965 kwa kura 2221 dhidi ya 88 za washiriki wa mtagusoi huo. Ina hadhi ya "tamko" tu na kuitwa kwa Kilatini "Nostra Aetate", yaani "Wakati Wetu".

Tamko hilo linasema kwanza juu ya dini za kimila, halafu juu ya dini zilizoendelea pamoja na elimu (k.mf. Ubaniani na Ubudha): Kanisa linaheshimu dini hizo, ambazo ni tofauti sana na ya kwake, ila linazidi kuwatangazia wote kuwa Yesu ndiye njia, ukweli na uzima.

Katika nafasi ya pekee unasifiwa Uislamu kwa tunu zake nyingi. Mtaguso mkuu ukizingatia magomvi ya zamani kati ya Wakristo na Waislamu umewahimiza wote kusahau yaliyopita na kuanza kuelewana na kushirikiana.

Mwishoni tamko linasifu Israeli likihimiza wote kufahamiana vizuri na Wayahudi na kuacha kuwalaumu kwa makosa wasiyonayo. Kanisa linalaani dhuluma yoyote dhidi yao ambao toka zamani wameteswa mno hata na Wakristo na kwa visingizio vya Kiinjili. Kumbe bado ni wapenzi wa Mungu, na Wakristo wanalishwa na utomvu wa mizizi yao.

Basi ni wajibu kuondoa ubaguzi wowote na kujenga udugu ili tuwe kweli wana wa Mungu.

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]