Nenda kwa yaliyomo

Nasaba ya Romanov

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Nasaba ya Romanov (kwa Kirusi: Рома́нов) ilikuwa nasaba ya kifalme ya pili na ya mwisho kutawala Urusi. Ilitawala kuanzia mwaka 1613 hadi 1917[1].

Jina la familia lilitokana na mkabaila Mrusi Roman Yurievich Zakharyin. Binti yake Anastasiya Romanovna alikuwa mke wa Tsar Ivan IV na kwa njia hiyo familia ya Romanov iliongezewa heshima na umuhimu katika Urusi.

Baada ya kifo cha Tsar wa mwisho wa nasaba ya Rurik na kipindi cha vurugu, bunge la makabaila wa Urusi lilimchagua Mikhail Romanov, mpwa wa Anastasia, kuwa tsar wa Urusi. Alikuwa tsar wa kwanza wa nasaba mpya ya Romanov.

Mtoto wake wa kwanza Alexei I aliimarisha utawala wa nasaba na kupanusha milki katika Siberia hadi mipaka ya China. Alifuatwa na mtoto wake Peter I aliyejaribu kubadilisha utamaduni wa nchi na kukaribia Ulaya akiunda pia mji mkuu mpya ya Peterburg kwenye mwambao wa Bahari ya Baltiki.

Baada ya kifo cha Peter I kwenye mwaka 1725 kulikuwa na ufuatano wa watawala wadhaifu na wengine walishindwa kuzaa warithi. Hatimaye utawala ulifika mkononi mwa tsarina (malkia) Elizabeth, binti mmojawapo wa Peter I. alitawala nchi hadi mwaka 1762. Ilhali mwenyewe hakuolewa wala kuzaa watoto, alimteua mpwa wake Peter wa Holstein-Gottorp, mwana wa dadaye na mtawala mdogo Mjerumani, kuwa mrithi wake. Kwa Peter alimchagua tena binti Mjerumani aliyepokea jina la Katharina baada ya ndoa.

Alipokufa Elizabeth, Peter III alikuwa tsar. Miezi michache baadaye mke wake Katharina alimpindua kwa msaada wa jeshi akaendelea kutawala kama Tsarina Katharina I wa Urusi.

Wafuasi wake mara nyingi hutajwa pia kama nasaba ya Holstein-Gottorp lakini waliamua kuendelea kutumia jina la Romanov.

Katharina I alifuatwa na mwanawe Paulo I aliyeuawa na wanajeshi wake. Mtoto wake Aleksander I alishiriki katika vita za Napoleoni, mara kushirikiana naye, mara kumpinga na kushambuliwa naye. Akishiriki katika ushindi juu ya Napoleoni, aliweza kupanusha milki yake kwa kuteka sehemu kubwa ya Poland na kuchukua cheo cha mfalme wa Poland pia akashinda vita dhidi ya Uajemi na Milki ya Osmani. Mdogo wake Nikola I aliendelea kupanusha milki na kusaidia mabadiliko ya uchumi lakini alisitisha harakati zote za kushiriki wananchi katika utawala. Kwenye Vita ya Krim alishindwa.

Mwanawe Aleksander II walijaribu kuleta matengenezo katima mfumo wa kisiasa. Alifuta hali ya nusu-utumwa kwa wakulima wa Urusi na kuwaweka huru. Aliandaa kuanzisha halmashauri ya kushiriki naye katika serikali. Hatimaye aliuawa na mgaidi mwenye mwelekeo wa uanakisti.

Mtoto wale Aleksander III hakukubali matengenzo ya babake akilenga kutetea mamlaka kuu ya tsar katika serikali ya nchi. Aliondoa majaribio yote ya kuleta demokrasia pia alongeza vizuizi dhidi ya Wayahudi (sehemu kubwa ya wakazi magharibi mwa milki yake).

Tsar wa mwisho alikuwa Nikola II aliyepinduliwa mwaka 1917. Alianzisha matengenezo kadhaa; baada ya Urusi kushindwa katika vita dhidi ya Japani alipaswa kukubali bunge la kwanza. Maka 1914 aliamua kusimama upande wa Serbia dhidi ya Austria-Hungaria, hivyo alishiriki katika kuanzisha Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Kutokana na hali mbaya ya Urusi vitani, alipinduliwa na uasi wa watu wa Sankt Peterburg na kukamatwa. Baada ya ushindi wa Wakomunisti katika mvurugo wa Mapinduzi ya Urusi aliuawa pamoja na watoto wake.

  1. "Romanov Dynasty". New World Encyclopedia. http://www.newworldencyclopedia.org/entry/Romanov_Dynasty. Retrieved 2009-06-20.