Nenda kwa yaliyomo

Mzunguko wa hedhi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Mzunguko wa mwanamke)

Mzunguko wa hedhi ni mfululizo wa mabadiliko ya kiasili katika uzalishaji wa homoni na muundo wa mfuko wa uzazi (uterasi) pamoja na ovari kwenye mfumo wa uzazi wa mwanamke, yanayowezesha ujauzito kutokea. Mzunguko wa ovari hudhibiti utengenezaji na utolewaji wa yai pamoja na mzunguko wa kutolewa kwa homoni za estrogeni na projesteroni. Mzunguko wa uterasi huandaa na kudumisha ukuta wa mfuko wa uzazi ili kuweza kupokea kiinitete. Mizunguko hii hutokea kwa pamoja na kwa uratibu, na kwa kawaida hudumu kati ya siku 21 hadi 35, huku wastani wake ukiwa siku 28. Menarche (kuanza kwa hedhi ya kwanza) mara nyingi hutokea takribani katika umri wa miaka 12; na mizunguko ya hedhi huendelea kwa takribani miaka 30–45.

Homoni zinazotokea kiasili ndizo huendesha mizunguko hii; kupanda na kushuka kwa homoni ya kuchochea vifuko vya mayai (Follicle Stimulating Hormone – FSH) huchochea utengenezaji na ukuaji wa oosaiti (seli za yai ambazo bado hazijakomaa). Homoni ya estrojeni huichochea ngozi ya ndani ya mfuko wa uzazi (endometriamu) kunenepa ili iwe tayari kupokea kiinitete endapo utungisho utafanyika. Mtiririko wa damu katika ukuta huo ulionenepa hutoa virutubisho kwa kiinitete kilichopandikizwa kwa mafanikio. Endapo upandikizaji hautatokea, ukuta huo huvunjika na damu hutoka. Tukio hili, linalochochewa na kushuka kwa viwango vya projesteroni, ndilo husababisha hedhi (maarufu kama *period*), ambayo ni mchakato wa kurudia kwa kupoteza ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi, na ni ishara kwamba mimba haikutokea.

Kila mzunguko hutokea kwa awamu kulingana na matukio yanayotokea aidha kwenye ovari (mzunguko wa ovari) au kwenye mfuko wa uzazi (mzunguko wa uterasi). Mzunguko wa ovari unahusisha awamu ya folikula, ovulesheni, na awamu ya lutea; mzunguko wa uterasi unahusisha awamu ya hedhi, ukuaji wa ukuta wa uterasi (proliferative phase), na awamu ya usiri (secretory phase). Siku ya kwanza ya mzunguko wa hedhi ni siku ya kwanza ya kuona damu ya hedhi, ambayo hudumu takribani siku 5. Karibu siku ya kumi na nne, yai kwa kawaida hutolewa kutoka kwenye ovari.

Mzunguko wa hedhi unaweza kusababisha wanawake wengine kupata dalili za mshindo wa kabla ya hedhi (premenstrual syndrome – PMS) zenye ishara kama vile maumivu ya matiti na uchovu. Dalili kali zaidi zinazoweza kuathiri maisha ya kila siku hujulikana kama ugonjwa wa kabla ya hedhi wenye madhara makubwa (premenstrual dysphoric disorder – PMDD), na huwapata takribani asilimia 3–8 ya wanawake. Katika siku za mwanzo za hedhi, wanawake wengine hupata maumivu ya hedhi (period pain) yanayoweza kuenea kutoka tumboni hadi mgongoni na kwenye mapaja ya juu. Mzunguko wa hedhi unaweza pia kubadilishwa kwa kutumia vidhibiti mimba vya homoni.

Mizunguko na Awamu za Mzunguko wa Hedhi

[hariri | hariri chanzo]

Mzunguko wa hedhi unaongozwa na mizunguko miwili inayofanyika kwa wakati mmoja na kwa uratibu, yaani mzunguko wa ovari na mzunguko wa uterasi.[1]

Mzunguko wa ovari unahusisha mabadiliko yanayotokea kwenye ovari kwa lengo la kuzalisha na kuachia yai, na unagawanyika katika awamu tatu [2]

1) Awamu ya folikula (follicular phase): Huanza siku ya kwanza ya hedhi na hudumu hadi ovulesheni. Katika kipindi hiki homoni ya kuchochea vifuko vya mayai (FSH) huendeleza ukuaji wa vifuko vya ovari, huku estrojeni ikiongezeka na kuandaa ukuta wa mfuko wa uzazi.

2) Ovulesheni (ovulation): Hutokea takribani katikati ya mzunguko (siku ya 14 katika mzunguko wa wastani wa siku 28). Utolewaji wa ghafla wa homoni ya luteinizing hormone (LH) husababisha yai kukomaa na kuachiliwa kutoka kwenye ovari.

3) Awamu ya lutea (luteal phase): Baada ya ovulesheni, ngozi ya kifuko cha yai kilichopasuka hubadilika kuwa corpus luteum ambacho hutoa projesteroni na kiasi cha estrojeni. Homoni hizi hudumisha ukuta wa uterasi. Endapo yai halitachavushwa, corpus luteum huharibika na viwango vya homoni hupungua, hali inayopelekea kuanza kwa hedhi.

Mzunguko wa uterasi unahusisha mabadiliko yanayotokea kwenye endometriamu (ukuta wa mfuko wa uzazi) na unagawanyika katika awamu tatu [3]

1) Awamu ya hedhi (menstrual phase): Huanza siku ya kwanza ya kutokwa damu ya hedhi (takribani siku 1–5). Kushuka kwa viwango vya projesteroni na estrojeni husababisha ukuta wa uterasi uliokuwa umetengenezwa kuvunjika na kutoka nje pamoja na damu.

2) Awamu ya ukuaji (proliferative phase): Huanza baada ya hedhi (takribani siku 6–14). Estrojeni huchochea ukuta wa endometriamu kukua na kunenepa upya ili kujiandaa kwa uwezekano wa ujauzito.

3) Awamu ya usiri (secretory phase): Hutokea baada ya ovulesheni (takribani siku 15–28). Projesteroni kutoka corpus luteum hufanya endometriamu kuwa nene zaidi na tajiri kwa virutubisho ili kuiandaa kwa upandikizaji wa kiinitete. Ikiwa upandikizaji hautatokea, kushuka kwa projesteroni husababisha kuanza kwa awamu ya hedhi na mzunguko mpya.

Kwa wastani, mzunguko wa hedhi hudumu kwa siku 28, lakini unaweza kuwa kati ya siku 21–35 kutegemea tofauti za kimaumbile kati ya wanawake.

Athari na Changamoto Zinazohusiana na Mzunguko wa Hedhi

[hariri | hariri chanzo]

Ingawa ni mchakato wa kawaida na wa kiasili, wanawake wengine hupata dalili za kabla ya hedhi (premenstrual syndrome – PMS) zenye ishara kama vile chunusi, maumivu ya matiti, na uchovu [4] . Dalili kali zaidi zinazoweza kuathiri maisha ya kila siku hujulikana kama ugonjwa wa kabla ya hedhi wenye madhara makubwa (premenstrual dysphoric disorder – PMDD), ambao huwapata takribani asilimia 3–8 ya wanawake.

Dismenorea (dysmenorrhea), inayojulikana pia kama maumivu ya hedhi, hutokea katika siku za mwanzo za hedhi na hujionyesha kama mikakamao ya tumbo inayoweza kusambaa hadi mgongoni na kwenye mapaja ya juu. Maumivu makali na yanayodhoofisha si ya kawaida, na mara nyingi huwa dalili ya hali mbaya zaidi kama vile endometriosis. Tatizo hili linaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa afya na ubora wa maisha ya wanawake, lakini uingiliaji wa mapema unaweza kuboresha maisha yao.

Kuna imani potofu za kitamaduni kwamba mzunguko wa hedhi huathiri kwa kiwango kikubwa hisia za wanawake, husababisha msongo wa mawazo, hasira au kuwafanya waonekane wachafu. Mara nyingi mabadiliko ya kawaida ya hisia hupewa maelezo yasiyo sahihi kwa kuhusishwa na hedhi. Tafiti nyingi bado ni dhaifu, lakini kuna ushahidi mdogo unaoonyesha ongezeko dogo la mabadiliko ya hisia katika awamu ya lutea na ya hedhi, huku kupungua kukionekana katika sehemu nyingine za mzunguko [5].

Mabadiliko ya viwango vya estrojeni na projesteroni katika mzunguko mzima wa hedhi huathiri mfumo mzima wa mwili, ikiwemo ubongo, metaboli, na mfumo wa misuli na mifupa. Hali hii inaweza kusababisha mabadiliko madogo ya kisaikolojia na mabadiliko yanayoonekana katika utendaji wa michezo wa wanawake, kama vile nguvu za misuli, uwezo wa mazoezi ya pumzi (aerobic) na yasiyo ya pumzi (anaerobic).

Mabadiliko ya ubongo pia yamebainika katika kipindi chote cha mzunguko wa hedhi, lakini hayajathibitishwa kuathiri uwezo wa kiakili, ikiwemo ufanisi wa kitaaluma, utatuzi wa matatizo, na kumbukumbu. Tafiti zingine zinaonyesha maboresho ya uwezo wa kufikiri kwa kutumia nafasi (spatial reasoning) wakati wa awamu ya hedhi, pengine kutokana na kupungua kwa viwango vya estrojeni na projesteroni.

Kwa wanawake wengine, ovulesheni huambatana na maumivu ya kipekee yanayojulikana kama mittelschmerz (neno la Kijerumani likimaanisha “maumivu ya katikati”). Maumivu haya husababishwa na kupasuka kwa kifuko cha yai na hutokana na kupotea kwa kiasi kidogo cha damu.

Hata pale mchakato unapokuwa wa kawaida, mabadiliko ya homoni katika mzunguko wa hedhi yanaweza kuongeza uwezekano wa kuibuka kwa magonjwa ya kinga mwilini (autoimmune diseases), hali inayoweza kuchangiwa na estrojeni kuongeza nguvu ya mfumo wa kinga.

Aidha, takribani asilimia 40 ya wanawake wenye kifafa huripoti ongezeko la msongamano wa degedege katika baadhi ya awamu za mzunguko wa hedhi. Hali hii, inayojulikana kama kifafa cha mzunguko wa hedhi (catamenial epilepsy), huweza kusababishwa na kupungua kwa projesteroni katika awamu ya lutea au mwanzoni mwa hedhi, au ongezeko la estrojeni wakati wa ovulesheni. Matibabu ya hali hii yanaweza kujumuisha kutumia dawa fulani kabla na wakati wa hedhi, kama vile virutubisho vya projesteroni, kuongeza kipimo cha dawa za kifafa anazotumia kwa kawaida, au kuongeza kwa muda mfupi dawa nyingine za kudhibiti kifafa kama vile clobazam au acetazolamide. Endapo njia hizi hazifanyi kazi, au iwapo mzunguko wa mwanamke si wa kawaida, matibabu yanaweza kujumuisha kusitisha kabisa mzunguko wa hedhi, kwa kutumia dawa kama medroxyprogesterone, triptorelin, goserelin, au matumizi endelevu ya vidonge vya kupanga uzazi.

  1. Richards JS (2018). "The ovarian cycle". Vitamins and Hormones (Review). 107: 1–25. doi:10.1016/bs.vh.2018.01.009. ISBN 978-0-128-14359-9. PMID 29544627.
  2. Reed BF, Carr BR, Feingold KR, na wenz. (2018). "The Normal Menstrual Cycle and the Control of Ovulation". Endotext (Review). PMID 25905282. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 28 Mei 2021. Iliwekwa mnamo 8 Januari 2021.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. Salamonsen LA (Desemba 2019). "Women in reproductive science: Understanding human endometrial function". Reproduction (Review). 158 (6): F55–F67. doi:10.1530/REP-18-0518. PMID 30521482.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. Gudipally, Pratyusha R.; Sharma, Gyanendra K. (2022). "Premenstrual Syndrome". StatPearls. StatPearls Publishing. PMID 32809533. Kigezo:NCBIBook2.
  5. Carmichael MA, Thomson RL, Moran LJ, Wycherley TP (Februari 2021). "The impact of menstrual cycle phase on athletes' performance: a narrative review". Int J Environ Res Public Health (Review). 18 (4): 1667. doi:10.3390/ijerph18041667. PMC 7916245. PMID 33572406.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)