Nenda kwa yaliyomo

Mtumiaji:Kituo cha Utamaduni cha Iran Dar es Salaam

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


ASILI YA USHIA

[hariri | hariri chanzo]

ASILI YA USHIA

Maana ya Neno Shia:

Lugha nyingi zina maneno ambayo yana aina mbili za maana: Ile ya asili au ya msingi na ile ya kitaalam au maana ya pili. Neno Shia kiasili linamaanisha mfuasi mmoja, wawili au kikundi cha wafuasi, kwa maana ya kwamba wafuasi wa mtu maalum ni wale wanaomhudumia au kumsaidia yeye katika mambo yake. Ndani ya Qur’ani Tukufu, neno hili linatumika mara nyingi kwa maana hii. Kwa mfano katika 28:15 Mwenyezi Mungu anazungumzia juu ya mfuasi mmoja waNabii Musa kama ni mmoja wa Shia wake. Mahali pengine, Ibrahim (a.s.) anatambulishwa kama Shia wa Nuh (a.s.) [37:83].

Maana ya Kiistilahi ya Neno Shia:

Mwanzoni mwa historia ya Kiislamu, neno Shia lilitumika katika maana yake ya asili au ya kawaida kwa ajili ya wafuasi wa watu mbalimbali. Kwa mfano, baadhi ya hadith zinazungumzia “Shia wa Ali bin Abutalib” na nyinginezo juu ya “Shia wa Muawiya bin Abusufyan.” Hata hivyo, kama tutakavyoona baadaye, neno hili polepole likapata maana ya pili au maana ya kiistilahi; yaani ya wafuasi wa Ali tu, wale ambao wanaamini katika suala la Uimamu wa Ali na kizazi chake, ule uimamu wa kuteuliwa na Mungu na kusimikwa na Bwana Mtume (saww).

Katika makamusi mengi ya Kiarabu, hili neno Shia limeelezewa katika maana zote, za neno kwa neno, yaani tafsiri sisisi, na ile ya kiistilahi, kwa namna ambayo ni rahisi kuona uhusiano uliopo baina ya maana mbili hizo, ya wafuasi kwa jumla na ya wafuasi wa Ali tu. Hali ni hivyo hivyo katika vyanzo vingi vya kitheolojia. Kwa mfano, Abul-Hasan al-Ash’ariy (kafariki 330 A.H.), katika kitabu chake mashuhuri Maqaalat al-Islamiyin wa Ikhtilaaf al-Musallin anaelezea juu ya maana ya kiistilahi, anasema: “Waliitwa Shia kwa sababu tu walimfuata Ali na waliamini kwamba yeye anazo fadhaili nyingi kuliko masahaba wengine wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.)”

Shahristani (kafariki 548A.H.) katika kitabu chake, al-Milal wa Nihal, ambacho ni chanzo maarufu sana kuhusiana na madhehebu tofauti ndani ya Uislamu, anaandika hivi: “Shia ni wale waliomfuata Ali hasahasa na wakaamini juu ya Uimam na ukhalifa wake kwa mujibu wa mafundisho ya wazi na ushuhuda wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.).” Haya ni maelezo sahihi kabisa, kwa vile Shia wenyewe wanaamini kwamba sababu ya kumfuata Ali (a.s.) ni kwamba iliamriwa na kutakiwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na kwamba haukuwa ni uamuzi wao wenyewe wa kuchagua ni nani wamfuate. Kinyume chake, wasio Shia, baada ya kifo cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) wao walimfuata yule aliyechaguliwa katika ukumbi wa Saqifah na waliamini kwamba Mtukufu Mtume aliwaachia watu waamue wenyewe wamfuate nani. Ndani ya kitabu chake Firaq al-Shi’ah, al-Hasan bin Musa al-Nawbakhti, mwanachuoni mashuhuri wa Shia (kafariki 313 A.H.), yeye anaandika: “Shia ni kundi la wafuasi wa Imam Ali ibn Abutalib (a.s.). Walikuwa wakiitwa kwa jina la ‘Shia wa Ali’ wakati wa uhai wa Bwana Mtume (s.a.w.w.) na baada ya kufariki kwake, na wanafahamika kama wafuasi wa Ali na wanaoamini Uimam wake.” Sheikh al-Mufid (kafariki, 423A.H.) mmoja wa wanachuoni wakubwa na mashuhuri wa Shia wa mwanzoni kabisa, anafafanua kuwa Shia ni wale wanaomfuata Ali (a.s.) na wanaoamini urithi wake wa uongozi wa baada tu ya kufariki kwa Mtukufu Mtume. Akielezea kwa nini Shia pia wanaitwa ‘Imamiyah’ yeye anasema: “Hiki ni cheo kwa ajili ya wale wanaoamini juu ya ulazima na umuhimu wa Uimam na muendelezo wake katika zama zote, na kwamba kila Imam ni lazima ateuliwe kwa uwazi dhahiri na lazima awe ni Maasum na mkamilifu.”

Hivyo inaweza kusemwa kwamba Shiani wale wenye imani zifuatazo kuhusu urithi ama uandamizi wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.): 1. Urithi (Uandamizi – Ushikamakamu) wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) unategemea juuya uteuzi wa kimungu. 2. Kwa vile Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliteuliwa na Mwenyezi Mungu, mwandamizi wake, Imam, vilevile ni lazima ateuliwe na Mwenyezi Mungu Mwenyewe na kutambulishwa na Mtume. 3. Yule mrithi wa mara moja wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alikuwa ni Ali. 4. Uimamu na uongozi wa Uislamu baada ya Ali ni wa kizazi chake kwa utaratibu na uainisho ulioainishwa na Mtukufu Mtume mwenyewe.

Ushia ulianza lini? Hili ni swali ambalo kwa kawaida hujitokeza. Swali hili linaweza kugawanywa katika maswali madogo mawili: 1. Ni lini ilikuwa ni mara ya kwanza kwamba kikundi cha watu kilikuja kuamini juu ya umuhimu wa kumfuata Imam Ali (a.s.) kama mrithi mwandamizi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliyeteuliwa kimungu? Kwa maneno mengine, ni lini wazo la Uimam lilianza?

2. Ni lini neno Shia lilipopata maana yake ya kiistilahi? Kwa maneno mengine, ni lini neno Shia lilianza kutumika kwa wafuasi wa Ali (a.s.) tu na wanaoamini juu ya Uimam wake? Maswali haya ni muhimu sana, ili kuthibitisha kuwa imani ya Shiailikuwa na msingi katika Uislamu katika kipindi cha upatikanaji wa sura yake wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), na kwamba wazo hili na dhana hii ya kitheiolojia na kiimani ya uimamu wa Ali na kizazi chake ilitokana na Uislamu wenyewe kupitia Qur’an na Mtukufu Mtume (saww).

Kuna hadith nyingi sana zilizosimuliwa na wote Shia na wasiokuwa Shia kuhusiana na suala la Uimam, ambazo tutazichunguza baadaye tutakapokuwa tunajadili itikadi za Shia, hata hivyo, kwa sasa tutachunguza tu zile hadith ambamo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alizungumzia kundi la watu kama Shia (wafuasi) wa Ali na kisha turejee kwenye hadith nyingine zaidi na vipengele vya historia ya Uislam, hadithi ambazo zinaweza kutoa mwanga zaidi katika somo la sasa hivi. Hadith zote zilizotajwa hapa chini zinasimuliwa kutoka kwenye vyanzo vinavyoheshimika vya Sunni. Hizo ni sampuli tu ya nini kinachoweza kupatikana katika vyanzo vilivyotajwa hapa na vinginevyo pia.

1. Ibn Asakir (kafariki 571 A.H.) amesimulia kutoka kwa Jabir bin Abdillah al-Ansari kwamba yeye alisema: “Wakati mmoja tulikuwa pamoja na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) pale Ali alipowasili, ambapo Mtukufu Mtume alisema: ‘Naapa kwa Yule ambaye maisha yangu yamo mikononi mwake kwamba hakika mtu huyu na Shia wake watakuwa na furaha katika Siku ya Kiyama,’ na kisha ikashuka Aya hii: “Hakika wale walioamini na kutenda mema, hao ndio wabora wa viumbe.” (98:7). Baadaye, wakati wowote ambapo masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) walipomuona Ali akija, walikuwa wakisema; ‘Mbora wa watu amekuja.’”

2. Al-Suyuti (kafariki 911 A.H.) amesimulia kutoka kwa Ibn Abbas kwamba: “Wakati ile Aya ya (98:7) “Hakika wale walioamini na kutenda mema, hao ndio wabora wa viumbe.” iliposhuka, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Ali (a.s.): ‘Hao ni wewe na Shia wako na katika Siku ya Kiyama mtakuwa radhi na wenye kumridhisha hasa Mwenyezi Mungu.’”

3. Ibn Hajar (kafariki 974 A.H.) amesimulia kutoka kwa Ibn Abbas kwamba: “Wakati ile Aya ya (98:7) “Hakika wale walioamini na kutenda mema, hao ndio wabora wa viumbe.” iliposhuka, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alimwambia Ali (a.s.): ‘Hao ni wewe na Shia wako. Wewe na Shia wako mtatokeza Siku ya Kiyama wakati mkiwa mmeridhia na wenye kumridhisha Mwenyezi Mungu sana, na maadui zako watakuja wakiwa wamechukia na wamekamatwa kwenye shingo zao.’”

4. Ibn al-Athiir (kafariki 774 A.H.) amesimulia kwamba, akimwambia Ali (a.s.), Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Ewe Ali! Wewe na Shia wako mtakutana na Mwenyezi Mungu mkiwa mmeridhika Naye na wenye kumridhisha sana Yeye, na maadui zako watakutana Naye wakiwa wamechukia na watakuwa wameshikwa kwenye shingo zao.” Kisha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) akaonyesha jinsi hili litakavyokuwa kwa kuweka mkono wake juu ya shingo yake mwenyewe.’”

Kuna hadith nyingine ambamo Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.) akiongea na Ali (a.s.) alikuwa akitumia msemo “Shia wetu.” Hili linakubaliana sana na kile kilichoonyeshwa hapo juu, kwamba Shia ni wale wanaomfuata Ali (a.s.) kwa mujibu wa mafundisho ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na sio kwa uamuzi wao binafsi. Kwa mfano, Ibn Asakir amesimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema:

“Hakika kuna mto huko Peponi mtamu zaidi kuliko nekta (majimaji matamu katika maua), laini kuliko siagi, baridi kuliko barafu, na ambao unanukia kuliko miski. Katika kijito hicho kuna udongo wa ufinyanzi (tiinah) ambao kutoka humo sisi (watu wa nyumbani kwangu na mimi mwenyewe) tuliumbwa kutokana nao, na Shia wetu wanaumbwa kutokana na ufinyanzi huo huo.”

Bado kuna hadith zingine ambamo Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) alipokuwa akizungumza na Ali (a.s.) alikuwa akitumia usemi wa “Shia wa kizazi chako.” Hili linathibitisha kile tulichodokezea hapo juu, kwamba Shiani wale wanaomfuata Ali (a.s.) kwa sababu wanaamini katika asasi ya Uimam. Kama tutakavyoona kwa upana zaidi baadaye, Shia wanaamini kwamba Ali (a.s.) alikuwa ndiye Imam wa kwanza, baaada yake Uimam uliendea katika kizazi cha Ali na Fatima, ambao waliteuliwa na Mwenyezi Mungu na kutambulishwa na Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Kwa mfano Zamakhshari (kafariki 538 A.H.) katika Rabiul-Abrar yeye anasimulia kwamba Mtume (s.a.w.w.) alisema: “Ewe Ali! itakapowadia Siku ya Kiyama, mimi nitakuwa nimeshikamana na Mwenyezi Mungu, nawe utakuwa umeshikamana na mimi, kizazi chako watakushikilia wewe na wafuasi wao Shia watawashikilia wao. Halafu utaona tutakapopelekwa.”

Ilikuwa ifahamike kwamba, kwa mujibu wa Qur’ani, utume nao pia unarithiwa. Qur’ani inasema: “Na bila shaka tulimpeleka Nuhu na Ibrahim na katika kizazi chao Unabii na Kitabu …..” (57:26). Hii ina maana kwamba wale ambao walistahiki kuteuliwa kwenye nafasi ya Utume na Mwenyezi Mungu walikuwa wamejumuishwa kwenye kizazi chao. Na ndani ya Qur’ani (2:124) kuna maelezo ya jinsi ambavyo Ibrahim ambaye tayari alikuwa ni Nabii na Khaliilu-llah (rafiki wa Allah) alivyonyanyuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Imam juu ya watu. Kisha yeye Ibrahim akamuomba Mwenyezi Mungu kuuweka Uimam kwenye kizazi chake vile vile. Mwenyezi Mungu alijibu kwamba Ahadi Yake (hapa ikimaanisha Uimam) haitawafikia watu madhalimu. Kwa njia hii Ibrahim alitambua kwamba Uimam utarithiwa na kizazi chake kiadilifu na cha wachamungu.

Kwa nyongeza ya hadithi zilizotajwa hapo juu na za mfano wao, na hadith juu ya Uimam ambazo zitatajwa baadaye, bado kuna sababu nyingine kadhaa za kwa nini kujitokeza kwa kundi la watu kama lile la Shia wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) lilikuwa ni jambo la kawaida na jambo la muhimu vile vile. Kwa mfano, pale mwanzoni mwa Uislamu wakati Mwenyezi Mungu alipomuamuru Mtukufu Mtume kuanza ulinganio wake wa ummah kwenye Uislam kwa kuwaalika jamaa zake wa karibu, Mtukufu Mtume aliwaalika jamaa zake kwenye chakula. Baada ya chakula hicho Mtume alitangaza ujumbe wake na akawaalika wageni wake hao kuukubali Uislamu, na akasema kwamba yeyote atakayeamini Uislam miongoni mwao na akamsaidia yeye basi huyo atakuwa mrithi wake. Wote walikaa kimya. Mtu mmoja pekee aliyekubali mwaliko wa kumsaidia yeye alikuwa ni Ali, aliyekuwa kijana wakati ule. Mtume (s.a.w.w.) akamwambia akae chini kimya na akalirudia ombi lake kwa mara ya pili na ya tatu. Tena na tena alikuwa ni Ali tu aliyeonyesha utayari wake wa kumsaidia Mtume. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) ndipo akaukubali mwitikio wa Ali kwenye mapenzi ya Mwenyezi Mungu na akatekeleza amri ya Mwenyezi Mungu ya kumteua yeye kama mrithi wake. Tukio hili limeandikwa kwenye vyanzo vingi tu.

Katika kauli muhimu sana, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa uwazi kabisa amethibitisha kwamba Ali (a.s.) alikuwa mkweli na aliyeepukana na imani potovu na vitendo visivyo sahihi, iwe ni kwa tabia yake binafsi au katika maneno yake na maamuzi yake na kwa kujitokeza kabisa aliwataka Waislam kumfuata yeye Ali (a.s.). Ummu Salamah amesimulia kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Ali wakati wote yuko na haki na Qur’ani, na ukweli siku zote uko pamoja na Ali, na mpaka Siku ya Kiyama hawatatengana.” Hadith hii maalum imesimuliwa na Ibn Abbas, Abu Bakr, Aisha, Abu Sa’id al-Khudri, Abu Layla na Abu Ayyub al-Ansari vilevile. Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) pia ananukuliwa akisema: “Mwenyezi Mungu ambariki Ali, Mwenyezi Mungu aifanye haki wakati wote kuwa pamoja na Ali.”

Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) vilevile amethibitisha katika nyakati mbalimbali tofauti kwamba Ali (a.s.) ndiye mtu mwenye elimu zaidi miongoni mwa watu wake katika masuala ya kufungamana na elimu na sayansi za Kiislam. Kwa mfano, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) amesema: “Hekima imegawanywa sehemu kumi, tisa zimetolewa kwa Ali na sehemu moja imegawanywa kwa watu wote waliobakia.” Baadaye Khalifa wa pili amesisitiza tena zile hadith za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kusema: “Mwenyezi Mungu asinihuzunishe na tatizo gumu wakati Ali akiwa hayupo.”


Tunahitimisha sehemu hii ya mjadala kwa kurejea kwenye hadith inayojulikana sana ya Ghadir. Akirejea kutoka kwenye Hijja yake ya mwisho ya Makka, Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) aliwataka maelfu ya Waislam waliofuatana naye kusimama hapo njiani. Alisimama kwenye jukwaa au mimbari iliyotengenezwa kwa ajili yake kutokana na matandiko ya vipando na akasema: “Yeyote ambaye amenichukulia mimi kama Mtawala (mawla) wake, basi Ali sasa hivi ni Mtawala wake.” Kisha watu waliokuwa pale, pamoja na wale makhalifa wa kwanza na wa pili wa baadae walitoa kiapo cha utii kwa Ali (a.s.) na wakampongeza. Hadithi hii imesimuliwa na zaidi ya vyanzo mia moja. Kwa ajili ya orodha ndefu ya vyanzo visivyo vya ki-Shia vya hadith hii, angalia majuzuu kadha ya Abaqaat al-Anwaar cha Mir Hamid Husayn al-Hindi (kafariki 1306 A.H.). Hivyo inaelekea kwamba makundi tofauti ya hadithi na pamoja na ushahidi wa kihistoria uliotajwa hapo juu yasingeacha shaka yoyote kwamba wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) Waislam wengi walikuja kumpenda sana Ali, walitafuta usuhuba naye na walidhamiria kumfuata yeye baada ya Mtukufu Mtume (s.a.w.w.). Watu hawa walikuwa mara kwa mara na kwa uwazi zaidi wakiitwa Shia wa Ali, kiasi kwamba neno Shia peke yake lilikuja kuwa sawa na wafuasi wa Ali. Muhimu zaidi wazo na dhana ya Uimam wa Ali na kizazi chake kwa hakika lilianza wakati wa uhai wa Mtukufu Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Kifo cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) kwa kawaida kililileta suala la Uimam kwenye kitovu cha mambo na kuwafanya wale ambao bado waliamini katika umuhimu wa kumfuata Ali (a.s.) kuwa tofauti na Waislam wengine, ambao walikuja kuamini katika uanzishwaji wa Ukhalifa kama wenye kutoa urithi wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) katika kutawala jumuiya ya Kiislam na sio cheo cha kimungu. Akielezea matukio baada ya kifo cha Mtukufu Mtume (s.a.w.w.), al-Mas’ud (kafariki 345 A.H.), mwanahistoria mashuhuri wa Sunni anaandika: “Kwa kweli Imam Ali na wale ambao miongoni mwa Shia wake ambao walikuwa pamoja naye walibakia ndani ya nyumba yake wakati ambapo kiapo kwa Abu Bakr kilipofanywa.”

Matukio ya baadae, kama vile vita vilivyotokea wakati wa Ukhalifa wa Ali (a.s.) na ule msiba wa Karbala ambamo Imam wa tatu wa Shia na watu 72 wa familia yake na wafuasi wake waliuawa yalisaidia umaarufu kwa Shia wa Ali kuvutia uundaji wa utambulisho wa Shia. Kwa mfano tu tunakuta katika moja ya vitabu vya awali kwamba Ali, wakati akimshutumu Talha na Zubeir alisema: “Kwa hakika wafuasi wa Talha na Zubeir huko Basra wamewauwa Shia wangu na mawakala wangu.” Abu Mikhnaf (kafariki 158 A.H.) anasimulia kwamba baada ya kifo cha Muawiyah, Shia walikusanyika kwenye nyumba ya Suleiman bin Surad na yeye akawaambia: “M’awiyah amefariki. Husein (a.s.) amekataa kutoa kiapo cha utii kwa Bani Umayyah na ameondoka kwenda Makka, na ninyi ni Shia wake na Shia wa baba yake.”

Kuna kauli ya kuvutia iliyotolewa na Abu Haatam al-Sijistaanii (kafariki 322 A.H.) ndani ya kitabu chake kiitwacho al-Ziinah: “Neno Shia lilikuwa ni jina la kwanza ambalo lilitokeza katika Uislam kwa ajili ya madhehebu fulani na lilikuwa ni cheo cha masahaba wanne wa Mtukufu Mtume (s.a.w.w.): Abu Dharr, Ammaar, Miqdad na Salman al-Farsii. Wanne hawa pia walikuwa ndio wafuasi wa Ali waliojitokeza sana.” Yeye vilevile anaongezea: “Baadaye, wakati wa vita vya Siffin neno hilo lilitumika kwa wafuasi wote wa Ali (a.s.).”