Nenda kwa yaliyomo

Mtumiaji:FREDRICK VENANCE/ukurasa wa majaribio

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Ujitokezaji wa Tafsiri Zenye Dosari Changamani: Mifano kutoka Tafsiri ya Riwaya ya

Mine Boy (1946) na Mchimba Madini (2021)

Fredrick Venance

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Freddvenn2011@gmail.com

Ikisiri

Makala haya yanalenga kuonesha sababu za matokeo ya tathmini ya tafsiri zenye dosari changamani kama matokeo ya data zikizotokana na tafsiri ya riwaya ya ‘Mchimba Madini’ (2021).  Hii ni tafsiri ya riwaya ya ‘Mine Boy’ (1946) iliyoandikwa na Peter Abrahams. Ni wazi kuwa matokeo yoyote yale ya tafsiri ni vema yakapimwa kwanza kabla ya kuwafikia wasomaji. Lengo likiwa ni kujiridhisha ikiwa mfasiri amefanya kazi iliyo bora kabla ya kuwafikia wasomaji.  Katika Makala haya tumeangazia sababu au mazingira yanayosababisha kutokea kwa matokeo ya tafsiri zenye dosari changamani kama zilivyojitokeza katika riwaya ya Mchimba Madini (2021) iliyotafsiriwa na Ben L.S. Ole Mollel. Katika mchakato wa kufanya tathmini ya tafsiri mbinu kadha wa kadha huweza kutumika. Mbinu hizo ni kama vile mbinu ya kulinganisha matini, mbinu ya kupima uasili, kupima uelewekaji, kupima usomekaji, kufanya rejeshi na kupima ulinganifu. Hivyo basi, makala haya yatakijita katika kuchunguza sababu au mazingira yanayosababisha matokeo ya tathmini ya tafasiri zenye dosari changamani kama zilivyojitokeza katika riwaya ya ‘Mchimba Madini (2021) ambayo ni tafsiri  ya riwaya ya ‘Mine Boy’ (1946).

Dhana za Msingi: Tathmini, Tafsiri zenye Dosari Changamani, Matini ya Kifasihi

1.0 Utangulizi

Tafsiri ni zoezi lenye tija katika jamii kutokana na ukweli kuwa limesadiia kuwaunganisha watu wa mataifa mbalimbali wanaoongea lugha tofauti. Kwa mujibu wa Mwaansoko (2013:43), dai kuwa matini za kifasihi ni ngumu kufasirika ni la ukweli kwa kiwango kikubwa. Matini hizi kwa kawaida huandikwa kisanii kuridhisha na kufurahisha nafasi ya mwandishi bila uzingativu mkubwa wa wasomaji. Pamoja na dhana hiyo, katika zoezi la kutafsiri suala la kufanya tathmini ni jambo lisilokwepeka. Hivyo, ni muhimu kufanyika kwa tathmini ya tafsiri baada ya mchakato mzima wa kutafsiri. Malangwa, 2008 na 2012). Kutathmini ni kuangalia ubora na (au) udhaifu wa jambo fulani. Aidha, kwa mujibu wa TUKI (2019) wanaeleza kuwa kutathmini ni kuangalia kitu au jambo na kuona ubora au udhaifu wake.  Hivyo, kufanya tathmini ya tafsiri ni kuangalia ubora na udhaifu wa matini za tafsiri kabla ya mchakato, wakati wa mchakato na baada ya mchakato wa kuhawilishwa kutoka MC kwenda ML (Mwalangwa, 2012).  Ifahamike kuwa ubora wa MC unapaswa kutathminiwa au kuhakikiwa kwa jinsi matini tafsiri (yaani, matini lengwa) inavyowasilisha ujumbe (Nzyoka, 2014). Tathmini ya tafsiri huweza kufanywa na mzungumzaji mzawa, mhakiki wa tafsiri, mhakiki wa matini, mshauri wa masuala ya tafsiri, mfasiri mwenyewe, mteje alieywasilisha matini inayofasiriwa au mtaalamu katika uwanja husika (Mlangwa, 2012).

Katika mchakato wa kufanya tathmini ya tafsiri zipo mbinu mbalimbai zitumikazo katika kufanya tathmini. Baadhi ya mbinu hizo ni pamoja na mbinu ya kulinganisha matini, mbinu ya kupima uasili, kupima uelewekaji, kupima usomekaji, kufanya rejeshi na kupima ulinganifu (Malangwa, 2012). Baada ya kufanyika kwa mchakato wa tathmini ya tafsiri kwa kutumia mbinu anuai, matokeo kadhaa  hupatikana kulingana na aina ya mbinu iliyotumika katika mchakato wa ufanyaji tathmini.  Hivyo, matokeo ya tafisiri hutupatia matokeo ya aina mbili. Aina hizo ni tafsiri mwafaka na tafsiri zenye walakini. Kwa kuwa lengo la makala haya ni kuchunguza sababu za utokeaji wa matokeo ya tathimini ya tafsiri zenye dosari changamani, ni wazi kuwa kiini cha mjadala wetu unajikita kwenye aina ya pili ya matokeo ya tathmini ya tafsiri ambayo ni tafsiri zenye wakakini.

2.0 Nadharia ya Tafsiri

Nadharia inayoongoza makala haya ni Nadharia ya “Neno kwa neno na Maana kwa Maana”. Mkabala au nadharia ya “neno kwa neno” umejikita katika kuweka msisitizo katika uhamilishaji wa Mawazo ya MC[1] kwenda ML[2] kwa lugha nyingine kwa kuzingatia au kutokuzingatia maana yake kamili. Aidha, tafsiri ya maana hutilia mkazo maana au fahiwa ya matini husika (Mpemba, 2016:24).  Baadhi ya waasisi wa nadharia hii ni pamoja na Horace (20BK) Marcus Tullius Cicero (106- 43 KK) na Mtakatifu Jaome (347-420 BK). Suala linalosisitizwa katika Nadharia ya “Neno kwa Neno” na “Maana kwa Maana” ni ulinganifu.  Kila nadharia hutawaliwa na misingi na kanuni zinazoiongoza nadharia hiyo.  Hivyo, makala haya yataongozwa na misingi mitatu ya nadharia hii kama zilivyoainishwa na Tytler (1790).Tytler anabainisha kanuni tatu za jumla za tafsiri ambazo ni (i) tafsiri lazima ibebe na kuwakilisha kikamilifu mawazo yaliyoko katika MC (ii) Mtindo wa namna ya uandishi wa ML lazima vilingane na mtindo wa namna ya uandishi  katika MC na (iii) Urahisi ulikatika MC uwe ni uleule ulio katika Matini Lengwa ML. Hivyo, ni wazi kuwa mfasiri hapaswi kutumia maneno magumu ambayo hayakutokana na MC (Munday, 2012; Mpemba, 2016).

3.0 Methodolojia

Mbinu iliyotumika katika ukusanyaji wa data za makala haya ni mbinu ya upitiaji wa machapisho mbalimbali. Aidha, machapisho yaliyopitiwa ni pamoja na viabu viwili vya riwaya vya Mine Boy (1946) na Mchimba Madini (2021) zikiwa ni matini zilozotumika katika kufanya tathmini ili kutoa matokeo ya ya uhakiki wa tafsiri. Vyanzo vingine vya data ni majarida na vitabu pamoja na tasnifu. Sabu ya kutumia mbinu hii ni kuwa, vyanzo hivyo ndivyo vilivyotumika katika kutoa data za kutosha katika kujibu tatizo linaloshughulikiwa na makala haya.  Aidha, ni wazi kuwa tafsiri huusu matini iliyoandikwa. Hivyo basi, ni wazi kuwa mbinu hii ni faafu katika kutupatia vyanzo bora vya data zitakazotumika katika makala.

Mkabala utakaotumika katika ufafanuzi wa data za makala haya ni makabala wa kimaelezo au kitaamuli.  Mkabala wa kitaamuli (maelezo) hujikita katika kutoa ufafanuzi na uchambuzi wa data kwa kutumia maelezo kwa kiasi kikubwa na kuliko tarakimu. Hivyo, uteuzi wa mkabala huu umezingatia  sababu ya msingi kuwa aina ya data zilizokusanywa katika makala haya ni data za kimaelezo na si za kitarakimu. Kwa hiyo, mbinu hii ni faafu katika kutoa ufafanuzi wa data zitakazotumika katika makala haya.

3.1 Mbinu za Kutathmini Tafsiri

Baadhi ya wataalamu hueleza kuwa kuna mbinu zipatazo tano ambazo hutumika katika mchakato wa kufanya tathmini ya tafsiri. Malangwa (2012:52) anaainisha mbinu zipatazo sita zitumikazo katika kufanya tathmini ya tafsiri. Mbinu hizo ni kulinganisha matini, kupima uasili, kupima uelewekaji, kupima usomekaji, kufanya rejeshi na kupima ulinganifu. Hata hivyo, makala haya yatajadili kwa uchache kuhusu mbinu moja pekee ambayo ni mbinu ya kulinganisha matini ili kurejelea hali halisi katika mchakato wa tathmini ya tafsiri ya ‘Mchimba Madini’ (2021) kutoka katika matini ya lugha chanzi ya ‘Mine Boy’ (1946).

3.1.1 Mbinu ya Ulinganishaji Matini

Mbinu ya Ulinganishaji Matini ni mbinu kongwe. Hii ni mbinu inayohusisha matini zote mbili katika zoezi la kufanya tathimini (yaani, matini chanzi na matini lengwa) Kwa kawaida mfasiri anapokamilisha zoezi lake la kufasiri matini huchukua tafsiri yake na kuilinganisha na MC. Zoezi hili hufanyika kwa malengo makuu mawili. Mosi, mfasiri hulinganisha matini zake ili kuona kama amefanikiwa kuingiza taarifa zote za MC. Pili, baada ya kuhakiki taarifa, mfasiri hulazimika kuangalia kama ameshughulikia kikamilifu vipengele vyote vya kimuundo. Aidha, mfasiri huhakiki kuona kama taarifa zingine za ziada zimeingizwa katika ML ambazo hapo awali hazikuwepo. Katika kufanya tathmini ya tafsiri kwa kutumia mbinu ya ulinganishaji matini kwa kulinganisha MC, mhakiki au mfasiri wa tafsiri hulazimika kupitia msitari kwa msitari ili kuhakikisha kuwa uhawilishaji wa taarifa zote umefanyika vilivyo. Kwa msingi huo, ni wazi kuwa endapo tafsiri itatolewa pasipo kufanyiwa tathmini inaweza kuwa na upungufu wa taarifa muhimu za MLC[3] na hatimaye kumpotosha msomaji wa MLL[4] (Malangwa, 2012; Mwaipaja, 2022).

4.0 Mazingira ya Ujitokezaji wa Tafsiri Zenye Dosari Changamani

Katika kufanya tathmini au uhakiki wa tafsiri, matokeo ya aina mbili huweza kujitokeza. Matokeo hayo huangukia aidha katika kundi la tafsiri mwafaka au kundi la tafsiri zenye walakini. Miongoni mwa matokeo ya tafsiri zenye walakini ni tafsiri pana, tafsiri finyu, tafsiri tenga na tafsiri zenye dosari changamani. Kwa kuwa makala haya yamelenga kuchunguza mazingira ya ujitokezaji (sababu) kwa matokeo ya tathmini ya Tafsiri zenye Dosari Changamani, ufafanuzi kuhusiana na aina hii ya tafsiri zenye walakini unahitajika.

4.1 Matokeo ya Tathmini ya Tafsiri zenye Dosari Changamani

Wataalamu wengi hukubaliana kwa kueleza kuwa tafsiri ni mchakato wa kuchukua mawazo kutoka lugha moja na kuyaweka badala yake mawazo yanayolingana kutoka lugha nyingine (taz. Catford,1965; Mwansoko na Wenzake, 2013; Mpemba, 2016). Kwa mujibu wa Cambaridge Dictionary (2024), neno ‘changamani’ huashiria hatua ya kitu kinapochukua nafasi juu ya sehemu au kingo za kitu kingineni, yaani hali ya kuvuka mpaka katika kufanya jambo fulani. Hivyo, kwa msingi huo, Tasfiri zenye Dosari Changamani ni aina ya tafsiri ambazo zimejumuisha au kubeba aina tofautitofauti za dosari au makosa. Aidha, Tafsiri zenye Dosari Changamani zinaweza kuelezwa kuwa ni aina ya tafasiri ambayo hurejelea ujitokezaji wa changamoto/dosari mbalimbali za tafsiri (mfano, dosari katika ufafanuzi, tofauti za kitamaduni, kimtazamo) zinapotokea kwa wakati mmoja au kuathiriana, na kufanya mchakato wa tafsiri kuwa mbaya zaidi.

Aina hii ya tafsiri ni matokeo ya matokeo ya tathimini ya tafasiri yanayopatikana baada ya kuwa Matini Lengwa imefanyiwa ukahiki (tathmini) na mfasiri, mhakiki wa tafsiri au mtu mwingine yeyote mwenye taaluma ya tafsiri. Kwa msingi huo basi, makala haya yatajadili sababu kadha wa kadha zinazosababisha kutokea kwa Tafsiri zenye Dosari Changamani kama sehemu ya matokeo ya tathmini ya tafsiri kwa kurejelea mifano kutoka katika riwaya ya Mchimba Madini (2021) ambayo ni tafsiri ya riwaya ya Mine Boy (1946).

4.2. Mazingira ya Ujitokezazi wa Tafsiri zenye Dosari Changamani katika Tathmini ya Tafsriri

Zipo sababu kadha wa kadha zinazoweza kusababisha kutokea kwa tafsiri zisizo muafaka katika mchakato wa kutathmini tafsiri na hivyo kusababisha matokeo yasiyo bora. Onyango (2018) anaeleza kuwa kuna sababu mbalimbali zinazoifanya tafsiri ya matini yoyote kuwa mgumu. Akimrejelea King’ei (1992:70-72) anaelezea sababu zifuatazo zinazochangia kukosekana kwa usahihi katika tafsiri: Mosi, ni kuwepo kwa tafsiri pana na tafsiri finyu ambazo hutokea pale mtafsiri anapokuongeza taarifa za ziada au kushindwa kutafsiri sehemu ya taarifa iliyoko katika matini chanzo. Pili, tofauti za kitamaduni. Tofauti za kitamaduni katika lugha ya chanzi zinaweza kusababisha ugumu katika kutafsiriwa moja kwa moja katika lugha lengwa. Tatu, ni tofauti za lugha katika kigezo cha maneno, muundo wa kisarufi na mfumo wa sauti vinaweza kutofautiana kati ya lugha ya chanzi na ile ya lengwa. Nne ni malengo na matumizi tofauti ya lugha kwa mtafsiri huweza kusababisha kuwa tofauti kati ya malengo na matumizi ya lugha ya mtafsiri na yale ya mwandishi wa maandishi ya chanzi. Tano ni tofauti za kifalsafa baina ya mfasiri na mwandishi wa matini chanzi pale ambapo mmoja anaweza kutumia lugha kwa njia ya alama (symbolically) wakati mwandishi wa matini chanzi anaweza kuitumia kwa njia ya uhalisi (realistically). Sita ni sababu zinazotokana na uandishi duni wa matini chanzi na ukosefu wa ujuzi wa mtafsiri ambao huathiri mchakato wa tafsiri (Onyango, 2018).

Changamoto za kutafsiri riwaya iliyotafsiriwa ‘Mine Boy” kwa Kiswahili zinahusiana na changamoto zilizotajwa na King’ei, hasa athari za lugha na utamaduni wa jamii ya watu wa Afrika Kusini, Kiingereza na Kiswahili, athari za itikadi ya mwandishi, pamoja na changamoto za ufasiri wa aina ya riwaya yenyewe ambazo kwa namna moja ama nyingine zimeweza kujitokeza wakati wa matokeo ya kutathmini tafsiri ya riwaya ya ‘Mchimba Madini’ (2021) na kusababisha kuwapo kwa tafsiri zenye dosari changamani. Zifuatzo ni sababu ama mazingira ya utokeaji wa tafsiri zenye dosari changamani kama zilivyojitokeza katika tathmini ya tafsiri ya ‘Mchimba Madini’ (2021).

4.2.1 Tofauti za lugha katika kigezo cha maneno, muundo wa kisarufi na mfumo wa sauti

Ni ukweli usiopingika kuwa lugha tofauti zina miundo ya sarufi na ujenzi wa sentensi katika namna tofauti. Hivyo, huweza kufanya tafsiri kuwa na ugumu hususasi kama mfasiri atatumia mbinu isiyomwafaka katika kufanya tafsiri. Mathalan, mbinu ya neno kwa neno au aina nyingine ya mbinu ya kutafsiri. Nukuu ifuatayo inatoa mfano wa namna utofauti wa kigezo cha maneno, muundo wa sarufi na mfumo wa sauti unavyoweza kuathiri tafsiri.

Matini ya LC Matini ya LL Tafsiri Mwafaka
The man inclined his heard, but the woman could not see it in the dark (pg. 1.) Yule mtu aliinamisha kichwa chake lakini mwanamke hakumwona kwa sababu ya giza. (uk.1) Yule mtu aliinamisha kichwa chake, lakini wanamke hakuweza kuona hilo katika giza.

Katika sampuli ya tafsiri ya matini lengwa inaonekana kwamba tafsiri ya Kiswahili haikufanyiwa tathmini au imefanyiwa tathmini lakini si kwa umakini unaotakiwa. Sababu za kudondoshwa wa viambishi vinavyounda kirai kitenzi ‘could not’ katika MLC ambazo hazipatikani katika MLL na hivyo, kutoweza kuleta upatanisho wa kisarufi unaosababisha kuongezwa kwa baadhi ya maumbo ya manneo ‘kwa sababu ya’ katika MLL. Aidha, kilichomaanishwa katika kirai kitenzi ‘could not see it’ katika LC chanzi kinarejelea hali ya mwanamke kutokuona tendo la kuinamishwa kwa kichwa lililofanyika katika giza. Halii hii inaweza kusababishwa na baadhi ya wafasiri kupuuza baadhi ya viambishi, maumbo ya maneno au muundo wa tungo katika MLC wakati wa kutafsiri MLL.

4.2.2 Athari za Utofauti wa Kiutamaduni

Zipo baadhi ya dhana katika utamaduni wa Kiingereza ambazo haziwezi kutafsiriwa kwa usahihi kabisa kwa Kiswahili, na kwa hiyo mtafsiri huweza kutumia tafsiri huru kukabiliana na changamoto hii. Mwansoko (2013) anaelezea kuwa tafsiri huru, au tafsiri ya mawasiliano, ni aina ya tafsiri inayolenga msomaji lengwa (hadhira), ambaye hatarajii ugumu wowote katika maandishi ya lugha lengwa. Badala yake, wanatarajia tafsiri rahisi ya dhana za kigeni zilivyo kwa lugha yao, pale inapowezekana. Mtafsiri ana uhuru wa kutafuta maneno au vikundi vya maneno vinavyolingana na methali, misemo, tamaduni na mazingira ya lugha lengwa. Kwa hivyo, ingawa tafsiri ya mawasiliano inafuata kanuni za sarufi ya LL, pia lazima izingatie mfumo wake wa kijamii, kihistoria, kitamaduni na mazingira. Nukuu zifuatazo zinaonyesha jinsi mtafsiri alivyotumia njia hii kushughulikia dhana ngumu kutoka utamaduni wa Kiingereza na kuuweka katika utamaduni wa Kiswahii ambao kwa namna moja unaposha maana kwa baadhi ya dhana kulingana na utamaduni wa Waswahili:

Matini ya LC Matini ya LL Tafsiri Mwafaka
And the Sun was going down they come back and looked to their beer but their beer was gone (pg.11) Jua lilipotua walirudi na kulitafuta tembo lao, halikuwepo (uk.15) Jua lilipozama walirejea na kutafuta kilevi chao, lakini hawakukikuta.

Kutokana na mfano huo utabaini kuwa tafsiri ya Kiswahili katika matini chanzi si sahihi kwani katika utamaduni wa lugha ya Kiswahili, wazungumzaji hawasemi ‘Jua lilipotua’ bali hunasema ‘Jua lilipozama’. Aidha, katika utamaduni wa lugha ya Kiswahili matumizi ya neno ‘beer’ katika Kiingereza kuweza kutumika kama ‘pombe’, ‘kilevi’ au ‘bia’ kama neno lililofanyiwa utohozi kulingana na muktadha wa utamaduni wa namna ya kuita vinywaji. Hivyo, ni wazi kuwa kutokuzingatiwa kwa utamaduni wa lugha lengwa katika ufasiri wa lugha ya Kiingereza kutoka MC kumesababisha kuwapo kwa matokeo yanayobainisha tafsiri zenye dosari changamani.

4.2.3 Athari zitokanazo na Asili ya Aina ya Riwaya

Changamoto chache za kutafsiri Mchimba Madini zinaweza kuelezwa kutokana na asili ya aina ya riwaya yenyewe. Ifahamike kuwa, wakati mwingine kunaweza kutokea makosa yanayoweza kujitokeza wakati wa mchakato wa tathmini ya tafairi ambayo yanatokana na matini asili. (Onyango, 2018). Nukuu ifuatayo inadhihirisha makosa yaliyojitokeza katika MC ambayo yamejidhihirisha pia katika matini lengwa:

Matini ya LC Matini ya LL Tafasiri Mwafaka
“To the best mine boy, Zuma!” To Zuma (Pg, 64) “Kwa afya ya kijana, Zuma, mchimba madini!” Kwa afya ya Zuma (uk. 83) Kwa kijana hodari kabisa wa mgodini! Xuma

Nukuu hizo zinaonesha makosa yaliyofanywa katika MC katika uandishi wa jina la mhusika Xuma ambalo limeandikwa ‘Zuma’. Hii ni dosari ambayo hata hivyo haikuweza kubainishwa na mfasiri wakati wa kufasiri matini ya LC. Hivyo, kusababisha kosa hilo kuonekana katika matini ya LL. Pamoja na hilo, pia kuna upotoshaji wa maana katika matini ya LL kwa kuongeza kirai ‘kwa afya ya kijana’ hali ambayo imesababishwa na kutokuwa na ufafanuzi mzuri wa uteuzi wa neno mwafaka badala ya ‘To Zuma’ ambalo kwa namna moja ama nyingine linapoteza maana na kupoteza uhalisi kwa kile kilichotakiwa kumaanishwa katika matini ya LL.

4.2.4 Uteuzi wa Visawe Usio Faafu katika Lugha Lengwa

Uteuzi usio faafu wa visawe vya Kiswahili vinavyorejelea matendo au majina katika lugha ya Kiingereza unaweza kusababisha kuwapo kwa tafsiri zenye dodari changamani. Data za makala haya zilidhihirisha kuwa, licha ya kuwa lugha ya Kiswahili haina visawe vingi mwafaka vya kurejelea maneno ya lugha ya Kiingereza, lakini kupatikana kwa tafsiri yenye dosari inaweza kusababishwa na kutokuzingatia tu uteuzi wa visawe kutoka katika LL. Mfano ufuatao unaonesha makosa ya uteuzi usio faafu wa viasawe uliofanywa katika muundo wa matini ya LL:

Matini ya LC Matini ya LL Tafsiri Mwafaka
He shifted little bundle from his right hand to his left, (pg. 1) Alikipitisha mkono wa kulia kizigo alichokuwa amekishikilia mkono wa kushoto (uk.1) Alikihamishia mkono wa kulia kifurushi kilichokuwa mkono wa kushoto.
He shifted a little bundle from his left hand to his right   and waited. (pg. 2) Alikirudisha mkono wa kulia kile kizigo na kungoja. (uk. 2) Alikihamisha kile kifurushi kutoka mkono wa kushoto kwenda kulia na kungoja.

Katika nukuu hizo inaonesha kuwa, mfasiri hakuzingatia uteuzi sahihi wa visawe vya maneno, ‘shifted’ na ‘bundle’ katika LL na badala yake kuamua kutumia vibadala ‘kupitisha’ akirejelea dhana ya kutoa kitu kutoka mkono mmoja kwenda mkono mwingine. Aidha, uteuzi wa kisawe nomino ‘kizigo’ kama kisawe cha neno ‘bundle’ haukuwa faafu badala yake alipaswa kutumia kisawe ‘kifurushi’ ili kuendana na muktadha wa mzungumzo na sarufi ya LL. Hali hii huweza kusababisha upotoshaji wa maana. Upotoshaji wa maana ni kitendo cha kubomoa maana ya awali iliyokusudiwa na kuibua maana mpya kwa kuteua visawe tofauti. Upotoshaji wa maana hujitokeza pale mfasiri anapoteua visawe vya LL ambavyo vina maana inayokinzana na neno la LC. Kwa hiyo, upotoshaji wa maana hujitokeza pale panapotokea ukinzani wa maana baina ya MC na ML. (Jilala, 2017).

4.2.5 Tafsri Tofauti ya Malimwengu

Kila jamii ina uelewa tofauti wa malimwengu yake na kuyatafsiri malimwengu hayo kwa namna tofauti na jamii nyingine inavyoweza kuyaelewa na kuyatafsiri. Ilibainika kuwa, tafsiri tofauti ya malimwengu ni moja ya changamoto ya kutafsiri matini za kiutamaduni katika jamii ya LL kwa sababu tafsiri ya Waingereza kuhusu malimwengu yanayowazunguka ni tofauti na jinsi Waswahili wanavyoyafasili maisha yao, mazingira na uzoefu wao. Tatizo hili husababisha mfasiri kushindwa kuhamisha kwa ukamilifu maana ya majina ya mavazi au vyakula yanayotumika katika jamii zaidi ya moja kwa kutumia Kiswahili. Pia, changamoto hii husababisha mtafsiri kuzalisha tafsiri kengeufu kwa sababu ya kushindwa kubaini tofauti ya tafsiri ya malimwengu ya jamii lugha anazozifanyia tafsiri (Jilala, 2017). Data zifuatazo zinabainisha hilo:

Matini ya LC Matini ya LL Tafsiri Mwafaka
Her mouth had slowly opened and a steam of saliva was trickling down on to her dress. (pg. 9) Mdomo wa yule mwanamke ulikuwa wazi na mate yalikuwa yanamtiririkia kwenye nguo yake. (uk. 11) Mdomo wake ulifunguka taratibu huku rundo la mate likiririka juu ya gauni lake

Hata hivyo, inapofika katika tafsiri neno ‘dress’ hutafsiriwa kwa kutumia visawe mbalimbali kutokana na namna linavyotumika katika jamii fulani ya watumiaji wa lugha ya Kiswahili. Matalani, neno ‘dress’ huweza kutafsiriwa kwa Kiswahili kama ‘gauni’ au ‘kanzu’ badala ya kisawe kilichotumika ambacho ni ‘nguo’ ambalo ni neno majumui. Katika mkabala huo, maana na dhima ya vazi hilo katika utamaduni wa LC hupotea na hivyo kusababisha mfasiri kushindwa kulitolea tafsiri iliyokamili na kuleta ungengeushi katika matini ya LL. Aidha, kuna uchopekaji wa kiambishi kirai ‘yule mwanamke ulikuwa wazi’ katika MLL ambavyo kinapoteza maana halisi iliyokusudiwa katika MLC kinachotokana na kufasiri visivyo kirai ‘her mouth had slowly opened’ katika MLL. Hii inachangiwa na kushindwa kuteua maneno muafaka ya kutumia katika kuelezea dhana ya ‘kufunguka taratibu kwa mdomo’ katika muktadha wa watumiaji wa lugha katika jamii ya Waswahili.

4.26 Changamaoto za Kisemantiki

Changamoto za kisemantiki hujidhihirisha katika nyanja tano ambazo ni: kupotea kwa maana, upanuzi wa maana, utata wa maana, upotoshaji wa maana na ufinyu wa maana (Jilala, 2014). Aidha, uelewa, upokezi na utambuzi wa maana na ujumbe wa matini hutofautiana baina ya mtu na mtu, na jamii na jamii. Hoja hii inaenda sambamba na mawazo ya Katani (2004) ambaye katika kubainisha matatizo yanayotokana na kutafsiri maana, ameyagawa matatizo hayo katika nyanja kuu mbili: kwanza, maana haijengwi bali hutafsiriwa kulingana na mtu binafsi na imani muambatano ya utamaduni. Pili, maana hujengwa katika muktadha wa kijamii. Hivyo, maana hujikita katika uelewa wa mtu binafsi na namna jamii inavyotafsiri maana ya neno husika. Tafsiri ya maana ya maneno hutofautiana kutoka jamii moja hadi jamii nyingine. Tofauti hizi hutegemea muktadha, wakati, historia na utamaduni (Jilala, 2014)

Matini ya LC Matini ya LL Tafrisi Mwafaka
A crowd of people formed a ring in the Street (pg.7) Kulikuwa na kikindi cha watu kilichofanya mduara barabarani. (uk. 9) Umati wa watu ulifanya duara katikati ya barabara
The light of the moon streamed into the room. He could see the outline of Eliza near him (pg. 58) Mbalamwezi iliingia chumbani. Aliweza kumwona Eliza karibu naye (uk. 75) Mwangaza wa mwezi uliingia taratibu chumbani. Aliweza kuliona umbo la Eliza lililokuwa karibu naye

Katika nukuu hiyo, maneno, ‘crowd’ na ‘ring’ katika lugha ya MC huweza kufasiliwa kwa namna tofauti na mfasiri kulingana na uelewa wa mtu binafsi na namna jamii linavyolitumia neno hilo katika muktadha fulani. Mathalan, neno ‘crowd’ linaweza kutumika kama ‘umati’katika Kiswahili huku neno ‘ring’ huweza kurejelea duara au kitu chenye umbo la mviringo. Hivyo basi, ikitazamwa kwa kina tafsiri ya maneno hayo mawili na namna yalivyotumika katika MLL wakati mwingine huweza kuzua utata, kupanua maana au kusababisha maana finyu tofauti na ilivyokusudiwa na MLC. Hivyo, matumizi ya neno ‘kikundi’ halikuwa sahihi katika muktadha wa kurejelea neno ‘crowd’ kumaanisha kundi kubwa la watu lililomaanishwa katika MC. Aidha, matumizi ya kirai kitenzi ‘kilichofanya mduara barabarani’ katika MLL badala ya matumizi ya kirai ‘ulifanya duara Katikati ya barabara’ ambacho ndicho sahihi ili kuleta upatanisho wa kisarufi kutokana na dhana ya umati umesababisha kupoteza maana  katika ML. Kutokana  na hali hiyo, wakati mwingine maana huweza kupotezwa na ML na kusababisha kutokueleweka vyema au kuzua utata kwa wasomaji.

5.0 Hitimisho

Makala haya yamejadili kwa kina ujitokezaji wa matokeo ya tathmini ya tafsiri zenye dosari changamani za kutafsiri matini za kifasihi katika katika matini za riwaya ya Mchimba Madini (2021) ambayo ni tafsiri ya riwaya ya Mine Boy (1946). Mjadala wa makala haya unasisitiza kuwa, katika katika mchakato wowote wa kufanya tathmini ya tafsiri, mfasiri anaweza kubaini dosari kadha wa kadha zinazoweza kusababishwa na makosa au changamto tofautitofauti. Kimsingi, changamoto zilizobainishwa katika makala haya ni za kisemantiki, uteuzi wa visawe usio faafu wa katika lugha lengwa, athari zitokanazo na asili ya aina ya riwaya, tafsiri tofauti ya malimwengu, tofauti za lugha katika kigezo cha maneno, muundo wa kisarufi na mfumo wa sauti. Aidha, makala haya yamepambanua mbinu zinazotumika katika mchakato wa kufanya tathmini ya tasfsiri.  Mbinu ambazo huweza kutumika kulingana na kusudi au lengo la kufanya tafsiri husika.

MAREJELEO

Abrahams, P. (1946). Mine Boy. Nairobi: East African Educational Publishers.

Abrahams, P. (2021). Mchimba Madini. Mfasiri B. L. S. Mollel. Nairobi: East African Educational Publishers.

Cambridge (2024). Cambridge Dictionary. Inapatikana: https://dictionary.cambridge.org/ved=2ahUKEwj-grStz.

Catford, J.C. A (1965). Linguistic Theory of Translation. London: Oxford University Press.

Jilala, H. (2017). “Changamoto za Kutafsiri Matini za Kiutamadunikatika Jmii Ulumu: Mifano kutoka Tafsiri ya

                       Majina katika Matini za Kitalii” katika Mwanga wa Lugha Vol. 1(1): Uk. 77-98. Inapatikana:

                        https://journal.mu.ac.ke.com. Imesomwa tarehe 15 Juni, 2015.

_______. (2014). “Matatizo ya Tafsiri katika Matini nchini Tanzania” katika Kioo cha Lugha, Juz.

Malangwa, P. S. (2012). “Mbinu Mbalimbali za Kutathmini Tafsiri” katika Kioo cha Lugha, Juz. 10: Uk.50-69.

                       Inapatikana: https://www.journal.udsm.ac.tz. Imesomwa tarehe 18 Juni 2025.

Mpemba, T. (2016). “Nadharia za Tafsiri na Ukalimani” katika H. Jilala (Mh.)  Nadharia za Tafsiri, Ukalimani na

                     Uundaji wa Istilahi.Uk. 19-51. Dar es Salaam:  Daudi Publishing Company

Munday, J. (2012). Introducing, Translation Studies: Theory and Application 3rd Edition. London and New York:

                     Routledge-Tylor & Francis Group.

Mwaipaja, M. L. & Malangwa, P. S. (2022).  “Changamoto za Mbinu za Kutathmini Tafsiri” katika Mwanga wa

                      Lugha, Juz. 2: Uk. 151-158. Inapatikana: https://journal.mu.ac.ke. Imseomwa tarehe 17 Juni, 2025.

Mwansoko, H. J.M. na Wenzake (2013). Kitangulizi cha Tafsiri: Nadharia na Mbinu. Dar es Salaam: TUKI.

Nzyoka, S. K. (2014).  Tathimini ya Tafsiri na Mkakati ya Kutafsiri Tamathali za Usemi katika Tamthiliya ya

                      Antigon” Tasnifu ya Shaada ya Uzamili (Haijachapishwa). Chuo Kikuu Kenyatta. Nairobi.

Onyango, J. O. (2018). “Challenges of Translating a Translate: The Role of Language, Culture and Ideology in

                  Shetani Msalabani.” In Mwanga wa Lugha Vol. 2(1): Uk149-165. Inapatikana: https://journal.

                   mu.ac.ke.com. Imesomwa tarehe 18 Juni, 2015.

TUKI (2019). Kamusi ya Kiswahili Sanifu. Nairobi: Oxford University Press.


[1] MC Matini Chanzi

[2] ML Matini Lengwa

[3] MLC: Humaanisha ya Matini ya Lugha Chanzi

[4] MLL: Humaanisha Matini ya Lugha Lengwa