Msukule

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Msukule ni mtu ambaye watu kadhaa wanaamini alikufa kimazingara: katika jamii husika mtu huyu amekufa na amezikwa, kumbe inasemekana hajafa kabisa ila amechukuliwa kimazingara na kwenda kuwekwa mahali na mtu mwingine kwa ajili ya kufanyishwa kazi za aina fulanifulani, hasa za kuchosha.

Ufafanuzi wa imani hiyo[hariri | hariri chanzo]

Kwa kuwa ni vigumu kumchukua mtu mwenye nguvu (za mwili na akili) na mamlaka, na kumfanyisha lolote unalotaka, na yeye akakubaliana na wewe, bila matata na ndugu, jamaa na marafiki zake nao wakakubaliana nalo hilo bila matata, basi, wachawi humchukua mtu na kumleta ulimwengu wa roho, lakini akitenda kazi zinazodhihirika kimwili kama kulima mashamba, kazi viwandani, ufugaji na kazi nyingine mbalimbali.

Wachawi humchukua mtu mzimamzima, yaani yeye na mwili wake na nafsi yake na roho yake, na kumweka kuishi kwenye ulimwengu wa roho.

Kwa hiyo mtu anaendelea kuwepo duniani, lakini kwenye ulimwengu wa roho. Ndiyo maana mtu anaweza akawa amewekwa kwenye duka auze au kuvuta/kuita (kulazimisha) wateja waje kununua hapo, lakini watu wa macho ya kawaida hawamwoni: yupo hapo, lakini ni kwenye ulimwengu wa roho. Kwa hiyo ili umwone ni lazima upewe macho ya kiroho au ufunguliwe macho ya kiroho ndipo uone kinachoendelea..

Kimsingi ulimwengu wa roho hakuna wenye mwili, Na wenye chochote chenye mwili kinakosa sifa ya kuishi kwenye ulimwengu wa roho (hiyo ndiyo asili ya ulimwengu wa roho).

Ila kuzimu na peponi ni mamlaka, ziko kwenye ulimwengu wa roho. Kwa hiyo mtu akifa (kwa roho yake kutoka ndani ya mwili), huenda mahali mojawapo pa kuzimu au peponi kutokana na matokeo ya thawabu yake ya maisha aliyoishi alipokuwa na mwili duniani (kwenye ulimwengu wa mwili).

Jambo lingine: kwa kuwa hakuna mwanadamu mwenye mamlaka ya kutoa uhai wa mtu hadi Mungu mwenyewe afanye hivyo au kuruhusu mtu afanye hivyo, ambaye naye huwa matatani kwa sababu ya kutoa roho ya mtu, kwa hiyo wachawi huwa hawamuui mtu ili awe msukule, ila humchukua mzimamzima na kumhamishia aishi kwenye ulimwengu wa roho.

Na kwa kuwa haiwezekani mtu kuwepo kwenye ulimwengu wa roho akiwa na mwili, basi wao humfunga kichawi asirudi kwenye ulimwengu wa mwili.

Ndiyo maana mtu huyu vifungo hivyo au nguvu hizo zinazomshikilia zikiisha au kumwachia nguvu ya mwili humvuta kurudi kwenye ulimwengu wa mwili.

Utaona mtu alikufa zamani ametokea tena, hata kama hakukufanyika maombi yoyote yale, au uganga wowote wa kumfanya mtu huyo arudi, atarudi kwa kuwa nguvu za kumfanya awe kwenye ulimwengu wa roho hazipo na matokeo yake nguvu ya mwili humvuta hadi kwenye ulimwengu wa mwili.

Mtu huyu aliyegeuzwa msukule hawezi kuonekana kwa macho ya kawaida ila na wachawi na watu maalumu tu (watumishi wa Mungu, waonaji na manabii) ndio wanaoweza kumuona.

Tathmini[hariri | hariri chanzo]

Maelezo hayo hayana msingi wowote katika sayansi. Hata hivyo imani hiyo inaendelea kupatikana katika Waafrika wengi, hata kama ni Waislamu au Wakristo, ingawa baadhi ya madhehebu yanaiona kuwa kufuatilia au kuamini mambo ya misukule ni ushirikina.

Icon-religion.png Makala hii kuhusu mambo ya dini bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Msukule kama historia yake au uenezi wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.