Nenda kwa yaliyomo

Mpunga wa Asia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Mpunga
(Oryza sativa)
Mpunga
Mpunga
Uainishaji wa kisayansi
Himaya: Planta (mimea)
(bila tabaka): Angiospermae (Mimea inayotoa maua)
(bila tabaka): Monocots (Mimea ambayo mche wake una jani moja tu)
(bila tabaka): Commelinids (Mimea kama kongwe)
Oda: Poales (Mimea kama nyasi)
Familia: Poaceae (Mimea iliyo na mnasaba na nyasi)
Jenasi: Oryza
Spishi: O. sativa
L.
Mama anatoa miche ya mpunga kabla ya kuipanda shambani
Shamba la mpunga huko Bangladesh
Mipunga iliyoiva (Marekani)[]
Mpunga kabla ya mavuno nchini Japani
Mavuno ya mpunga nchini Hispania
Oryza sativa[]

Mpunga wa Asia ni mmea wa familia ya nyasi katika ngeli ya monokotiledoni. Mbegu au punje za mpunga zikisafishwa huitwa mchele na mchele ukipikwa ni chakula cha wali. Wali ni chakula muhimu cha watu katika sehemu nyingi za dunia, hasa Asia lakini pia Afrika na penginepo.

Historia ya mpunga

[hariri | hariri chanzo]

Asili ya mpunga iko Asia. Wataalamu huamini ulipatikana mwanzoni ama China kusini au Uhindi. Wengine huona ya kwamba nyasi za aina Oryza sativa ziliendelezwa na wakulima China na Uhindi bila kutegemeana. Wakulima waliona nyasi zenye mbegu nzito kushinda nyasi nyingine waliteua yale yaliyokuwa kubwa hasa na kuzipanda kwenye matuta ya bustani. Kwa njia hiyo nyasi zenye nafaka nzito zilipatikana. Wataalamu wa akiolojia walitambua alama za mpunga na matumizi yake katika mabaki asili ya mwaka 6000 KK katika China na mwaka 5000 KK katika Uhindi.

Mnamo karne ya 3 KK mpunga ulipelekwa Japani kutoka China na kuwa chakula kikuu huko.

Aina nyingine ya Oryza (k.m. O. glaberrima na O. barthii) zilikuzwa katika Afrika ya Magharibi. Baadaye Waarabu walileta aina ya Asia iliyopandwa zaidi kutokana na mavuno makubwa. Hata sasa mpunga wa Afrika (O. glaberrima) hupandwa kidogokidogo. Tangu miaka ya 1990 haibridi za O. sativa na O. glaberrima zinakuzwa nazo zinaitwa "Nerica" (New Rice for Africa).

Uenezaji

[hariri | hariri chanzo]

Kutoka Bara Hindi mpunga ulipelekwa magharibi. Waroma wa Kale walijua mpunga uliolimwa Misri wakala wali. Baadaye Waarabu walipeleka mpunga wa aina ya O. sativa katika sehemu mbalimbali za Afrika.

Wahispania na Wareno walipeleka mpunga hadi Amerika walipoulima katika koloni zao.

Hadi leo maeneo makuu ya kilimo cha mpunga yako Asia hasa China, Bara Hindi na Asia ya Kusini-Mashariki. Asilimia 95 ya mavuno ya dunia hupatikana huko. Maeneo mengine ya maana ni kusini mwa Marekani na Italia ya Kaskazini. Penginepo mavuno hayana maana ya kimataifa hata kama kilimo cha mpunga kwenye nchi kama Tanzania au Kenya ina umuhimu fulani kimahali.

Mpunga hulimwa hasa kwa njia mbili:

  • "bichi" kwenye mashamba yanayogharikishwa ambapo mpunga unapandwa katika maji.
  • "kavu" kwenye mashamba ya kawaida kwa kutegemea mvua

Kwenye mtindo "bichi" mpunga hupandwa katika maji na mimea hukua kwenye maji vilevile. Maji huzuia majani ya kando yasiyotakiwa na vilevile wadudu wengi. Wakulima wengine wanatumia mabwawa yale pia kwa kukuza samaki kwenye shamba wakati wa mafuriko. Wakati wa kuiva maji huondolewa ili mpunga upate kukauka kabla ya mavuno.

Mpunga mara zote hukuzwa kama zao la mwaka mmoja, japo mara kadhaa katika maeneo ya tropiki huweza kudumu kwa miaka mingi, hata kwa miaka ishirini. Mpunga hukua kufikia urefu wa mita 1 -1.8 ka kimo, na hutegemea hasa aina ya udongo na rutuba yake. Mmea huwa na majani marefu kufikia hata sentimita 50 – 100 kwa urefu na upana wa sentimita 2 – 2.5. Maua madogo yanayochvushwa kwa upepohuzalishwa, na hujishikiza kwenye fimbo ndefu zenye urefu wa sentimita 30 – 50. Mbegu yenyewe huwa na urefu takribani milimita 5 – 12 na upana milimita 2 -3.

Kilimo cha mpunga kinafanikiwa sana kwenye maeneo yenye ufanyaji kazi rahisi na kiwango kikubwa cha mvua, sababu ulimaji wake ni kazi kubwa na huhitaji mvua ya kutosha. Mpunga kwa kawaida unaweza kulimwa popote, hata kwenye kilima kikali au hata milimani haswa. Japokuwa mimea yake ya asili imetokea huko Kusini mwa Asiana sehemu Fulani za Afrika, biashara na safari za kale zimeufanya utawanyike mahali pengi duniani.

Kitamaduni, njia itumikayo kuzalisha mpunga ni kujaza maji shambani, huku au baada ya kuweka vimea vya mpunga kuanzisha shamba jipya. Njia hii rahisi huhitaji mpango na huduma ya umwagiliaji, lakini pia hupunguza idadi ya magugu na magonjwa yasiyostahimili hali ya ubichi na kuzama majini kwa muda mrefu. Wakati kukuza mpunga ndani ya maji ikiwa si lazima, njia zote nyingine huhitaji uangalizi mkubwa sana wa magugu na magonjwa ya mimea pamoja na namna mbalimbali ya kuweka mbolea katika mimea.

Uzalishaji wa mpunga duniani

[hariri | hariri chanzo]

Uzalishaji wa mpunga duniani kiliongezeka sana kutoka tani milioni 200 mnamo 1960 mpaka tani milioni 600 mwaka 2004. Wazalishaji wanaoongoza ni China (26% ya mazao ya dunia), India (20%), Indonesia (9%) na Bangladeshi (5%).

Mpunga kama chakula

[hariri | hariri chanzo]

Mpunga ndio chakula kinacholiwa zaidi duniani. Ukiwa miongoni mwa nafaka, mpunga ni chakula kikuu kwa sehemu kubwa duniani, hasa Mashariki, Kusini na Kusini Mashariki mwa Asia, Kati na Mashariki mwa Amerika ya Kusini na India Mashariki.

Ni nafaka inayolimwa kwa wingi zaidi duniani baada ya mahindi, lakini kwa kuwa mahindi hulimwa kwa makusudi mbalimbali, tofauti na chakula cha binadamu, nafaka iliyo muhimu kwa binadamu kama chakula hubakia kuwa mpunga huku ukichangia zaidi ya kalori ya moja ya tano ya kalori inayotumika duniani kote.

Kama chakula cha asili huko Afrika, mpunga husaidia kuinua na kuboresha mlo, kuongeza ulinzi wa chakula, kukuza maendeleo ya eneo husika na kusaidia maendeleo endelevu ya ardhi ya eneo husika.

Maandalizi kama chakula

[hariri | hariri chanzo]
Wauzaji wa mpunga mnamo 1820 huko Japani.
Namna ya kale ya ukoboaji wa mpunga.

Mbegu za mpunga hukobolewa kuondoa maganda yake ya nje na kupata mchele. Mchele uliokobolewa sana hata kuondoa sehemu ya kahawia ya mchele na kupata mchele mweupe husababisha ugonjwa wa beriberi.

Mchele mweupe huweza kuchanganywa na virutubisho vingine ili kuuongezea kiwango cha virutubisho na kuufanya uwe bora zaidi kwa afya ya mlaji.

Kilimo cha umwagiliaji cha mpunga katika vilima vya Indonesia.

Huko India mchele hupikwa kwa kuchanganywa na maziwa na kuongezewa vionjo vingine na chakula huitwa ‘payash’ au ‘ksheer’. Mchele mbichi pia huweza kusagwa kuwa unga na kutumika katika matumizi mbalimbali, ikiwa pamoja na kutengeza vinywaji mbalimbali kama vile amazake, horchata, na sake.

Mpunga ni chanzo kizuri cha protini na ni chakula kikuu katika maeneo mengi duniani, japo si protini kwa asilimia mia: haina kiasi chote cha aside za amino muhimu kwa afya, na hulazimika kuchanganywa na vyanzo vingine vya protini kama vile maharagwe, samaki na nyama.

Mchele kabla ya kupikwa.

Mchele hupikwa kwa kawaida kwa kuchemsha au kuvukiza mvuke, na kufyonza maji. Inaweza kupikwa kulingana nakisi cha maji inachoweza kuchukua, au kiasi kikubwa cha maji inachokifyonza kabla ya kupikwa. Siku hizi kuna majiko maalumu ya kupikia mchele, yanayofanya kazi kuwa rahisi zaidi.

Mchele pia waweza kutumika kupikia uji kwa koungeza maji mengi kuliko kawaida, ili kwamba wali unaopikwa unakuwa na maji mengi zaidi na kutanuka zana na kuwa laini mno. Uji huu hutumika mara nyingi kama kifungua kinywa na ni chakula cha asili kwa wagonjwa.

    Viungo vya nje

    [hariri | hariri chanzo]
    WikiMedia Commons
    WikiMedia Commons