Nenda kwa yaliyomo

Milipuko ya Mabomu - Mbagala

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Milipuko ya Mabomu - Mbagala ni tukio lililotokea mnamo saa 11:45 asubuhi ya tarehe 29 Aprili 2009 katika eneo la Mbagala jijini Dar es Salaam, Tanzania. Ni baada ya mabomu kulipuka katika ghala ya silaha ya kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) namba 671 KJ.

Mabomu hayo yaliyokuwa yakilipuka kwa mfululizo yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 20, kujeruhi zaidi ya watu 200 na mamia kadhaa, wengi wao wakiwa ni watoto, kupotea. Athari nyingine ni uharibifu wa majumba na mali. Kati ya watu waliopoteza maisha katika mkasa huo ni mama mmoja ajulikanaye kwa jina la Sophia Shango, mkazi wa Mbagala kuu pamoja na mtoto wake. Wote walifyekwa vichwa na moja ya mabomu yaliyokuwa yakifyatuka kutoka kambi hiyo ya jeshi.

Maelezo na waathirika

[hariri | hariri chanzo]

Wakisimulia mkasa huo mmoja wa majirani aliyejitambulisha kwa jina la Eliya Deo, anasema,

“Siku hiyo muda wa saa tano asubuhi, mama huyo akiwa nyumbani baada ya kukesha kazini, alikuwa nje ya nyumba yake akitayarisha chai. Mume wake naye alikuwepo.

Mara tukasikia mlipuko wa kwanza, kilikuwa kishindo kikubwa sana, lakini tukadhani ni Transfoma ya umeme imelipuka, tukapuuzia. Mlipuko huo ukawa unafuatiwa na milipuko midogo midogo. Baada ya dakika tano ukatokea mlipuko mzito kama ule wa kwanza. Hapo ndipo tukaona watu wakikimbia kuja maeneo yetu. Wakasema kuna kambi ya jeshi imelipuka.

Ndipo Sophia akamchukua mtoto wake akaanza kukimbia. Mume wake akamsihi asikimbie, lakini hakumsikiliza akaendelea kukimbia.

Wakati huo nyumba zilikuwa zinatingishika na kutoa nyufa, watu walikuwa wanakimbia ovyo ovyo.

Mara tukasikia kishindo kikubwa cha tatu, na lile bomu tuliliona likipita angani kuelekea alikokuwa amekimbilia Sophia. Baada ya muda mfupi tukaja kuambiwa kwamba lile bomu limemfyeka kichwa na mkono na kumpasua kichwa mtoto aliyekuwa amembeba, ambaye anaitwa Deo,” anasema Eliya Deo.

Majibu baada ya tukio

[hariri | hariri chanzo]

Idadi ya watu zaidi ya 770 ikiwa bado hawajulikani mahala walipo kutokana na milipuko ya mabomu iliyotokea katika ghala la kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ), iliyoko Mbagala Kizuiani, maiti sita zaidi wakiopolewa kutoka katika mto Kizinga, uliopo katika eneo hilo.

Kupatikana kwa maiti hao, kunatia shaka kwamba huenda maiti zaidi wa tukio hilo lililoathiri maelfu ya wakazi wa eneo la Mbagala, wamo katika mto huo.

Maiti zilizoopolewa kwa mara ya kwanza katika mto huo, zinafanya idadi kubwa ya watu waliofariki dunia kufikia 20, kutoka 14 wakiwemo askari watano JWTZ.

Kutokana na hofu ya kuwapo maiti zaidi katika mto huo, idadi kubwa ya askari wa JWTZ, walikuwa katika mto huo, kujaribu kusaka maiti zaidi.

Hakuna mtu aliyeruhusiwa kufika katika eneo hilo la mto Kizinga wakati askari wa JWTZ walipokuwa wakiendelea kutafuta maiti wengine katika mto huo.

Inasadikiwa kuwa, watu wengi hasa watoto, walikimbilia katika mto huo kwa ajili ya kujiokoa wakati wa milipuko hiyo lakini wakazama na kusababisha vifo vyao.

Daktari Mkuu wa Hospitali ya Manispaa ya Temeke, Dk. Asha Mahita, alielezea kuwa alipokea maiti wapya sita zilizoopolewa katika mto huo.

Kuhusu majeruhi waliobakia katika hospitali hiyo, alisema wanaendelea vizuri, wengi wakiwa wameruhusiwa isipokuwa mwanamke mmoja ambaye baadaye alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu zaidi baada ya kushikwa na shinikizo la damu.

Dk. Asha, aliongeza kuwa, amempokea mtoto mmoja majeruhi, aliyejulikana kwa jina la Anna Hamisi (13), mkazi Mbagala Kizuiani na tangu alipofika hospitalini hapo, hakuna ndugu aliyejitokeza, kumchukua wala kuhudumia.

Makazi ya muda ya wahanga

[hariri | hariri chanzo]

Katika kambi ya muda ya Kituo cha Polisi Mbagala, watoto walikuwa wakiendelea kutambuliwa na kuchukuliwa na ndugu na wazazi wao. Kamanda wa Operesheni Jeshi la Polisi, upande wa Mbagala, Triphon Rutaihwa, alisema polisi inaendelea kuokota mabomu na kukusanya vyuma vyote ambavyo vilisambaa katika makazi ya watu. Alitoa wito kwa wananchi wenye kuviona vitu visivyo vya kawaida kutoa taarifa katika kituo hicho cha polisi.

Alisema hali ya usalama kwa sehemu hiyo bado si ya kuridhisha, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari.

Tunaendelea kuokota vipande vya vyuma na kutafuta mabomu, lakini hali bado si nzuri sana, wala mbaya sana,alisema Kamanda Rutaihwa.

Wakati polisi ikihimiza kuwataka wananchi wawe makini na vyuma wanavyovitilia shaka, jana baadhi ya wakazi wa Mabagala, hasa vijana walikamatwa wakiwa na vyuma vya mabaki mabomu.

Misaada kwa wahanga

[hariri | hariri chanzo]

Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, Reginald Mengi, pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Quality Group, Yusuf Manji, kwa nyakati tofauti, wametoa msaada kwa ajili ya waathirika hao.

Mengi, alitoa sh. milioni. 25, kwa ajili ya kusaidia mazishi na shughuli nyingine kwa wahanga wa tukio hilo.

Alikabidhi hundi kwa Mweneyekiti wa Kamati ya Mazishi, Bwanahusi katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Manispaa ya Temeke, Mengi alisema, anaungana na wahanga hao pamoja na wafiwa katika kipindi hiki cha majonzi.

Alisema kuna kila haja ya kulifanya suala hili kuwa la kitaifa, kwa kila mwenye uwezo kujitokeza kuwasaidia ili kuwawezesha wafiwa waweze kuzika ndugu zao.

Naye Manji ambaye aliwakilishwa na Meneja Utumishi wa kampuni hiyo, Amir Ally, alisema kuwa kampuni hiyo inatoa vifaa na vyakula vyenye thamani ya sh milioni 30.

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni magodoro 200, maji ya kunywa aina ya uhai chupa 438, tambi 1,000 pamoja na mchele tani tano.

Akipokea msaada huo, Meya Bwanahusi alisema bado kamati yake inahitaji misaada mingine mingi, ili kuwawezesha wananchi wa Mbagala walioathirika kwa tukio hilo kuendelea kuishi.[1]

Viungo vya Nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Milipuko ya Mabomu - Mbagala kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.