Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Rukia: urambazaji, tafuta
Mfumo wa Mmeng'enyo wa Chakula wa Binadamu
Tafsiri: utumbo mwembamba (small intestine), utumbo mpana (large intestine), ini (liver), kongosho (pancrease), ulimi (tongue), tumbo (stomach), tezi za mate (salivary glands), umio (esophagus), puru (rectum), mkundu (anus)

Mfumo wa Mmeng'enyo wa Chakula (pia: mwanya wa chakula[1]) ni jumla ya viungo mwilini mwa binadamu na mamalia wengine vinavyofanya kazi ya kuingiza chakula mwilini, kukisagasaga, kukisafirisha ndani ya mwili, kukimeng'enya, kuondoa lishe ya mwili mdami yake, na kuondoa mabaki nje ya mwili. Kwa hiyo mfumo wa mmeng'enyo wa chakula ni njia yote kuanzia mdomo hadi mkundu.

Kwa lugha nyingine unahusika na umeng'enyaji wa chakula mpaka kuwa katika hali inayoweza kusharabiwa na mwili. Ili chakula kiweze kutumika mwilini, ni lazima kivunjwevunjwe kiwe katika hali rahisi ya kuweza kusharabiwa. Kazi hiyo hufanywa na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula. Mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa mwanadamu hufanana na ule wa sungura, panya au pimbi. Sehemu kuu zinazohusika katika umeng’enyaji huo ni kinywa, umio, mfuko wa tumbo, ini, mfuko wa nyongo, utumbo mwembamba, kongosho, utumbo mpana na rektamu.

Chakula kinaposafiri katika njia yake hufanyiwa mabadiliko ya kiumbo na mabadiliko ya kikemikali. Kila sehemu ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula ina kazi maalum. Chakula cha mnyama au binadamu huweza kuwa cha kabohaidreti/wanga, protini, fati au mchanganyiko wa vyakula hivyo. Myeyuko wa makundi hayo ya vyakula hutokea katika sehemu mbalimbali za njia ya chakula kwa njia za kemikali.


Mmeng’enyo Kinywani[hariri | hariri chanzo]

Kinywa ni sehemu ya kwanza kupokea chakula. Chakula kinapokuwa mdomoni huvunjwavunjwa na kusagwa na meno au kwa lugha nyingine husagwa kimekanika. Mate husaidia kukilainisha. Ulimi husaidia kugeuzageuza chakula hicho na kukiviringisha kuwa tonge.

Meno[hariri | hariri chanzo]

Meno huvunjavunja chakula na kuwa vipande vidogovidogo wakati wa kutafuna na kusaga. Hivyo chakula huwa katika vipande vipande ambavyo huongeza eneo zaidi kwa shughuli za umeng’enyaji zinazofanywa na vimeng’enya vinavyopatikana katika njia ya chakula. Vilevile meno husaidia kufanya chakula kuwa rahisi kumezwa.

Mate[hariri | hariri chanzo]

Mate ni mchanganyiko wa maji, uteute na kimeng’enya kinachofahamika kama salivary amylase au ptyalin. Kazi za mate katika umeng’enyaji ni kama ifuatavyo:

 • Maji yaliyo katika mate hutumika katika kuyeyusha chakula.
 • Uteute wake hulainisha chakula hivyo chakula huwa rahisi kumezwa.
 • Kimeng’enyo chake (ptyalin)au salivary amylase hubadili wanga/kabohaidreti kuwa sukari rahisi (maltose).

Ulimi[hariri | hariri chanzo]

Ulimi huzungusha zungusha chakula na huwa kama tonge. Kwa msaada wa ulimi, tonge hilo husukumwa kuelekea kwenye umio (kiingereza huitwa oesophagus). Chakula kinapoingia katika umio, huelekea kwenye mfuko wa tumbo. Vyakula rojorojo hupita kwa haraka zaidi kuliko vyakula vizito.

Mfuko wa tumbo[hariri | hariri chanzo]

Chakula huhifadhiwa katika mfuko wa tumbo. Mfuko huo una uwezo wa kupanuka wakati unapopokea chakula na kusinyaa unapokuwa hauna chakula. Chakula huwa katika tumbo mwa muda wa saa tatu hadi nne. Muda huu hutegemea aina ya chakula. Chakula cha kabohaidreti, kwa mfano uji wa mahindi, huwa tumboni kwa muda usiozidi saa moja. Chakula cha protini kwa mfano nyama, huweza kuwa tumboni kwa muda wa saa moja au mbili. Katika mfuko wa tumbo, kuta za tumbo zina tezi (gastric glands) zitoazo misusumo ya gastriki (gastric juice) ambayo huwa na asidi ya haidrokloriki, uteute na kimeng’enya. Vimeng’enya vinavyotolewa tumboni ni pepsinogen , prorennin, renin

Asidi ya Haidrokloriki[hariri | hariri chanzo]

Asidi ya haidrokloriki(HCL) husaidia kufanya mambo yafuatayo tumboni:

 • Husaidia kuweka mazingira ya asidi ili vimeng’enya vya tumbo viweze kufanya kazi. Vimeng’enya vya tumboni hufanya umeng’enyaji kwa ufanisi katika hali ya uasidi.
 • Huvunja sukari tata (complex sugar) kuwa sukari rahisi.
 • Huuwa bakteria walio katika chakula.
 • Huanzisha ufanyaji kazi wa vimeng’enyo vingine katika tumbo. Pepsinogen na prorennin hubadilishwa kutoka katika hali ya awali na kuwa pepsin na rennin kwa mpangilio uliotajwa; hali ambazo ndizo hasa hufanya umeng’enyaji.

Pepsin[hariri | hariri chanzo]

Pepsin humeng’enya chakula cha protini na kuwa peptides. Pepsin hutolewa katika namna ya pepsinogen. Namna hii haiwezi kufanya mmeng’enyo mpaka itakapokutana na asidi; hivyo kuzuia kumeng’enya seli zinazoitoa katika tezi za tumbo.

Rennin[hariri | hariri chanzo]

Rennin hugandisha protini iliyo katika maziwa ili kimeng’enya cha pepsin kiweze kuivunja protini kwenda katika peptides. Kimeng’enya hiki pia hutolewa katika namna ya prorennin, ambacho huhitaji pia asidi ile kiweze kufanya kazi yake. Kimeng’enya hiki hupakitana sana katika matumbo ya mamalia wachanga walio katika kipindi cha kunyonya.

Uteute[hariri | hariri chanzo]

Uteute wa tumbo hulinda kuta za tumbo ili zisikwanguliwe na asidi ya haidrokloriki na pepsin. Bila uteute huu tumbo linaweza kujimeng’enya linyewe. Kuna uhusiano wa karibu sana kati ya uteute huu, asidi ya haidrokloriki na ugonjwa wa vidonda vya tumbo (ulcers).

Kazi za tumbo[hariri | hariri chanzo]

Kwa ufupi kazi za tumbo ni kama ifuatavyo:

 • Hutumika kama sehemu ya kutunzia chakula kwa muda mfupi kabla ya kuendelea umeng’enywaji katika sehemu zingine za mfumo wa chakula.
 • Umeng’enywaji wa chakula cha protini huanzia katika tumbo.
 • Kwa kutumia misuli yake, tumbo husaidia katika kuchanganya chakula na misusumo ya tumbo, hivyo kuboresha zoezi la umeng’enyaji tumboni.
 • Usharabiwaji wa maji, alkoholi na baadhi ya vitamin hutokea katika tumbo. Mfuko wa tumbo una misuli ambayo husinyaa na kutanuka mara nyingi, hivyo kwa muda wote chakula kinapokuwa kwenye mfuko huo huchanganywachanganywa. Kitendo hicho pamoja na athari za misusumo iliyopo kwenye mfuko wa tumbo husababisha kufanyika kwa tuitumbo (kiingereza huitwa chyme).

Utumbo mwembamba[hariri | hariri chanzo]

Kutoka kwenye mfuko wa tumbo, chakula huelekea kwenye utumbo mwembamba. Utumbo mwembamba ni mrefu zaidi kuliko ogani nyingine yoyote ya njia ya chakula. Chakula huwa ndani ya utumbo mwembamba kwa muda mrefu zaidi kuliko sehemu nyingine za nia ya chakula. Katika utumbo mwembamba chakula hukutana na misusumo yenye vimeng’enya ambavyo hutoka kwenye kongosho na utumbo mwembamba. Vimeng’enya hivyo husaidia kuyeyusha chakula. Utumbo mwembamba umegawanyika katika sehemu mbili, duodenum na ileum.

Duodenum[hariri | hariri chanzo]

Tumbo (stomach), Kongosho (Pancrease) na Duodenum

Ini[hariri | hariri chanzo]

Ini ni ogani kubwa kuliko ogani zingine katika mwili wa binadamu. Ini huweka akiba ya chakula kama vile aina za wanga iitwayo glaikojeni, vitamin na chumvi za madini. Ini pia hutengeneza nyongo ambayo husaidia katika mmeng’enyo wa fati. Nyongo hufanya kazi zifuatazo:

 • Huvunja vunja fati (lipids) na kuwa vipande vidogovidogo ambavyo huongeza nafasi kwa vimeng’enya vingine viweze kufanya kazi zao.
 • Huweka hali ya alkali ambayo ni mazingira mazuri kwa vimeng’enya vya utumbo mwembamba kufanya kazi.
 • Kuondoa asidi iliyo katika tuitumbo iliyoipata wakati chakula kilipo tumboni.

Kongosho[hariri | hariri chanzo]

Misusumo inayotengenezwa na kongosho hufikia chakula kwa kutumia mfereji unaounganisha duodenum na kongosho. Misusumo ya kongosho huwa na vimeng’enya vifuatavyo

 • Pancreatic amylase: hii huvunjavunja wanga/kabohaidreti iliyobaki kwenda katika maltose.
 • Pancreatic Lipase: humeng’enya vipande vidogovidogo vya fati na kuwa asidi za fati na glaiserini (glycerol).
 • Trypsin: Huvunja protini iliyobakia na kuwa peptides. Trypsin hutolewa katika namna ya trypsinogen.
 • Sodium Hydrogen Carbonate (NaHCO3): Huweka hali ya alkali ambayo ni mazingira mazuri kwa vimeng’enya vya utumbo mwembamba kufanya kazi.

Ileum[hariri | hariri chanzo]

Hii ni sehemu ya pili ya utumbo mwembamba ambayo ni ndefu sana na imekunjakunja sana. Sehemu imejikunja ili iweze kutosha sehemu ya tumbo ambayo ingekuwa ndogo kama ungenyooka (inafikia karibia mita saba). Ileum hutoa misusumo yenye vimeng’enya vifuatavyo:

 • Erepsin (peptidase): Humeng’enya peptides na kuwa asidi za amino.
 • Maltase: Huvunja maltose na kuwa glucose.
 • Lipase: humeng’enya vipande vidogovidogo vya fati na kuwa asidi za fati na glaiserini (glycerol).
 • Sucrase: Huvunja sucrose na kuwa glucose.

Mchakato wa umeng’enyaji humalizikia kalizikia katika ileum. Ileum kwa ujumla ina kazi kuu mbili: Umeng’enyaji wa kabohaidreti, protini na fati. Pia usharabiwaji wa chakula ambacho ni matokea ya umeng’enyaji kwenda katika mkondo wa damu.

Kusharabiwa kwa chakula Chakula kinapofikia hatua hizo huwa kiko tayari kusharabiwa na vinywelea vilivyo katika utumbo mwembamba viitwavyo vilasi. Vilasi hizo huchukua asidi za amino, sukari rahisi (glucose) na chumvi na kupeleka katika mishipa ya vena hadi kwenye ini. Katika ini sukari rahisi hubadilishwa kuwa glaikojeni na kuhifadhiwa. Asidi za amino za ziada hugeuzwa kuwa glaikojeni na yurea(kemikali fulani ambayo baadaye huwa mkojo). Kutoka kwenye ini chakula kinachohitajiwa na mwili husafirishwa na damu hadi kwenye moyo. Damu hiyo husambaza chakula hicho katika mwili mzima kwa matumizi mbalimbali. Sehemu kubwa ya chakula humeng’enywa na kusharabiwa katika utumbo mwembamba. Chakula kilichobaki huelekea kwenye utumbo mpana.

Utumbo mpana[hariri | hariri chanzo]

Chakula kinachotoka katika utumbo mwembamba na kuingia utumbo mpana huwa ni kile ambacho hakikuweza kumeng’enywa au kile ambacho kimeng’enywa lakini hakikusharabiwa. Sehemu ndogo tu ya chakula kilichomeng’enywa husharabiwa na utumbo mpana. Sehemu kubwa ya maji iliyotokana na mmeng’enyo wa chakula husharabiwa na utumbo mpana. Sehemu iliyobaki ya chakula huelekea kwenye rektamu na kutolewa nje kupitia njia ya haja kubwa (mkundu) kama kinyesi.

Tazama Pia[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

 1. Mwaniki, J. M. (2008) Fundamentals of Biology Second Edition, Delah Educational Publishers, Dar es Salaam
 2. Taasisi ya Ukuzaji Mitaala, Sayansi, Kitabu cha Nne, Eastern Africa Publications Limited
 3. Namna Mfumo wa Umeng'enyaji Unavyofanya kazi
Gray188.png Makala hii kuhusu mambo ya anatomia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mfumo wa mmeng'enyo wa chakula kama matumizi yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
 1. Mwanya wa chakula na Mwanya wa umeng'enyaji ni mapendekezo ya KyT