Hedhi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Menstruation)
Vifaa vya kuzuia damu ya hedhi.

Hedhi (kutoka Kiarabu حيض) ni kipindi maalumu katika mzunguko wa mwanamke mwenye umri wa kuzaa. Wakati huo, ambao kwa kawaida unarudi kila baada ya mwezi mmoja hivi, yeye hutokwa na damu kwenye uke.

Maelezo ya sayansi[hariri | hariri chanzo]

Sababu ya damu kutoka ni kwamba, kijiyai kilichokomaa na kutoka nje ya kifuko cha vijiyai kisipopata mbegu ya mwanamume baada ya siku moja kinaharibika harakaharaka; hapo ngozi nyembamba ya tumbo la uzazi, iliyotanuka kwa damu ili kupokea na kulisha mimba, inachanikachanika na kutoa damu.

Kumbe mbegu ikikifikia kijiyai, mimba inapatikana na kujishikiza kwenye kuta za tumbo la uzazi ili iendelee kukua; hapo damu haitoki na mama anaweza kujihisi mja mzito.

Mizunguko mingi ya hedhi huwa na siku kadhaa za mwanzo ambapo mimba haiwezi kupatikana (muda wa kutoshika mimba kabla ya kudondosha kijiyai), halafu siku ambazo mimba inaweza kutungika, na kisha siku kadhaa tu kabla ya hedhi ambazo mimba haiwezi kutungika (muda wa kutoshika mimba baada ya kijiyai kudondoshwa).

Siku ya kwanza ya kuvuja damu inahesabiwa kuwa siku ya kwanza ya mzunguko wa hedhi. Mbinu mbalimbali za kufahamu uwezo wa kushika mimba huhesabu kwa njia tofauti kidogo kipindi ambapo kuna uwezekano wa kupata mimba, yaani hutumia ishara za msingi za uwezekano huo, historia ya mzunguko, au zote mbili.

Dysmenorrhea[hariri | hariri chanzo]

Dysmenorrhea ni jina la kitabibu kwa maumivu kipindi cha hedhi, ambayo hutokana na kusinyaa kwa misuli ya mji wa mimba wakati wa hedhi ili kuruhusu kumeguka kwa ukuta wa mfuko wa mimba na kutoa damu iliyochanganyika na kijiyai ambacho hachikurutubishwa nje.

Maumivu haya yamegawanyika katika aina mbili.

Maumivu ya hedhi aina ya kwanza ya kawaida (Primary Dysmenorrhea)[hariri | hariri chanzo]

Maumivu haya ni ya kawaida kabisa kwa wanawake wanapopitia kipindi hiki ambacho hujirudia kila mwezi. Maumivu kwa kawaida huanza kati ya siku moja ama mbili kabla ya hedhi kuanza kutoka, mwanamke hujiskia mamumivu haya kwenye tumbo la chini, kwenye nyonga na kiuno kwa ujumla. Maumivu haya yanaweza kuwa madogo au yakawa makali sana na huisha ndani ya masaa 12 mpaka 72 huku yanaweza kuambatana na kutapika na kupata kizunguzungu. Kwa wanawake wengi maumivu haya, ambayo ni ya kawaida kabisa, hupungua kadiri umri unavyokwenda na pia pale mwanamke akijifungua.

Maumivu aina ya pili yasiyo ya kawaida (Secondary Dysmenorrhea)[hariri | hariri chanzo]

Maumivu haya hutokana na tatizo fulani la kiafya kwenye via vya uzazi vya mwanamke, kama vile uvimbe ambayo si wa saratani ndani ya mfuko wa mimba (uterine fibroids), kukua kwa tishu laini za mfuko wa mimba kuelekea kwenye viungo vingine kama uke na mifuko ya vijiyai (endometriosis) na pia kupanuka kwa ukuta wa uterasi kutokana na kukua kwa tishu za ndani za uterasi kuelekea ukuta wa nje (adenomyosis).

Maumivu haya yasiyo ya kawaida yanaweza pia kusababishwa kwa athari za bakteria ama virusi katika via vya uzazi. Kwa kawaida maumivu haya huanza mapema zaidi wakati wa hedhi ya huchukua muda mrefu zaidi kuisha ukilinganisha na maumivu ya kawaida (primary dysmenorrhea), na pia maumivu haya yanakuwa hayaambatani na kutapika, kuharisha, kizunguzungu wala kukosa nguvu na ganzi.

Maumivu kipindi cha hedhi kwa kiasi kikubwa hulenga viungo hivi[hariri | hariri chanzo]

  • Via vya uzazi - kama maumivu yako hutokana na kukua zaidi kwa tishu za uterasi, basi maumivu husambaa hadi kwenye tumbo la uzazi.
  • Tumbo la chini — huathirika pia na maumivu haya kwa kiasi kikubwa, kama maumivu haya hutokana na kukua kwa tishu za uterasi, basi mwanamke anahisi kama ameunguzwa na kitu cha moto katika tumbo.
  • Kiuno - maumivu ya kiuno mara nyingi hutokana na kukua kwa tishu za uterasi kuelekea uke na mifuko ya vijiyai.
  • Miguu - maumivu yanaweza pia kutokea kwenye mapaja yakishuka chini ya miguu na kufanya mwanamke kushindwa kutembea.
  • Maumivu ya kisaikolojia hutokea pia kwa kiwango kukubwa kwa wanawake ambao maumivu yao ya hedhi hutokanana na tishu za uterasi kukua bila mpangilio: wanawake hawa hupata msongo wa mawazo kutokana na kufikiri kwamba
    • Pengine tatizo la uvimbe haliwezi kupona na hakuna dawa
    • Ama hawataweza kupata mtoto kwa siku za baadae
    • Mahusiano yao na marafiki ama wapenzi yatavunjika kama wakijua ana tatizo la uvimbe
    • Ama kufikiri jinsi ambavyo hawatafanya kazi zao kwa ufanisi na kutofurahia maisha kama mwanzo, walipokuwa wazima.

Chanzo cha maumivu kipindi cha hedhi[hariri | hariri chanzo]

Maumivu hayo hutokana na kitendo cha misuli ya uterasi kukaza na kusinyaa kupitia, kitendo hiki huratibiwa na homoni ya prostaglandins. Ni kawaida kwa uterasi ambao ni mfuko unaobeba mimba kusinyaa kipindi chote cha mzunguko wa hedhi ambacho huchukua siku 28. Lakini tofauti ni kwamba wakati wa kutoa hedhi yenyewe mfuko huu husinyaa na kujikaza zaidi na hivyo kukatisha hewa safi ya oksijeni kufika kwenye misuli ya mfuko huu wa mimba. Maumivu ni matokeo ya kukosekana kwa muda kwa hewa ya oksijeni kwenye baadhi ya misuli ya uterasi.

Cha kufanya pale unapopata maumivu kipindi cha hedhi[hariri | hariri chanzo]

Kuna njia nyingi ambazo husaidia kupunguza maumivu ya hedhi ambazo unaweza kutumia ukiwa nyumbani kwako pasipo kwenda hospitali. Kama mauvimu ni makali sana unaweza:

  • Kumeza dawa za kukata maumivu kama aspirini na ibuprofen kwa ahueni ya haraka. Lakini dawa hizi zitumike kwa uangalifu: zisiwe na nia ya kutumika kila mara kwani madhara yake ni makubwa kiafya.
  • Tumia maji vuguvugu kukandakanda mahali pa tumbo la chini ukiwa umelala chali.
  • Usitumie vinywaji na vyakula vyenye kafeini, mfano chai au kahawa.
  • Fanya masaji upande wa kiuno na sehemu ya tumbo la chini.
  • Pata muda mwingi wa kupumzika.
  • Weka ratiba ya kufanya mazoezi mara kwa mara: tafiti zinasema wanawake wanaofanya mazoezi hupunguza maumivu ya hedhi kwa kiwango kikubwa ukilinganisha na wasiofanya mazoezi.

Lini unatakiwa kumuona daktari ili kupata matibabu na ushauri zaidi[hariri | hariri chanzo]

Kama maumivu yako ni makali kuliko kawaida na yanachukua zaidi ya siku tatu hakikisha unamwona daktari wako haraka, kwa sababu yawezekana maumivu yako si ya kawaida na yaweza kuwa una uvimbe ama maambukizi ya bakteria na virusi kwenye mfuko wa mimba, hivyo kuwahi hospitali kutasaidia kutibu tatizo lako mapema kabla halijawa kubwa. Pia inashauriwa kuwahi kumwona daktari kwa sababu ukuaji wa tishu za mfuko wa mimba unahusishwa na kusababisha saratani ya shingo ya kizazi, hivyo kujua chanzo cha tatizo lako mapema kutasaidia kulitibu mapema.

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Makala hii kuhusu mambo ya biolojia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Hedhi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.