Meli ya abiria

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Meli ya abiria ni chombo kikubwa cha majini kilichotengenezwa kwa kusudi la kubeba watu hasa, mara nyingi pamoja na magari au kiasi cha mizigo.

Aina za meli za abiria[hariri | hariri chanzo]

Feri ya Mega Smeralda inahudumia usafiri kati ya visiwa vya Korsika (Ufaransa) na Sardinia (Italia)
Freedom of the Seas ni kati ya meli kubwa za burudani
  • feri ni boti au meli inayobeba watu hasa pamoja na kiasi cha mizigo kwenye maji kwa umbali mdogo; tofauti na kivuko kinachohudumia usafiri ya kuvuka mto au ziwa feri kubwa zinategenezwa kama meli kabisa inayoweza kupita kwenye mawimbi wakati wa dhoruba. Zinaunganisha miji kando la bahari au maziwa makubwa na safari zao zinadumu masaa hadi siku kadhaa. Kwa kawaida hufuata ratiba na masaa maalumu. Feri za kisasa mara nyingi huwa na nafasi ya kuingia kwa gari, lori au mabehewa ya reli pamoja na vyumba vya abiria na huduma za chakula.
  • Meli za abiria zilizofuata ratiba baina ya mabandari maalumu zilikuwa njia kuu ya usafiri kati ya mabara kuanzia katikati ya karne ya 19 hadi katikati ya karne ya 20. Baadaye nafasi yao ilichukuliwa na eropleni na katika karne 21 ni chache sana zilizobaki.
  • Meli za burudani (ing. cruise ships) ni biashara iliyopanuka sana. Zina nafasi zote za hoteli kubwa kwenye maji zikisafirisha watalii wanaokuja -mara nyingi kwa ndege hadi bandarini- kwa safari za siku kadhaa hadi wiki kadhaa ambako meli hizi zinapita karibu na pwani ambako watalii wanapata nafasi kwenda nchi kavu mara kwa mara na kuangalia vivutio vya mahali.

Meli kubwa za aina hii zina nafasi kwa abiria 6,000 - 7,000 wanahudumiwa na mabaharia na watumishi zaidi ya 2,500.

Historia ya meli za abiria[hariri | hariri chanzo]

Meli inayoingia bandari ya Dar es Salaam mnamo 1910 meli za aina hii zilibeba abiria lakini pia mizigo
SS Normandie ilikuwa kati ya meli bora zilizounganisha Ulaya na Marekani katika miaka ya 1930

Meli ya abiria ya pekee zilianza kutokea wakati wa karne ya 19, hadi wakati ule jahazi na pia meli zilibeba mizigo pamoja na watu na zilikuwa na vyumba vichache vya abiria wenye pesa ilhali wengine walikaa kwenye sitaha au pamoja na mizigo.

Kutokea kwa injini ya mvuke na mawimbi ya uhamiaji kutoka Ulaya kwenda Marekani na mabara mengine kulisababisha kuundwa kwa meli hasa kwa kusudi la kubeba abiria zilizopangwa kubeba mamia au zaidi ya watu. Njia za meli ziizofuata ratiba ziliunganisha pande zote za Dunia.

Tangu miaka ya 1950 eropleni zilianza kuchukua asilimia kubwa ya usafiri wa kimataifa na hivyo meli za abiria zinazofuata ratiba karibu zimepotea.

Baada ya kukosa abiria kwa safari baina ya mabara makampuni ya meli zilianza kukazia safari za burudani, kwa mfano katika Mediteranea au katika Bahari ya Karibi. Polepole meli za zamani zilitolewa kwenye huduma na meli zilitengenezwa kwa kusudi ya burudani pekee[1] .

Soko nyingine kwa meli za abiria ni huduma ya feri za baharini. Huduma hii ni muhimu hasa kama kuna magari mengi pamoja na visiwa na miji muhimu inayotengwa na gimba la maji lisilo kubwa mno. Kwa hiyo safari nyingi kwa feri zinahesabiwa Ulaya (Uingereza, Skandinavia, Bahari Baltiki), kwenye Mediteranea pale Ugiriki na Uturuki, na katika Amerika ya Kaskazini.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Cruise Ship Tonnage. 123Ttravel.com. Jalada kutoka ya awali juu ya October 11, 2007. Iliwekwa mnamo 2007-12-28.