Malezi ya kijinsia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Elimu ya kijinsia inayotegemea vifaa badala ya tunu inalenga kukwepa uzazi na maradhi tu, si kufanya mtu aelewe maana ya jinsia kwa maisha.

Malezi ya kijinsia ni sehemu muhimu ya malezi inayolenga kumsaidia mtoto kukabili vema hali yake ya kuwa mwanamume au mwanamke ili jinsia imjenge badala ya kumvuruga.

Wavulana wanaongelea siri zao wasitake wasichana wazijue, na wasichana wanafanya vilevile kati yao. Lakini wanahitaji kusaidiwa na watu waliokomaa.

Malezi ya kijinsia zamani[hariri | hariri chanzo]

Afrika zamani ilikuwa kawaida waziongelee na wazee (babu, bibi, n.k.). Pia kulikuwa na mafundisho rasmi katika jando na unyago.

Mara nyingi kwa njia hizo zilienea habari zisizoaminika, kwa kuwa waliotoa maelezo hawakuwa na ujuzi wa sayansi, tena pengine mtazamo wa maadili ulikuwa mpungufu.

Hali ya sasa[hariri | hariri chanzo]

Siku hizi tunaweza tukapotoshwa zaidi, tena kwa makusudi, na vipindi shuleni na vyombo vya upashanaji habari vinavyopuuzia msimamo sahihi upande wa jinsia na uzazi, ukiwa ni pamoja na usafi wa moyo na hata uhai wa watoto. Mkazo ni kwamba tuzini tu, mradi tukwepe matokeo yake, yaani mimba na maradhi ya zinaa.

Hivyo watu wanaelekezwa wazidi kuzama katika ashiki badala ya kulenga ukomavu na uadilifu kwa bidii zote na kwa kujiombea msaada wa neema ya Mungu.

Wanaelekezwa kufuata anasa kwa kukwepa uzazi wasije wakaongezeka wakalazimika kujitafutia mahitaji halisi (chakula, matibabu, mavazi n.k.) badala ya vitu vya ziada vinavyoleta faida kubwa kwa wafanyabiashara matajiri (vileo, soda, tumbaku, simu n.k.).

Katika kulenga anasa bila ya kuwajibika (kwa watoto watarajiwa) wanaelekezwa na propaganda za nguvu wazitumie njia za teknolojia za kupanga uzazi ambazo (tofauti na njia zinazotegemea maumbile) zina gharama kwa watumiaji na hivyo faida kwa watengenezaji.

Vilevile wanahamasishwa kuharibu mimba, ambazo pia ni chanzo cha mapato makubwa kwa wale wanaoziua na kwa wale wanaozitumia katika maabara zao kwa majaribio na utengenezaji wa dawa na vipodozi.

Haja ya malezi bora[hariri | hariri chanzo]

Hasa katika hali hiyo tunaona umuhimu wa kujua mapema ukweli kuhusu umbile zima la binadamu.

Kadiri mtoto anavyozidi kukua anahitaji kujifahamu kijinsia aweze kukomaa na hatimaye kuzaa kadiri ya mpango wa Mungu.

Ndiyo sababu ni muhimu mafundisho hayo yatolewe kuanzia utoto na kukamilishwa kabla mtu hajajichagulia maisha (njia ya ndoa au nyingine) ili aweze kujua anafanya nini au anaacha nini.

Wahusika[hariri | hariri chanzo]

Lakini nani ana haki na wajibu wa kuamua mafundisho yatolewe vipi? Kwa kuwa watoto ni wa wazazi hasa, uamuzi ni juu yao na juu ya viongozi wa dini yao. Serikali inaweza tu kuwasaidia katika kazi hiyo mradi isiiingilie maadili yao.

Utakatifu wa uhai na jinsia[hariri | hariri chanzo]

Katika mila nzuri za Mwafrika mojawapo inafundisha kuheshimu viungo vya uzazi kama milango ya uhai. Kwake uhai ni jambo takatifu linalotokana na Mungu ambalo binadamu anapaswa kulistawisha kwa kila namna upande wake binafsi na upande wa jamii (ukoo n.k.). Kwa msingi huo kila kitu kinachohusu uzazi kinaheshimika.

Mtazamo huo unakwenda kinyume cha ule unaoenea sasa kuanzia nchi za magharibi, ambao unaona mwili na jinsia kuwa ni vyombo vya kuchezea tu ili kujifurahisha bila ya kuwajibika kwa ustawi wa uhai.

Utakatifu wa uhai na jinsia unatokana na ukweli kwamba mtu kwa mpango wa Mungu anaweza kushiriki katika uumbaji wa wengine ambao waishi milele. Ukweli huo unaeleweka kwa akili yetu tena umefunuliwa na Mungu.

Upande mmoja yeye haumbi binadamu pasipo wazazi; upande mwingine wazazi wakiungana na kuwezesha mimba ipatikane, mara tu Mungu anaitia roho. Hivyo imani ya dini inaiunga mkono mila ya kuheshimu milango ya uhai kama fumbo la ajabu.

Kuliheshimu hakutuondolei wajibu na haki ya kulichunguza kwa njia ya sayansi ili tufurahie maajabu ya Mungu, halafu tuelewe na kutekeleza vizuri zaidi mpango wake.

Hivyo tunaipokea kwa mikono miwili zawadi hiyo kubwa na kuifanyia kazi ili kumpendeza aliyetuzawadia; si kuitupa kama kitu cha bure wala kuitumia kwa madhara.

Tunapaswa kuelewa:

  • 1. jinsi tulivyoumbwa kama umoja wa roho na mwili;
  • 2. tena tulivyoumbwa wanaume au wanawake toka kichwa hadi kidole cha mguu: jinsia si viungo vya uzazi tu;
  • 3. viungo vyetu hivyo jinsi vilivyo na vinavyofanya kazi;
  • 4. jinsi kazi hiyo inavyoelekea muungano na mtu wa jinsia nyingine na kwa njia hiyo uzazi pia.

Ndipo tutakapoweza kuwajibika katika ndoa au kujinyima kwa lengo lingine kubwa zaidi.