Nenda kwa yaliyomo

Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari ya Tuol Sleng

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Vyumba vingi vya shule viligawanywa kuwa seli za wafungwa.
Seli ya matofali ndani ya gereza la S-21 nchini Kambodia.
Muonekano kutoka ndani ya seli ya Gereza la S-21.
Seli ndogo zilizokuwemo ndani ya gereza hilo.
Waya wa miiba uliowekwa kuzunguka eneo lote.
Muonekano wa ndani wa makumbusho hayo hivi sasa.

Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari ya Tuol Sleng ni Jumba la Makumbusho linayohifadhi historia ya mauaji ya kimbari ya Kambodia yaliyotokea mjini Phnom Penh. Eneo hili zamani lilikuwa shule ya sekondari ya Tuol Svay Prey kabla ya kugeuzwa kuwa gereza na kituo cha ulinzi na utesaji kilichojulikana kama Gereza la Usalama 21 (S-21) chini ya utawala wa Khmer Rouge kuanzia mwaka 1975 hadi 1979. Kati ya miaka 1976 na 1979 takriban watu 20,000 walifungwa hapo ambapo pakawa moja kati ya vituo vya utesaji na mauaji vilivyoanzishwa na polisi wa siri wa utawala huo.[1] Mnamo tarehe 26 Julai 2010 mahakama maalumu ya Kambodia ilimtia hatiani mkuu wa gereza hilo Kang Kek Iew kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu na ukiukaji mkubwa wa Mikataba ya Geneva ya 1949 ambapo alifia gerezani mwaka 2020 akitumikia kifungo cha maisha.[2][3]

Majengo matano ya shule hiyo yaligeuzwa kuwa gereza mnamo Machi au Aprili 1976 ambapo yalizungushiwa nyaya za umeme na madarasa kugawanywa kuwa seli ndogo na vyumba vya utesaji huku madirisha yakifungwa nondo za chuma kuzuia wafungwa kutoroka au kujiua.[4][5] Kwa wakati mmoja gereza lilikuwa likihifadhi kati ya wafungwa 1,000 hadi 1,500 walioteswa vikali ili kuwataja ndugu na marafiki zao ambao nao walikamatwa na kuuawa. Katika miezi ya kwanza waathirika wengi walikuwa wanajeshi na maofisa wa serikali iliyopita ya Lon Nol pamoja na wasomi, madaktari, walimu, na wanafunzi lakini hapo baadaye uongozi wa chama ulianza kuwasaka hata wanachama wake wenyewe na kuwaua pamoja na familia zao katika kituo cha Choeung Ek kutokana na hofu ya kupinduliwa kwa Pol Pot.[4] Gereza hili liligunduliwa na jeshi la Vietnam lililovamia nchi hiyo mwaka 1979 na kurejeshwa kama makumbusho ya kihistoria kati ya miaka 1979 na 1980 na serikali mpya.

Wafungwa walipofika walipigwa picha na kulazimishwa kuandika wasifu wa maisha yao tangu utotoni hadi walipokamatwa kabla ya kuvuliwa nguo zao na kufungiwa kwenye seli wakiwa wamefungwa minyororo ya miguu kwenye kuta au sakafu ya zege bila mikeka wala mablanketi huku wakikatazwa kuzungumza.[4] Maisha ya gerezani yalianza saa kumi na nusu alfajiri kwa walinzi kukagua minyororo na seli zao ili kuzuia kujiua ambapo wafungwa walipewa vijiko vinne tu vya uji wa mpunga mara mbili kwa siku na kupewa adhabu ya vipigo vikali wakinywa maji bila idhini au kukaidi sheria zilizowataka kuomba ruhusa kwa kila jambo ikiwemo kulazimishwa kula kinyesi na kunywa mkojo.[6] Mazingira hayo machafu yalisababisha magonjwa ya ngozi na chawa huku matibabu yakitolewa na wauguzi wasio na ujuzi kwa lengo la kurefusha tu maisha yao ili waendelee kuhojiwa wakiwa wamefungwa vitambaa machoni wakati wa kwenda vyumba vya utesaji.[4]

  1. Locard, Henri (Machi 2005). "State Violence in Democratic Kampuchea (1975–1979) and Retribution (1979–2004)" (PDF). European Review of History. 12 (1): 121–143. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2013-10-30.{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  2. "Case 001 | Extraordinary Chambers in the Courts of Cambodia (ECCC)". Extraordinary Chambers of the Courts of Cambodia. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 23 Desemba 2016. Iliwekwa mnamo 5 Septemba 2017.{{cite web}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  3. "Cambodia genocide: Khmer Rouge prison chief Comrade Duch dies". BBC News. 2 Septemba 2020.{{cite news}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
  4. 1 2 3 4 A History of Democratic Kampuchea (1975–1979). Documentation Center of Cambodia. 2007. uk. 74. ISBN 978-99950-60-04-6.
  5. Vickery, Michael (1984). Cambodia, 1975-1982. Boston, MA, USA: South End Press. uk. 151.
  6. Howard J. De Nike; John B. Quigley; Kenneth Jay Robinson, whr. (2000). Genocide in Cambodia: documents from the trial of Pol Pot and Ieng Sary. University of Pennsylvania Press. uk. 375. ISBN 978-0-8122-3539-5. Iliwekwa mnamo 12 Oktoba 2010.{{cite book}}: CS1 maint: date auto-translated (link)
Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Makumbusho ya Mauaji ya Kimbari ya Tuol Sleng kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.