Maji

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Maji katika hali tatu tofauti: kiowevu, mango (barafu), na gesi (mvuke hewani). Mawingu ni malundo ya matone ya maji yaliyotokana na hewa iliyojaa mvuke.
Maji ya bomba

Maji huwa ni kiini cha uhai wowote duniani na pia kiini cha utamaduni wa binadamu. Hakuna mtu anayeweza kuishi bila maji kwa sababu asilimia 50 - 65 za mwili wa mwanadamu ni maji. Hata miili ya mimea na wanyama kwa kiasi kikubwa ni maji.

Maji kikemia

Kikemia maji ni kampaundi ya elementi za oksijeni na hidrojeni, ikiunganisha atomi mbili za hidrojeni na atomi moja ya oksijeni kuwa molekuli ya H2O au maji.

Jina la maji hutumika hasa kwa hali ya kiowevu ya H2O. Hali mango huitwa barafu na hali ya gesi huitwa mvuke. Yenyewe hayana rangi wala ladha au harufu.

Maji huwa ni kiowevu kinachopatikana kwa wingi duniani. Yajaza mito, maziwa na bahari. Theluthi mbili za uso wa dunia hufunikwa na maji.

Maji katika historia ya binadamu

Upatikanaji wa maji ulikuwa jambo muhimu katika historia ya utamaduni wa kibinadamu tangu mwanzo. Njia za maji zilikuwa kati ya njia za kwanza za mawasiliano kwa watu; mabonde ya mito inakata milima na kurahisisha usafiri.

Hata kwa watu kwenye ngazi ya wawindaji kando ya mto au ya ziwa ilikuwa mahali muhimu walipopata wanyama waliokuja kunywa.

Watu wenyewe walipanga makazi yao penye maji.

Binadamu walipoanza kulima maji kwa mashamba yalikuwa muhimu zaidi, hasa katika maeneo pasipo mvua ya mara kwa mara.

Wataalamu wengi huona kwamba ugawaji wa maji ulikuwa chanzo cha hisabati, sayansi na serikali. Madola makubwa ya kwanza yametambuliwa katika mabonde ya mito kwenye nchi yabisi kama mto Naili, Frati na Hidekeli au Indus. Haja ya kugawa maji, kujenga mifereji, kuitunza na kusimamia shughuli hizi zilileta haja ya kujenga uwezo wa kuhesabu, kutunza kumbukumbu, kuanzisha mwandiko na kuwa na vyombo vya utawala.

Njia za kukusanya, kugawa na kufikisha maji kwa watumiaji zimekuwa chanzo cha miundombinu katika nchi nyingi.

Viungo vya nje

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Maji kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.