Majadiliano:Kwanzaa

Yaliyomo ya ukurasa hayatumiki katika lugha nyingine.
Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Maajabu ya Kwanzaa[hariri chanzo]

Ndesanjo hujambo! Baada ya kusoma makala kuhusu Kwanzaa ninegependa kukuuliza kuhusu Kwanzaa jinsi unavyoiona ukiwa Mwafrika na Mwsahili. Nimetazama desturi hii kwa miaka kadhaa nikiwa mbali nikashangaa. Kwangu ilikuwa wazi ya kwamba sherehe hii haina kitu cha kiafrika ndani yake. Wala Afrika ya mashariki wala ya magharibi nimesikia ya kwamba kuna sikukuu ya mavuno wakati wa Disemba.

Kiswahili wanachotumia - basi naiona mtandaoni tu. Lakini kama ningemjibu mtu anayenisalimu "Habari gani" kwa maneno kama "kuumba" sijui angeniangalia namna gani.. Ama ataona nimesahau lugha au atajiuliza kama nimelewa. Wanaweka mahindi wakiita "muhindi" (sina neno kuhusu mahindi - imekuwa kiafrika sawa jinsi kiazi kimekuwa kiingereza au kijerumani ingawa zote zimetoka Amerika ya Kusini, hata kama Wachagga na Waganda wasingekubali kamwe :-)) - ila tu lugha bovu). Unajua wewe mahali Afrika penye sherehe ya "matunda ya kwanza"???

Kwangu imeonekana kama sherehe ya kisintetiki yaani isiyo ya asili kabisa. Ni kama ndoto nyingine tena juu ya Afrika: Waingereza wanaota ndoto zao za "Out of Africa", karne zilizopita wataalamu wa Ulaya walikuwa na ndoto hizi za "Washenzi watukufu". Afrika ilikuwa na bado leo iko mara nyingi kama skrini ya filamu watu wanapotupa picha zilizomo kichwani mwao. Lakini si Afrika yenyewe.

Kwa upande mwingine nimefikiri basi si kitu kibaya kama watu wanatafuta habari za Kiswahili hata kama njia ni potovu. Ikisaidia kueneza kwa lugha ya Kiswahili nifunge macho? (Juzi nimepita mahali mtandaoni wanapotaja majina kwa ajili ya watoto wakidai ni ya Kiswahili - taz. http://www.babynology.com/swahili/baby-names-boy_M_100.html - natumaini ya kwamba kuna matokeo mazuri zaidi ya upendo ule wa Kiamerika wa lugha kuliko orodha hii!)

Juzi tu nimeona mara ya kwanza habari za huyu Karenga kuwa jina lake ni Ron Everett amekuwa na historia mbaya asiyopenda kukubali. Umewahi kukutana naye? Ameanza kujifunza Kiswahili siku hizi? Kujiita "Maulana" ili watu wote Marekani wanaamini ni neno la Kiswahili kwa ajili ya "mwalimu" ni ajabu nyingine kwangu.

Kwa hiyo - ningependa kusikia mawazo yako kweli! --Kipala 17:05, 8 Januari 2006 (UTC)[jibu]

Mjadala wa maana sana huu. Nitaweka maoni yangu hapa baadaye. Ninamaliza mambo kadhaa. Asante.----Ndesanjo

Kipala asante kwa changamoto yako kuhusu Kwanzaa. Mimi nilikuwa nawaza kama wewe wakati fulani lakini baadaye nimebadili mawazo yangu. Sidhani kama ni sahihi kusema kuwa sherehe hii sio ya Kiafrika kwakuwa haisherehekewi sehemu yoyote ya Afrika. Wamarekani wa Kiafrika ni Waafrika kihistoria na Wamarekani kiuzoefu.

Tukumbuke kuwa watu hawa wametoka Afrika miaka mingi sana. Na wapo kama akina Karenga ambao wanataka sana kujua historia yao na kufanya mambo ambayo yatawaunganisha na utamaduni wa Kiafrika. Lakini wakati huo huo ni vigumu sana kujua utamaduni wao wa Kiafrika kwasababu kadhaa: kuondoka kwao Afrika miaka mingi, vyanzo vichache vya elimu na maarifa kuhusu utamaduni wa Afrika, Waafrika walioko Afrika kutojua utamaduni wao na kutotaka kuuenzi.

Kwahiyo lazima watu hawa waliondolewa Afrika kwa nguvu miaka na miaka iliyopita watakuwa na mambo fulani ambayo hawayafahamu vizuri kuhusu utamaduni wao. Ni wajibu wetu ambao tunaufahamu kuwasaidia kuwaelimisha na pia kuwapa moyo pale wanapojaribu kujitafuta na kuenzi kile kidogo wanachokijua kuhusu Uafrika.

Pia tufahamu kuwa sio rahisi kwa mtazamo wao kuhusu utamaduni wa Afrka kuwa ni sawa kabisa na utamaduni ulioko Afrika katika makabila mbalimbali. Kuna maswali mengi ya kujiuliza: je utamaduni huo utakuwa wa Kimasai, Kiyoruba, Kifulani, n.k.? Kumbuka neno utamaduni wa Afrika linaweza kupotosha maana linaonyesha kuwa kuna mfumo mmoja wa kitamaduni wa Afrika wakati ukweli ni kuwa kuna tamaduni mbalimbali ziinazotofautiana barani Afrika. Kwahiyo ingawa utamaduni wa Kishona na Kichagga ni wa Kiafrika, mambo mengi hayafanani. Wengi wa Waafrika wa Marekani hawajui wametoka wapi hasa, wanachojua ni kuwa wametoka Afrika. Hili ni muhimu sana. Mwandishi wa kitabu cha “Afrocentricity” Molefi Asante anasema kuwa Wamarekani wanaposema wanaenzi utamaduni wa Kiafrika, utamaduni huo sio lazima eti ukienda Afrika uukute ukifanana kabisa na ule wanaouenzi Wamarekani. Anasema kuwa utamaduni wa Kiafrika ni utamaduni wa Waafrika (wawe wako Brazili, Angola, Zambia, Cuba, Venezuela, Marekani, n.k.) popote pale walipo. Utamaduni huo sio lazima eti uwepo Afrika. Muhimu ni kuwa utamaduni huo uwe umezaliwa na Waafrika katika jitihada zao za kutunza utu na heshima yao.

Kwahiyo unakuta sanaa ya kujilinda na dansi iitwayo “capoiera” maarufu huko Bahia, Brazili, inajulikana kama sanaa ya Kiafrika ingawa ukienda Afrika hutakuta “capoiera” kama ilivyo Brazili. Utaona hata imani za kidini kama Santeria, Vodoo, na nyinginezo huko Brazili, Cuba, Haiti, New Orleans, n.k. zinatambulika kama imani za asili ya Afrika ingawa yako mengi ambayo hutayaona Afrika katika imani hizo.

Umetaja suala la kuwa Afrika hawasherehekei mavuno mwezi Desemba. Jambo ambalo hujatazama ni kuwa Waafrika wa Marekani wanaishi Marekani na sio Afrika. Marekani mwezi Desemba ni mwezi unaochukuliwa kama ni wakati wa familia kukaa pamoja, kupumzika, na kufurahia mwisho wa mwaka na kujiandaa kwa mwaka mpya. Kwahiyo wamechagua mwezi huo kutokana na sababu zinazoendana na mazingira yao. Jambo ambalo nawaunga mkono kabisa.

Kuhusu Kiswahili wanachotumia: sioni ubaya wowote wa wao kuamua kutumia maneno kama “kuumba” kujibu wanaposalimiana. Kwakuwa nia yao ni kuenzi nguzo za Kwanzaa, sioni kuwa sababu hii itafanya sikukuu isiwe ya Kiafrika. Ndugu hawa wanajitafuta, na wanafaya mambo ambayo Waafrika wenyewe hawafanyi. Nadhani kuna kila sababu ya kuwaunga mkono kwakuwa wanachofanya ni kuunda utamaduni wa Waafrika wa Kimarekani. Utamaduni huo utakuwa ni wa kipekee maana wao ni wa kipekee. Tukumbuke kuwa wao sio tu Waafrika. Bali ni Wamarekani pia. Utamaduni wao hautakuwa kama Waafrika tulio Afrika na hautakuwa kama wa Wamarekani weupe walioko Marekani. Utakuwa ni utamaduni wa Kiafrika Kimarekani.

Utaona muziki kama wa Blues ambao ni wa Kiafrika. Chimbuko lake ni Afrika, huko Mali, Senegal, Guinea, n.k. Lakini wakati huo huo magitaa na vinanda wanavyotumia Waafrika wa Marekani kupiga muziki huo unaotambulika kuwa ni wa Kiafrika hayajatoka Afrika.

Kuhusu kusema “muhindi” badala ya “mhindi.” Wahindi pale Tanzania Kiswahili wanachotumia ni Kiswahili au sio Kiswahili? Je Wakongo Kiswahili chao ni Kiswahili au sio Kiswahili? Badala ya kusema “mtu” huwa wanasema, “mutu.” Kiingerea, kwa mfano, wanachotumia Wanigeria ni kiingereza bado ingawa sio kama Kiingereza cha Malikia. Muhindi na mhindi ni sawa tu na maharage na maharagwe, tofauti ambayo tunayo sisi tulioko Afrika. Tofauti hii haifanyi anayetumia neno hili kuwa Mwafrika zaidi ya mwingine.

Umezungumzia suala la sherehe ya kisintetiki. Nikuulize, nini kinafanya sherehe iwe ya asili? Sherehe ya asili au ya kitamaduni ni lazima iwepo miaka na miaka kabla yetu? Sikukuu zote (hata tunazoziita za asili) zina mwanzo wake. Uko wakati hazikuwa za asili. Tukianzisha sikukuu leo, baada ya miaka mingi, vizazi vijavyo vitaiona ya asili. Lakini ukweli ni kuwa sikukuu zote, mambo yote ya kitamaduni, kabla ya kuwa ya kiasili yalikuwa na mwanzo wake.

Tunapokuta ndugu hawa wanakosea mambo kama vile kuwa na majina wanayoamini kuwa ni ya Kiafrika kumbe sio, tunachotakiwa ni kuwasaidia badala ya kuwanyooshea kidole. Watajuaje tusipowasaidia? Watajuaje wakati Waafrika walioko Afrika majina hayo hawayatumii? Nadhani katika dunia ambayo tamaduni zisizo za Kimagharibi zimetikiswa na kupondwapondwa, wanapotokea watu au kundi wakitaka kuenzi Uafrika wao (hata kama haufanani nukta kwa nukta na Uafrika ulioko Afrika) ni kosa kubwa iwapo tutawaandama.

Suala la nini “utamaduni wa Afrika” ni gumu sana wakati mwingine. Tazama muziki wa Lingala wa Kongo ambao unafahamika kama muziki wa Kiafrika, wakati huo huo magitaa wanayotumia na vifaa vingine katika bendi zao havijatoka Afrika au sio vya asili ya Afrika.

Nadhani watu ambao walinyofolewa toka katika utamaduni wao miaka mingi iliyopita na kutumikishwa na kunyang’ganywa utu wao na haki za kutukuza utamaduni wao wanapojaribu kuenzi walikotoka sio jambo rahisi. Ni jambo gumu sana. Kumbuka kuwa watumwa walikatazwa kabisa kuenzi tamaduni zao. Waliadhibiwa vikali. Wanachofanya ni kupapasa huku na kule kujitafuta. Kwanzaa ni moja ya matokeo ya kupapasa huko.

Nimekutana na Waafrika wa Marekani wengi wakieleza masikitiko yake kuhusu jinsi Waafrika tuiotoka Afrika tunavyowanyooshea vidole bada ya la kusaidiana nao maana sisi tu wamoja ingawa pia tu tofauti. Wanashangaa kwanini tunapenda kuwatuhumu wakati ambapo sisi tunafanya kila tuwezalo ili kukimbia utamaduni wetu. Wao wanapojaribu kuutafuta, kuufufua, n.k. tunakimbia kutafuta mapungufu katika juhudi zao.

Nitamaliza kwa kusisitiza kuwa tusitegemee kuwa Waafrika wa Marekani watafanya mambo kama tunavyofanya Afrika. Haitakuwa hivyo maana mazingira ni tofauti kabisa. Wakati sisi ni Waafrika, wao ni Waafrika ila pia ni Wamarekani. --Ndesanjo 12 Januari 2006.