Nenda kwa yaliyomo

Maisha Nje ya Dunia

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Moja ya darubini za redio zinazotumika na mradi wa Breakthrough Listen kutafuta mawasiliano ya Viumbe hai nje ya Dunia

Maisha Nje ya Dunia (maarufu kama Viumbe wa Sayari Nyingine au Aliensi) ni kiumbe chochote hai ambacho asili yake si sayari ya Dunia.[1] Hadi leo, hakuna ushahidi wowote wa kisayansi uliothibitishwa kuwepo kwa maisha ya aina hiyo. Maisha haya yanajuisha kuanzia viumbe wadogo sana (kama vile bakteria) hadi viumbe wenye akili na ustaarabu, ambao huenda wakawa wameendelea zaidi au kuwa nyuma zaidi kulinganishwa na binadamu.[2] Sayansi inayochunguza uwezekano wa maisha haya inajulikana kama "Astrobiolojia" (Elimu ya Maisha katika Anga).

Dhana ya kuwepo kwa viumbe hai nje ya Dunia (Aliensi) ina historia ndefu. Kuanzia katikati mwa karne ya 20, utafiti hai ulianza kutafuta dalili za maisha nje ya Dunia. Uchunguzi katika Mfumo wa Jua umelenga sayari na miezi kama vile Mirihi (Mars), Europa (mwezi wa Mshtarii), na Titan (mwezi wa Zohali), kwa kuchunguza mambo muhimu yanayowezesha kiumbe hai kuishi.[3] Wakati huo huo, programu za kutafuta akili nje ya Dunia (kama vile SETI) zimetumia redio na darubini kuchunguza ishara za mawasiliano. Kuongezeka kwa uthibitisho wa sayari zinazozunguka nyota nyingine (Exoplanets) kumeongeza idadi ya maeneo ya utafiti kwa kiasi kikubwa.

Uwezekano wa kuwepo kwa Maisha Nje ya Dunia unajadiliwa sana kupitia kanuni kama vile Mlinganyo wa Drake (Drake equation), unaokadiria idadi ya ustaarabu unaoweza kuwasiliana katika galaksi ya Milky Way. Wanasayansi wengi wanaunga mkono Kanuni isiyo Maalum (Mediocrity Principle), wakisema kuwa Dunia haina nafasi ya kipekee na ni ajabu kama uhai utapatikana mahali pamoja tu. Hata hivyo, wengine wanashikilia "Nadharia ya Dunia Adimu" (Rare Earth hypothesis), wakidai kwamba mchanganyiko wa mambo uliosababisha uhai changamano duniani (kama vile uwepo wa Mwezi na eneo katika galaksi) ni nadra sana kujirudia.[4] Dhana ya viumbe nje ya Dunia imekuwa na athari kubwa katika utamaduni na tafiti za kisayansi, zikichochea mjadala kuhusu hekima ya kujaribu kuwasiliana na viumbe hao.

  1. Bennett, Jeffrey (2017). Life in the universe. United States: Pearson. pp. 3–4. ISBN 978-0-13-408908-9.
  2. Dick, Steven J. (1996). The Biological Universe: The Twentieth Century Extraterrestrial Life Debate and the Limits of Science. Cambridge. ISBN 978-0-521-34326-8.
  3. Dick, Steven J.; Strick, James E. (2004). The Living Universe: NASA And the Development of Astrobiology. Rutgers. ISBN 978-0-8135-3447-3.
  4. Ward, Peter D. (2005). Life as we do not know it-the NASA search for (and synthesis of) alien life. New York: Viking. ISBN 978-0-670-03458-1.
Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Maisha Nje ya Dunia kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.