Mafundisho ya Kibaha'i
Mafundisho ya Dini ya Kibaháʼí yanatokana na maandiko ya Baháʼu'lláh, mwanzilishi wake. Mkusanyiko wa maandiko ya Kibaháʼí unajumuisha vitabu na maandiko ya Báb na Baháʼu'lláh, pamoja na mazungumzo ya hadharani na maandiko ya ‘Abdu’l-Bahá, mwana wa mwanzilishi. Dhana kuu ya Dini ya Kibaháʼí ni umoja wa dini kuu za dunia (Uzoroasta, Uhindu, Uyahudi, Ubuddha, Ukristo, na Uislamu) kama sehemu ya mpango mmoja unaosimamiwa na Mungu mmoja. Mafundisho hayo pia yanazungumzia masuala ya kitheolojia ikiwa ni pamoja na umoja wa Mungu, umoja wa binadamu na umoja wa dini, pamoja na mambo juu ya maisha ya binadamu kama vile umoja wa sayansi na dini, kuondoa tofauti kubwa za utajiri na umaskini, elimu ya lazima kwa wote, na usawa wa watu wote, bila kujali jinsia, mbari, utaifa, rangi, au daraja la kijamii.[1][2]
Muhtasari
[hariri | hariri chanzo]Wakati wa safari za ‘Abdu’l-Bahá kuelekea magharibi kati ya mwaka wa 1911 na 1912-1913, alifafanua waziwazi misingi ya mafundisho ya Baháʼu’lláh, ambayo pamoja na sheria na kanuni za Kitáb-i-Aqdas zinaunda msingi wa Dini ya Kibaháʼí:
Utafutaji huru wa ukweli, bila kuathiriwa na ushirikina au mila; umoja wa binadamu wote, kanuni kuu na fundisho la msingi ya Dini hii; umoja wa dini zote; kupinga aina zote za upendeleo, uwe ni wa kidini, kikabila, kitabaka au kitaifa; maelewano yanayopaswa kuwepo kati ya dini na sayansi; usawa wa wanaume na wanawake, mbawa mbili ambazo kwazo ndege ya mwanadamu inaweza kuruka; utambulishi wa elimu ya lazima; kuwepo kwa lugha ya ulimwengu; kuondoa tofauti zilizokithiri za utajiri na umasikini; uanzishaji wa mahakama ya dunia ya kusuluhisha migogoro kati ya mataifa; kusifiwa kwa kazi inayofanywa katika roho ya huduma, hadi kiwango cha ibada; utukufu wa haki kama kanuni ya utawala katika jamii ya wanadamu, na dini kama ngome ya kuhifadhi watu na mataifa yote; na kuanzishwa kwa amani ya kudumu ya ulimwengu kama lengo kuu la wanadamu wote—.[3]
Umoja
[hariri | hariri chanzo]Kiini cha mafundisho ya Dini ya Kibaháʼí ni mada tatu kuu, Umoja wa Mungu, Umoja wa Dini na Umoja wa binadamu.[4] Maandiko ya kibaháʼí yanasema kwamba kuna Mungu mmoja mwenye nguvu zote ambaye hufunua ujumbe wake kupitia safu ya wajumbe au waelimishaji wa kiungu ambao mafundisho yao yanachangia “kuendeleza ustaarabu unaoendelea daima",[5] mchakato ambao unatazamwa kama mfululizo wa ufunuo kutoka kwa Mungu na kuelezwa kama "ufunuo unaoendelea".[6] Dini hii moja inayofunuliwa kwa hatua kwa hatua inatolewa kwa jamii moja ya binadamu, ambapo wote wana roho yenye kuelewa na ambao wanatofautiana tu kulingana na rangi na utamaduni. Wazo hili ni la kimsingi sio tu katika kuelezea imani za Kibaháʼí, bali pia katika kuelezea mtazamo wa Wabaháʼí kuelekea dini zingine, ambazo wanaziona kama zilizotoka kwa Mungu. Kukubalika kwa kila rangi na utamaduni duniani kumeleta utofauti katika jamii ya Wabaháʼí, ambayo imefanya Dini hii kuwa dini ya pili iliyosambaa zaidi duniani,[7] maandiko yake yametafsiriwa katika zaidi ya lugha 800.[8]
Umoja wa Mungu
[hariri | hariri chanzo]Mtazamo wa Kibaháʼí kuhusu Mungu ni kimsingi wa asili ya kuwa mmoja. Mungu ni nafsi isiyoharibika, isiyoumbwa ambayo ni chanzo cha uwepo wote.[7][9] Anajulikana kama "Mungu, asiyefahamika, asiyeweza kupatikana, chanzo cha Ufunuo wote, wa milele, mwenye ujuzi wote, anayekuwepo kila mahali na mwenye nguvu zote".[10][11] Ingawa yupo juu na hawezi kufikiwa moja kwa moja, mfano wake unaakisiwa katika uumbaji wake. Kusudi la uumbaji ni kwa kiumbe kilichoumbwa kuwa na uwezo wa kumjua na kumpenda muumba wake.[12]
Kwa mtazamo wa imani ya Kibaha'i, ingawa tamaduni na dini zinatofautiana juu ya maelezo yao kuhusu Mungu na asili yake, marejeleo hayo tofauti tofauti ya Mungu hata hivyo yanahusu Kiumbe yule yule mmoja. Tofauti hizo, badala ya kuchukuliwa kama mitazamo isiyoweza kupatanishwa ya tamaduni tofauti, zinaonekana kama zikionesha mahitaji yanayobadilika ya jamii ambazo kwazo ujumbe mtakatifu ulifunuliwa.[13]
Mafundisho ya Kibaháʼí yanasema kwamba Mungu ni mkuu sana kwa wanadamu kuweza kujua asili yake kwa usahihi. Katika ufahamu wa Kibaháʼí, sifa zinazotajwa kumhusu Mungu, kama vile Mwenye Nguvu Zote na Mwenye Upendo Wote zinatokana na uelewa mdogo wa wanadamu juu ya nguvu na upendo. Baháʼu'lláh alifundisha kwamba kumjua Mungu kunahusiana na kujua sifa na tabia ambazo zinaweza kufahamika kwetu, kwa hivyo ujuzi kamili wa Mungu hauwezekani. Aidha, Baháʼu'lláh anasema kwamba ujuzi wa sifa za Mungu unafunuliwa kwa wanadamu kupitia wajumbe wake.[14][15]
Kama vile ujuzi wetu wa mambo, hata yale juu ya vilivyoumbwa na vyenye mipaka, unavyohusu sifa zao na si asili yao, inawezekanaje kuelewa asili ya Uhalisia wa Kimungu, ambao hauna mipaka? ... Kumjua Mungu, kwa hivyo, kuna maanisha kuelewa na kujua sifa Zake, na si Uhalisia Wake. Ujuzi huu wa sifa pia unalingana na uwezo na nguvu za mwanadamu; sio kamili.[16][17]
Maandishi ya Kibahaí yamejaa majina na sifa za Mungu ambazo kupitia hizo, wanadamu wanaweza kupata kiwango fulani cha kumuelewa kama mmoja, na kuwa nafsi kuu na isiyojulikana.[10] Mafundisho ya Kibahaí yanasema kwamba mtu humkaribia Mungu kupitia sala, tafakari, kusoma maandiko matakatifu, na huduma.[7]
Umoja wa binadamu
[hariri | hariri chanzo]Maandiko ya Kibaha'i yanafundisha kwamba binadamu ni wamoja, na watu wote ni sawa mbele za Mungu. Dini ya Kibaha'i inasisitiza kwamba umoja wa binadamu ni wa msingi zaidi na wa umuhimu wa juu kuliko tofauti zozote za kimbari, kitaifa, kijinsia, kitabaka, na daraja la kijamii, huku ikisherehekea utofauti uliopo wa jamii hii ya binadamu.[4] ʻAbdu'l-Bahá anasema kuwa umoja wa wanadamu sasa umebaki kuwa "suala kuu na muhimu katika hali za kidini na kisiasa duniani." [7] Maandiko ya Kibaha'i yanathibitisha umoja wa kibailojia, kisiasa, na kiroho wa wanadamu, Baháʼu'lláh akisema:
Ninyi ni matunda ya mti mmoja, na majani ya tawi moja. Tendeaneni mmoja kwa mwingine kwa upendo na maelewano makuu, kwa urafiki na ushirika.[18][19]
Maandiko ya Kibaháʼí yanasisitiza kwamba mbari ya wanadamu wote ni asili moja iliyounganishwa, spishi (species) moja maalum,[20] Baháʼu'lláh alisema, "Tulikuumba nyote kutokana na mavumbi yale yale".[21] Maandiko ya Kibaháʼí yanaendelea kusisitiza kwamba tofauti kati ya mbari za watu, mataifa, na makundi ya kikabila ni juu juu tu (mfano rangi ya ngozi) au ni matokeo ya tofauti za malezi au elimu.[22] Mojawapo ya kanuni kuu ya mafundisho ya Kibaháʼí ni kuondoa aina zote za ubaguzi, ikijumuisha ule wa kikabila, kijinsia, kiuchumi na kijamii..[23]
Ubahá'í unafundisha kuwa ingawa utofauti wa kikabila na kitamaduni utaendelea kuwepo, mkumbatio wa kwanza wa binadamu utakuwa ule wa kwa jamii ya binadamu badala ya kundi lolote dogo kama vile mbari, taifa, au kikundi cha kikabila. Kutakuwa na mwisho si tu wa vita, bali pia wa ushindani kati ya makundi.
Ingawa maandiko ya Kibaha'i yanasisitiza umuhimu wa umoja wa ulimwengu na watu wake, umoja hauwezi kuwa ufanani (uniformity), maandiko hayo yanathibitisha thamani ya utofauti wa kitamaduni, kitaifa na ya mtu binafsi kupitia kanuni ya "umoja katika utofauti (unity in diversity)," na kusema kwamba wakati wa kutambua umoja wa wanadamu, utofauti wa kitamaduni unapaswa kusherehekewa.[4] Umoja katika utofauti mara nyingi huelezwa katika maandiko ya Kibaha'i kupitia mfano wa maua katika bustani ambapo maua yenye rangi tofauti yanaboresha uzuri wa bustani.[24]
[Imani] haipuuzi, wala haijaribu kukandamiza, utofauti wa asili wa kikabila, hali ya hewa, historia, lugha na utamaduni, mawazo na desturi, zinazotofautisha watu na mataifa ya ulimwengu...Kaulimbiu yake ni umoja katika utofauti...[25][26]
Umoja wa dini
[hariri | hariri chanzo]Mafundisho ya kibaháʼí yanabainisha kuwa kuna dini moja ambayo Mungu huifunua kwa wanadamu kwa muendelezo kupitia kwa manabii/wajumbe wake kadri jamii ya binadamu inavyokomaa na uwezo wake wa kuelewa unavyokua.[4][7] Maandiko ya Kibaháʼí yanathibitisha kuwa tofauti za nje kati ya dini zinatokana na mahitaji ya wakati na mahali ambapo kila dini ilifunuliwa.[7] Baháʼu'lláh alidai kuwa ndiye mjumbe wa Mungu wa hivi karibuni, lakini si wa mwisho, katika msururu wa waalimu wa kiroho ambao wanajumuisha, miongoni mwa wengine, Yesu, Buddha na Muhammad.[4][7]
Maandiko ya Kibaháʼí husema kwamba asili ya msingi ya wajumbe wa Mungu ni mbili, moja ni asili ya kibinadamu na nyingine ni asili ya kimungu. Wao ni wa kimungu kwa kuwa wote wanatoka kwa Mungu yule yule na kufafanua mafundisho yake. Hata hivyo, ingawa wanaweza kuonekana sawa, wao pia ni watu binafsi tofauti wanaojulikana kwa majina tofauti, kila mmoja akitimiza utume maalum na kusimamia ufunuo maalum.[6] Katika maandiko yake mengi, Baháʼu'lláh anasema kwamba kumkataa yoyote kati ya wajumbe wa Mungu ni sawa si tu na kuwakana wajumbe wake wote, bali pia kumkataa Mungu mwenyewe. Kuhusu uhusiano kati ya waelimishaji hawa, ambao Wabaháʼí huwaita Wadhihirishaji wa Mungu, Baháʼu'lláh anaandika:
Mungu ameagiza kuwa kuwafahamu Viumbe hawa Waliotakaswa kuwe sawa na kufahamu Nafsi Yake Mwenyewe. Yeyote anayewatambua ameutambua Mungu. Yeyote anayesikiliza mwito wao, amesikiliza Sauti ya Mungu, na yeyote anayeshuhudia ukweli wa Ufunuo wao, ameshuhudia ukweli wa Mungu Mwenyewe. Yeyote anayewaepuka, amemuepuka Mungu, na yeyote asiyeamini ndani yao, amemkataa Mungu... Hao ni Wadhihirishaji wa Mungu miongoni mwa watu, ushuhuda wa Ukweli Wake, na alama za utukufu Wake.[27][28]
Ufunuo Uendeleao
[hariri | hariri chanzo]Wabaháʼí wanaamini kuwa Mungu hufunua mapenzi yake kwa wanadamu mara kwa mara katika nyakati tofauti na sehemu tofauti kupitia wajumbe/manabii wanaojulikana kama Wadhihirishaji wa Mungu, kila mmoja wao huanzisha agano na dini. Kulingana na maandiko ya Kibaháʼí, mchakato huu wa ufunuo ni wa milele, kinyume na mifumo mingi ya imani nyingine ambazo huamini kuwa nabii/mjumbe wao kuwa wa mwisho.[29] Mada kuu ya dini zinazofuatana na endelevu zilizoanzishwa na Wadhihirishaji wa Mungu ni kwamba kuna mwelekeo wa mabadiliko, na kwamba kila Mdhihirishaji wa Mungu huleta kiwango kikubwa zaidi cha ufunuo (au dini) kwa wanadamu kuliko ya awali.[30]
Tofauti kati ya ufunuo ulioletwa na Mdhihirishaji wa Mungu mmoja na mwingine hautokani na sifa bainifu zinazomtofautisha Mdhihirishaji mmoja wa Mungu na mwingine, bali hutokana na mambo mbalimbali ya kidunia, kijamii na kibinadamu,[30] tofauti hizi huendana na "hali", "mahitaji yanayobadilika ya zama" na "uwezo wa kiroho" wa wanadamu.[30] Tofauti hizi zinatambuliwa kuwa zinahitajika kutokana na ukweli kwamba jamii ya wanadamu imekuwa ikisonga polepole kutoka hatua moja hadi nyingine ya juu zaidi ya umoja kutoka familia hadi makabila na kisha mataifa.[30]
Kila mjumbe alitangaza maadili na ukweli wa kiroho wa milele ambao ulifanywa upya na wajumbe waliokuja baada yake, ambapo mafundisho ya kila mmoja yalionyesha mabadiliko ya kiroho na kimwili ya kipekee ya binadamu wa wakati huo.[29] Kulingana na mtazamo wa Kibaháʼí, kwa vile uwezo wa kiroho wa jamii ya wanadamu na upokevu umeongezeka kutoka kipindi kimoja hadi kingine, kiwango ambacho kweli hizi za kiroho zimefafanuliwa hubadilika.[30]
Baháʼu'lláh alifafanua kwamba kuonekana kwa mitume wanaofuatana ni kama ujio wa kila mwaka wa Masika, ukileta uhai mpya kwa dunia ambayo imeshapuuza mafundisho ya mjumbe aliyetangulia.[29] Alitumia pia mfano wa dunia kama mwili wa mwanadamu, na ufunuo kama nguo ya "haki na hekima".
Baháʼu'lláh alitaja katika Kitáb-i-Íqán kwamba Mungu atafufua "Mji wa Mungu" karibu kila baada ya miaka elfu moja, na alitaja hasa kwamba Mdhihirishaji wa Mungu mwingine hatatokea ndani ya miaka 1000 tangu ujumbe wa Baháʼu'lláh.[31]
Agano
[hariri | hariri chanzo]Agano ni makubaliano kati ya makundi ya watu yanayojumuisha majukumu yaliyokubaliwa kwa pamoja. Agano katika Dini ya Kibaháʼí, ambalo linajulikana kama 'kitovu cha wanadamu na ambalo hukakikisha umoja wa Imani', linahusu maagano mawili mahususi yanayopatikana katika historia ya dini. La kwanza ni Agano Kuu ambalo hufanyika kati ya kila Mdhihirishaji wa Mungu na wafuasi wake kuhusu ahadi ya ujio wa Mdhihirishaji anayefuata. Kama ilivyooneshwa katika unabii, kila Mdhihirishaji, wakiwemo Ibrahimu, Musa, Yesu, Muhammad, Báb na Baháʼu'lláh, walitabiri ujio wa atakayefuata, wafuasi wao wanawajibika kuchunguza madai ya Mdhihirishaji yeyote anayofuata. Agano Dogo linahusu Mdhihirishaji na mrithi wake anayemfuata baada ya kutoweka kwake, ambapo Bahá’u’lláh alimchagua ʻAbdu'l-Bahá kama kitovu cha agano lake katika Kitabu cha Agano lake. Katika Wosia na Agano lake, ʻAbdu'l-Bahá aliwaelekeza waumini kumfuata Shoghi Effendi, ambaye naye aliahidi mwendelezo wa mwongozo wa kiungu kupitia Nyumba ya Haki ya Ulimwengu ambayo ingeundwa. Agano la Kibaháʼí pia linahusu agano la jumla zaidi ambalo, kwasababu hutupa neema zake nyingi, Mungu anadai kutambulika kwa Mitume wake na utiifu kwa sheria zake.[32]
Kanuni za Kijamii
[hariri | hariri chanzo]Wakati wa ziara zake barani Ulaya na Amerika ya Kaskazini, 'Abdu'l-Bahá mara kwa mara alielezea kwa muhtasari maeneo muhimu yanayohusiana na imani ya Kibaháʼí katika orodha za kanuni ambazo zinajumuisha zifuatazo.[33] Orodha hiyo si rasmi na zipo aina mbalimbali za orodha kama hii.[34][35]
Usawa wa wanawake na wanaume
[hariri | hariri chanzo]Mafundisho ya Dini ya Kibaháʼí yanathibitisha usawa wa wanawake na wanaume, Baháʼu'lláh alisema kuwa Mungu sasa ameondoa tofauti ambazo hapo awali zilikuwa zikitenganisha hadhi za wanaume na wanawake. Hivyo, wanawake na wanaume ni sawa mbele ya Mungu. Katika maandiko na hotuba zake ʻAbdu'l-Bahá alisisitiza mara kwa mara usawa wa kijinsia kuwa mojawapo ya mafundisho tofauti ya Dini ya Kibaháʼí, akisema kuwa wanawake na wanaume wote wanamiliki uwezo sawa kwa fadhila na akili; pia alilinganisha hadhi ya wanawake na wanaume na maendeleo ya ustaarabu na bawa mbili za ndege ambapo tu ikiwa bawa zote mbili zina nguvu, ndipo ndege ya mwanadamu itaweza kuruka. Wanawake na wanaume wanapaswa kupewa fursa sawa katika masuala ya elimu, ikiwa ni pamoja na kupata mtaala sawa, wakati huo huo wakipewa haki sawa za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Ingawa mafundisho ya Kibaháʼí yanathibitisha usawa kamili wa kiroho na kijamii wa wanawake na wanaume, yanathibitisha utofauti wa kijinsia katika baadhi ya maeneo ya maisha. Wanawake na wanaume wanatambuliwa kuwa na nguvu na uwezo tofauti unaowawezesha kutimiza majukumu tofauti vizuri zaidi. Hivyo basi, kuna mafundisho fulani ambayo yanawapa wanaume upendeleo katika hali fulani ndogo na mengine yanawapa wanawake upendeleo, moja ya vipengele hivi inahusiana na hali halisi ya kibaolojia ya uwezekano wa kuwa mama kwa wanawake. ʻAbdu'l-Bahá alisema kwamba inapobidi, wasichana wanapaswa kupewa kipaumbele cha elimu kwa kuwa kama mama watarajiwa, watakuwa waalimu wa kwanza wa watoto wao.[36]
Katika suala la utawala wa Kibaha'i, nyadhifa zote isipokuwa ujumbe kwenye Nyumba ya Haki ya Ulimwengu ziko wazi kwa wanawake na wanaume. Ingawa hakuna sababu maalum iliyotolewa juu ya hili, ʻAbdu'l-Bahá amesema kuwa kuna hekima ndani yake ambayo hatimaye itaeleweka.[36]
Upatano wa dini na sayansi
[hariri | hariri chanzo]Upatano wa sayansi na dini ni kanuni kuu ya mafundisho ya Kibaháʼí,[37] ikisisitiza kwamba sayansi ya kweli na dini ya kweli lazima viwe na upatano, na hivyo ikikataa maoni kwamba sayansi na dini ziko kwenye mgongano. ʻAbdu'l-Bahá alisisitiza kwamba dini inayotegemea ushirikina na ambayo haiendani na sayansi bali inategemea dhana na mawazo ya kibinadamu, inapaswa kukataliwa. Wakati dini ina upatano na sayansi, msingi wake ni thabiti, na ina uwezo wa kuathiri moyo wa mwanadamu.[38] ʻAbdu’l-Bahá pia alithibitisha kwamba nguvu za kufikiri na kuchambua zinahitajika ili kuelewa kweli za dini,[37] na alilaani ustaarabu unaotegemea mambo ya kimwili tu bila kuzingatia dini ambayo, licha ya ubora wa kiteknolojia, huibua maovu ya kimaadili kama vile vita.[37]
Elimu ya ulimwengu
[hariri | hariri chanzo]Mafundisho ya Imani ya Kibaháʼí yanasisitiza umuhimu wa elimu, ya kidini na isiyo ya kidini, kama sehemu muhimu katika maendeleo ya jamii, yakiwa na mkazo wa kukuza elimu ya kiroho na maadili pamoja na sanaa, biashara, sayansi na taaluma. Katika maandiko yake, Baháʼu'lláh alisema kwamba uwezo wa kiroho wa mtu binafsi unaweza tu kupatikana kupitia elimu ya kiroho, hili likikazia uhitaji wa elimu ya kiroho/dini kwa watoto tangu wakiwa na umri mdogo. Kwa muktadha huu, mafundisho ya Kibaháʼí yanasisitiza kuwa ni jukumu la wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata elimu, huku kipaumbele kikitolewa kwa elimu ya wasichana.[39]
Lugha msaidizi ya ulimwengu
[hariri | hariri chanzo]Mafundisho ya Kibaha'i yanaona kuboreshwa kwa mawasiliano kati ya watu wote ulimwenguni kuwa na umuhimu mkubwa katika kuleta umoja na amani duniani.[40] Wingi wa lugha zinazotumika hivi sasa unachukuliwa kuwa kikwazo kikubwa kwa umoja, zikizuia mtiririko huru wa taarifa na kufanya iwe vigumu kwa mtu wa kawaida asiye na lugha mbili kupata mtazamo wa ulimwengu juu ya matukio ya dunia.[41]
Baháʼu’lláh alihimiza wanadamu kuchagua lugha msaidizi itakayofundishwa shuleni pamoja na lugha ya kienyeji ili watu wa ulimwengu waweze kuelewana popote wanapokwenda duniani.[42] Baháʼu’lláh alisisitiza kwamba umoja kamili kati ya sehemu mbalimbali za ulimwengu utaendelea kuwa ndoto hadi kupitishwa kwa lugha msaidizi.[43]
Baháʼu'lláh pia alisisitiza kwamba lugha msaidizi haipaswi kwa namna yoyote kukandamiza lugha za asili zilizopo, huku dhana ya umoja katika utofauti ikitumika kwa lugha kama ilivyo kwa tofauti zingine.[41] Mafundisho ya Kibaháʼí yanatamka kwamba utofauti wa kitamaduni unapatana na umoja, na kwamba kwa vile jamii ya binadamu inatajirishwa na tamaduni nyingi duniani sasa ni wakati wa kukumbatia utofauti wa kitamaduni katika jitihada za kupata umoja.[44] Mafundisho ya Kibaháʼí pia yanatamka kwamba kuwa na lugha ya kimataifa msaidizi kungeondoa shinikizo la asili la kukuza vikundi vya lugha vyenye idadi kubwa ya watu na kusaidia kuhifadhi lugha za wachache, wakati huo huo kuhifadhi tamaduni za wachache.[41]
Kuondoa Umasikini na Utajiri Uliopitiliza
[hariri | hariri chanzo]Mafundisho ya imani ya Kibaháʼí yanasema kwamba kuondoa umasikini na utajiri uliopitiliza ni muhimu, [45] ʻAbdu'l-Bahá akizingatia kwamba hali hizi mbili zinakwamisha jamii yenye huruma kwa kuwa umasikini uliopitiliza unavunja moyo maskini, na utajiri uliopitiliza unawaelemea matajiri. Baháʼu’lláh aliamuru kwamba matajiri wanapaswa kuwalinda maskini, ambao ni amana ya kimbingu, na ili kushughulikia hali hizi mbili za utajiri na umasikini na kuhakikisha ustawi wa watu wote, mafundisho ya Kibahá’i yanaagiza kuwepo kwa asasi zenye ufanisi, ikiwemo ya Huqúqu'lláh, na kukuza hisia za kujali jamii kwa pamoja.[46]
Wote Báhá’u’lláh na ʻAbdu’l-Bahá walianzisha mpangilio mpya wa kiuchumi wa jamii kama njia ya kuondoa viwango vya juu vya umaskini na utajiri, lakini ingawa walisisitiza umuhimu wa heshima na haki sawa kwa wote bila kujali hadhi ya kijamii, hawakuunga mkono falsafa za jamii au ujamaa, Báhá’u’lláh alihalalisha umiliki binafsi wa mali na haki ya kuhamisha hati za mali. [46] ʻAbdu'l-Bahá aliongeza kuwa ingawa kutokujishughulisha na mambo ya kidunia ni sifa nzuri, utajiri wenyewe si mbaya, na katika hali zingine unamwezesha mtu kutoa msaada kwa jamii kupitia kuendeleza ustawi wa kijamii na elimu.[45]
Uchunguzi Huru wa Ukweli
[hariri | hariri chanzo]Baháʼu'lláh alifundisha kwamba kila mtu lazima achunguze ukweli kwa uhuru, bila kufuata kwa upofu imani za wengine au kutegemea ushirikina na mila kama vyanzo vya maarifa.[47] Maandiko ya Kibaháʼí husema kwamba ili kuchunguza ukweli, mtu lazima aachane na upendeleo wowote, huku yakisisitiza kwamba kwa kuwa Ukweli wa msingi wa uhalisia wa kila kitu ni mmoja, uchunguzi huru ni hatua yenye nguvu kuelekea umoja wa binadamu.[48]
Wabaháʼí wanahimizwa kutafakari na kufikiri kila siku juu ya maandiko ya Kibaháʼí[49] katika kile ambacho kimeelezewa kama "mchakato wa milele au usio na mwisho" wa kutafuta ukweli.[50] Safari hii inaweza kuwa na kipengele cha kiroho ambapo mtafutaji wa ukweli anaendeshwa na mvuto wake kwa uzuri wa Mungu, kama ilivyoangaziwa katika maandiko ya kiroho yenye mafumbo ya Baháʼu'lláh, kama vile 'Mabonde Saba'.[51]
Mafundisho ya Kibaháʼí yanaeleza kwamba kwa kuwa binadamu wana "nafsi yenye utashi", wao ni wa kipekee kati ya aina zote za viumbe.[52] ʻAbdu’l-Bahá alisema kwamba ili kukuza uwezo huu wa utashi "Mungu ametupa akili yenye utashi kwa madhumuni haya, kuchunguza mambo yote, kutambua ukweli".[53] Sambamba na uwezo wa kuchambua mambo, mafundisho ya Kibaháʼí pia yanasema kuwa imani ni sifa ya roho ya mwanadamu. Wakati mwingine hufikiriwa kuwa kuna tofauti kati ya moyo na akili au imani na uwezo wa kuchambua mambo, kwa Wabaháʼí, imani si upofu usio wa mantiki kwa ukweli. Shoghi Effendi anasisitiza kwamba Baháʼu'lláh "hatutaki tumfuate kwa upofu" na anawahimiza Wabaháʼí "Kusoma maneno Yake [Baháʼu'lláh], kuzingatia mafundisho Yake, na kupima thamani yake kwa mwangaza wa matatizo ya kisasa".[54] Kwa Wabaháʼí neno imani linaonesha maana ya "maarifa ya kukusudia" na imani inayojionesha katika "utendaji wa matendo mema".[55] Imani pia inapaswa kujumuisha kuhudumia maslahi ya umma kwa dhati na moyo wote.[56] Hivyo, katika Imani ya Kibaháʼí, kama alivyoandika mwandishi mmoja, "kuchambua mambo ni muhimu lakini hakutoshi".[57] Vyote viwili, imani na uchambuzi wa mambo yote yanahitajika ili kufikia uhalisia na ukweli.
Mafundisho ya Kiroho
[hariri | hariri chanzo]Maandishi ya Kibaha'i yana marejeo mengi kuhusu sifa za kiroho na maadili ambayo watu binafsi wanapaswa kujitahidi kuendeleza. Vipengele vya tabia njema ni pamoja na, kati ya vingine, uaminifu,[58] ukweli,[59] usafi wa nia, heshima, kuepuka kusengenya, huduma, haki, kiasi, usafi, vyote vikiwa ndani ya mazingatio ya utashi na maarifa.[60][61]
Mungu anaelezewa katika maandiko ya Dini ya Kibaháʼí kama ni mmoja, wa kipekee, asiyeweza kufikiwa, mjuzi wa mambo yote, yupo kila mahali, asiyeharibika, na mwenye nguvu zote Mungu ambaye ni muumba wa vitu vyote katika ulimwengu.[62] Uwepo wa Mungu na ulimwengu unafikiriwa kuwa wa milele, bila mwanzo wala mwisho.[63] Mafundisho ya Dini ya Kibaháʼí yanadai kwamba Mungu yuko juu zaidi ya ufahamu wa wanadamu, na kwamba ufahamu wa kibinadamu kuhusu Mungu unawezekana tu kupitia kwa Maandiko Yake.[64][65] Kwa kuwa Mungu yuko juu ya ufahamu wa akili ya kibinadamu, ujuzi juu yake unawezekana tu kupitia kwa sifa na tabia zake, kama vile mwenye nguvu zote, mpendwa wote, mwenye haki isiyo na kipimo, maneno ambayo yana mipaka kulingana na uzoefu wa kibinadamu.[66] Kanuni za kijamii zinazofundishwa na Wadhihirishaji wa Mungu zinatoa mazingira ambamo ukuaji wa kiroho unawezeshwa, na kusudi la kweli la jamii linafanywa liwezekane,[67] kusudi la binadamu likiwa ni kujifunza kumjua na kumpenda Mungu kupitia mbinu kama sala, tafakari na kutoa huduma kwa wanadamu.[64]
Maandiko ya Kibaháʼí yanaeleza kuwa wanadamu wana "nafsi yenye utashi" ambayo inampa mwanadamu uwezo wa kipekee wa kutambua daraja la Mungu na uhusiano wa wanadamu na Muumba wao. Kila mwanadamu anaonekana kuwa na wajibu wa kumtambua Mungu kupitia kwa wajumbe wake, na kufuata mafundisho yao.[68] Kupitia utambuzi na utiifu, kuwatumikia wanadamu na maombi ya mara kwa mara pamoja na matendo mema, maandiko ya Kibaháʼí yanaeleza kwamba nafsi inakuwa karibu na Mungu, ambalo ni lengo la kiroho katika imani ya Kibaháʼí. Mwanadamu anapokufa, nafsi yake inahamia ulimwengu mwingine, ambapo maendeleo yake ya kiroho katika duniani hii ya muumbo huwa ni msingi wa hukumu na maendeleo katika ulimwengu wa kiroho. Wabaháʼí wanaamini katika maisha ya milele ya roho tofauti na ule mtazamo wa roho kuingia tena katika maisha ya mwili. Mbingu na Jehanamu hufundishwa kuwa ni hali za kiroho za ukaribu au umbali na Mungu ambazo zinaeleza mahusiano katika ulimwengu huu na ule ujao, na si mahali pa kimwili pa malipo (zawadi) na adhabu baada ya kifo.[69]
Muundo
[hariri | hariri chanzo]Kipengele cha msingi na muhimu kwa maendeleo, ukuaji, na umoja wa Dini ya Kibaha'i ni Utaratibu wake wa Kiutawala.[70] Agano la Baháʼu'lláh linaunda hati ya msingi kwa dini yake, nyaraka kuu zikiwa ni Kitáb-i-Aqdas na Kitab-i-‘Ahd na Wosia na Agano la ʻAbdu'l-Bahá[71]ambayo ni hati ya maendeleo ya Mfumo wa Kiutawala. Asasi za Utawala zinagawanyika katika makundi mawili tofauti, linalochaguliwa na linaloteuliwa, yote yakiongozwa na Nyumba ya Haki ya Ulimwengu,[72]ambayo iko Haifa, Israel.[73]
Mashauriano kama mbinu ya kutatua tofauti
[hariri | hariri chanzo]Mashauriano ni kipengele cha msingi katika utendaji wa asasi za Kibaháʼí katika ngazi zote za utawala, na ni mbinu ya uamuzi ambayo asasi zote za Dini ya Kibaháʼí zinatumia. Mashauriano yanawezesha mchakato wa uamuzi ambapo wote wanaoshiriki wanahimizwa kueleza mawazo yao kwa uhuru bila kukosolewa, na ambao unalenga kugundua ukweli kupitia ushiriki wa wote na ushirikiano wenye nidhamu.[74]
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ Cole 2012, p. 438–446.
- ↑ Smith 2008, pp. 52–53
- ↑ Effendi 1944, pp. 280–282.
- 1 2 3 4 5 Hutter 2005, pp. 737–740
- ↑ Hatcher Martin, William S na J. Douglas (1985). The Baha'i Faith. The emergence of a global religion. Australia: Harper &Row. uk. 2.
- ↑ Hatcher Martin, William S J.Douglas (1985). The Baha'i Faith. The emerging global religion. Australia: Harper &Row. uk. 82.
- 1 2 3 4 5 6 7 Britannica 1988
- ↑ The National Spiritual Assembly of the Baha'is of the United States 2006.
- ↑ Hatcher & Martin 1985, p. 74
- 1 2 Smith 2008, p. 106
- ↑ Effendi 1944, p. 139
- ↑ Smith 2008, p. 111
- ↑ Britannica 2005, p. 797
- ↑ Adamson 2007, pp. 186–188
- ↑ Smith 2008, pp. 107–108
- ↑ Hatcher 1980, p. 32
- ↑ ʻAbdu'l-Bahá 2014, pp. 220–21
- ↑ Hatcher & Martin 1985, p. 78
- ↑ Baháʼu'lláh 1976, p. 288
- ↑ Hatcher, Martin, William S. J. Douglas (1986). The Baha'i Faith. The emerging global religion. Australia: Harper & Row. uk. 75.
- ↑ Hatcher Martin, William S. J. Douglas (1986). The Baha'i Faith. The emergence of a global religion. Australia: Harper & Row. uk. 87.
- ↑ Hatcher & Martin 1998, pp. 75–76
- ↑ Danesh & Fazel 2004, p. 35
- ↑ Hatcher & Martin 1998, p. 79
- ↑ Lepard 2003, p. 50
- ↑ Effendi 1938, p. 41
- ↑ Baháʼu'lláh 1976, p. 346
- ↑ Momen 2012, p. 117
- 1 2 3 Smith 2000, pp. 276–277
- 1 2 3 4 5 Lundberg 1996
- ↑ McMullen 2000, p. 7
- ↑ Smith 2000, p. 114.
- ↑ Smith 2008, p. 52.
- ↑ Bausani 2007.
- ↑ Cole 1989
- 1 2 Smith 2000, pp. 358–359.
- 1 2 3 Smith 2000, pp. 306–307
- ↑ Smith 2000, pp. 290–91
- ↑ Smith 2000, pp. 130–31
- ↑ Smith 2008, p. 139
- 1 2 3 Hatcher Martin, William s. J. Douglas (1986). The baha'i Faith. The emerging global religion. Australia: Harper & Row. ku. 95–96.
- ↑ Stockman 2000, p. 9
- ↑ Esslemont 1980, p. 164
- ↑ Meyjes 2006, p. 27
- 1 2 Smith 2000, pp. 128–29
- 1 2 Smith 2008, pp. 142–43
- ↑ Gandhimohan 2000
- ↑ Smith 2000, p. 195
- ↑ Schaefer 1992.
- ↑ Lambden 1982, p. 69–80.
- ↑ Ferraby, John (2011). All things made new : a comprehensive outline of the Bahá'í faith. New Delhi : Bahá'í Publishing Trust. ku. 139–142.
- ↑ Baha, Abdu'l. The Secret of Divine Civilization. Baha'i Pub. Trust. uk. 3.
- ↑ Baha, Abdu'l. 'Abdu'l-Bahá on Divine Philosophy. Tudor Press. uk. 102.
- ↑ Effendi 2021.
- ↑ Baha, Abdu'l. Tablets of ‘Abdu’l-Bahá. Juz. la 3. uk. 549.
- ↑ Baha, Abdu'l. The Secret of Divine Civilization. Baha'i Pub. Trust. ku. 96–7.
- ↑ Kluge 2013.
- ↑ Smith 2000, p. 342
- ↑ Smith 2000, pp. 342–343
- ↑ Smith 2000, pp. 327–328
- ↑ Smith 2000, pp. 326–327
- ↑ Smith 2008, p. 106
- ↑ Britannica 1992
- 1 2 Hatcher 2005, pp. 1–38
- ↑ Cole 1982, pp. 1–38
- ↑ Hatcher & Martin, William s. J.Douglas (1985). The Baha'i Faith. The emerging global religion. San Francisco: Harper and Row. ku. 123–124.
- ↑ Hatcher. Martin, William S. J.Douglas (1985). The Baha'i Faith. The emerging global religion. San Francisco: Harper & Row. uk. 114.
- ↑ McMullen 2000, pp. 57–58
- ↑ Masumian 1995
- ↑ Stockman, Robert (2022). The world of the Baha’i Faith. Abingdon: Routledge. uk. 426.
- ↑ Stockman, Robert (2022). The world ofthe Baha’i Faith. Abingdon: Routledge. uk. 412.
- ↑ Stockman, Robert (2022). The world ofthe Baha’i Faith. Abingdon: Routledge. ku. 426–427.
- ↑ Stockman, Robert (2022). The world ofthe Baha’i Faith. Abingdon: Routledge. uk. 431.
- ↑ Stockman, Robert H (2022). The World of the Baha'i Faith. Abingdon: Routledge. uk. 438.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ʻAbdu'l-Bahá (2014). Maswali Baadhi Yaliyotibiwa (tol. la Toleo jipya lililosahihishwa). Haifa, Israeli: Kituo cha Ulimwengu cha Baháʼí. ISBN 978-0-8774-3374-3.
- Baháʼu'lláh (1976). Mkusanyiko wa Maandiko ya Baháʼu'lláh. Wilmette, Illinois, Marekani: Baháʼí Publishing Trust. ISBN 0-8774-3187-6.
- The National Spiritual Assembly of the Baha'is of the United States (2006). "Maandiko ya Baháʼí". bahai.us. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2006-08-05. Iliwekwa mnamo 2006-08-03.
- Kluge, Ian (2008). "Pomoja na Maandiko ya Bahá'í". Lights of Irfan: 118.
- Saiedi, Nader (2008). Lango la Moyo: Kuelewa Maandiko ya Báb. Kanada: Wilfrid Laurier University Press. ISBN 978-1-5545-8056-9. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2024-01-02. Iliwekwa mnamo 2021-04-07.
- Baha'i World Centre (10 Machi 2008). "Asilimia ya Wajumbe wa Bunge la Kiroho la Kitaifa ambao ni Wanawake, 1953-2007". Takwimu. Baháʼí Library Online. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2010-10-06. Iliwekwa mnamo 2010-08-08.
- Schaefer, Udo (1992). "Changamoto kwa Masomo ya Bahá'í". Baháʼí Studies Review. 2:!.
- Schaefer, Udo (2006). "Baadhi ya Vipengele vya Maadili ya Bahá'í". The 20th Hasan M. Balyuzi Memorial Lecture: 4.
- Cole, Juan (30 Desemba 2012) [15 Desemba 1988]. "BAHAISM i. Dini". Encyclopædia Iranica. Juz. la III/4. New York: Chuo Kikuu cha Columbia. ku. 438–446. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 23 Januari 2013. Iliwekwa mnamo 5 Januari 2021.
- "Wanawake katika Mabunge ya Kitaifa". Muungano wa Mabunge ya Kati Kati. 30 Juni 2010. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2007-03-30. Iliwekwa mnamo 2010-08-16.
- Juan R. I. Cole (Mei 1999) [Juni 1998]. "Imani ya Baha'i huko Amerika kama Panopticon, 1963-1997". The Journal for the Scientific Study of Religion. 37 (2): 234–248. ISSN 0021-8294. OCLC 7789869572. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Novemba 9, 2012. Iliwekwa mnamo Aprili 1, 2021.
{{cite journal}}: CS1 maint: date auto-translated (link) - Effendi, Shoghi (1944). Mungu Anapita. Wilmette, Illinois, Marekani: Baháʼí Publishing Trust. ISBN 0-8774-3020-9.
- Effendi, Shoghi (1938). Mpangilio wa Dunia wa Baháʼu'lláh - Barua Zilizochaguliwa. Wilmette, Illinois, Marekani: Baháʼí Publishing Trust. ISBN 0-8774-3231-7.
- Effendi, Shoghi (2021). "Uchanganuzi wa Usomi". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-08-01. Iliwekwa mnamo 2021-04-07.
- Baha, Abdu'l (2021). Siri ya Ustaarabu wa Kiungu. US Bahá’í Publishing Trust. uk. 96. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-05-12. Iliwekwa mnamo 2021-04-08.
- Bausani, Alessandro (2007). "Wabahá'í". Encyclopaedia of Islam Online. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 7 Mei 2007. Iliwekwa mnamo 2007-05-03.
- Lambden, Stephen (1982). ""Problemu za Usomi wa Dr. MacEoin...": Mawazo Kadhaa". Bahá'í Studies Bulletin. 1 (3): 69–80. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2022-05-22. Iliwekwa mnamo 2021-04-08.
- Chamberlain, Isabel Fraser (1918). Abdul Baha kuhusu Falsafa ya Kiungu. Tudor Press. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-03-04. Iliwekwa mnamo 2021-04-08.
- Moojan Momen (2007). "Uko Kando na Usaliti katika Jamii ya Bahá'í". Dini. 37 (3): 187–209. doi:10.1016/j.religion.2007.06.008. ISSN 0048-721X. OCLC 4926459513. S2CID 55630282. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo Oktoba 6, 2010. Iliwekwa mnamo Aprili 1, 2021.
- Adamson, Hugh (2007). Kamusi ya Kihistoria ya Dini ya Baháʼí. Oxford, Uingereza: Scarecrow Press. ISBN 978-0-8108-3353-1.
- Britannica (1988). "Dini ya Baháʼí". Kitabu cha Mwaka cha Britannica. Chicago: Encyclopædia Britannica. ISBN 0-8522-9486-7.
- Britannica (1992). "Dini ya Baháʼí". Katika Daume, Daphne; Watson, Louise (whr.). Kitabu cha Mwaka cha Britannica. Chicago: Encyclopædia Britannica. ISBN 0-8522-9486-7.
- Britannica (2005). "Dini ya Baháʼí". Britannica Micropaedia. Chicago: Encyclopædia Britannica. ISBN 1-5933-9236-2.
- Cole, Juan (1989). "Dini ya Bahai". Nakala iliyohifadhiwa. Encyclopædia Iranica. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2009-01-02. Iliwekwa mnamo 2025-03-15.
- Cole, Juan (1982). "Dhima ya Udhibiti katika Maandishi ya Baháʼí". Masomo ya Baháʼí. monograph 9: 1–38.
- Danesh, John; Fazel, Seena (2004). Kutafuta Maadili: Maadili katika Mawazo ya Baha'i (Masomo katika Dini za Babi na Baha'i). Kalimat Press. ISBN 1-8906-8832-0.
- Fisher, Mary Pat (1996). Maisha ya Dini: Ensaiklopedia ya Imani za Dunia. I B Tauris & Co Lt. ISBN 1-8606-4148-2.
- Esslemont, J.E. (1980). Baháʼu'lláh na Enzi Mpya (tol. la 5th). Wilmette, Illinois, USA: Baháʼí Publishing Trust. ISBN 0-8774-3160-4.
- Gandhimohan, M. V. (2000). "Mafundisho ya Baháʼí". Mahatma Gandhi na Baháʼí: Kupambana na Ustaarabu Usiotumia Nguvu. New Delhi: Baháʼí Publishing Trust of India.
- Hatcher, William; Martin, Douglas (1985). Dini ya Baháʼí. San Francisco: Harper & Row. ISBN 1-9318-4706-1.
- Hatcher, William (Aprili 1980). "Sayansi ya Dini" (PDF). Masomo ya Baháʼí. 2. Association for Baháʼí. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo (PDF) mnamo 2011-07-18.
- Hatcher, W.S.; Martin, J.D. (1998). Dini ya Baháʼí: Dini Inayoinuka ya Dunia. Wilmette, Illinois, USA: Baháʼí Publishing Trust. ISBN 0-8774-3264-3 – kutoka Google Books.
- Hatcher, John S. (2005). "Kufunua Hurí ya Upendo". Jarida la Masomo ya Baháʼí. 15 (1): 1–38.
- Hutter, Manfred (2005). "Wabahá'í". Katika Ed. Lindsay Jones (mhr.). Encyclopedia of Religion. Juz. la 2 (tol. la 2nd). Detroit: Macmillan Reference USA. ISBN 0-0286-5733-0.
- Klebel, Wolfgang (2016). "Lugha ya Moyo: Kutoka kwa Lugha ya Ndoto kuelekea Kuelewa Lugha ya Moyo". Lights of Irfan. 17: 65–110.
- Kluge, Ian (2013). Iraj Ayman (mhr.). "Mantiki na Maandishi ya Bahá'í". Lights of 'Irfán. 14. Wilmette, IL: Haj Mehdi Armand Colloquium: Haj Mehdi Arjmand Memorial Fund: 163–232. ISBN 978-3-9424-2618-3. Iliwekwa mnamo Aprili 1, 2021.
- Lepard, Brian D. (2003). Kutafakari Upya Jitihada za Kibinadamu: Njia Mpya ya Kisheria Inayotegemea Kanuni za Msingi za Maadili katika Sheria ya Kimataifa na Dini za Dunia. Pennsylvania State University Press. ISBN 0-2710-2313-9.
- Lundberg, Zaid (1996). Apokaliptisimu ya Baha'i: Dhima ya Ufunuo unaoendelea. Idara ya Historia ya Dini katika Kitivo cha Theolojia, Chuo Kikuu cha Lund. Iliwekwa mnamo 2006-11-25.
- Masumian, Farnaz (1995). Maisha Baada ya Kifo: Utafiti kuhusu Maisha ya Baada ya Kifo katika Dini za Dunia. Oxford: Oneworld Publications. ISBN 1-8516-8074-8.
- McMullen, Michael D. (2000). Wabahá'í: Ujenzi wa Kitambulisho cha Kidini Duniani. Atlanta, Georgia: Rutgers University Press. ISBN 0-8135-2836-4.
- Meyjes, Gregory Paul (2006). "Lugha na mpangilio wa dunia katika mitazamo ya Baha'i". Katika Omoniyi, Tope; Fishman, Joshua A. (whr.). Uchunguzi katika Sosholojia ya Lugha na Dini. John Benjamins Publishing Co. ku. 26–41. ISBN 9-0272-2710-1.
- Momen, Moojan (1 Desemba 2012). Dini ya Baha'i: Mwongozo wa Mwanzoni (kwa Kiingereza). Simon and Schuster. ISBN 978-1-7807-4131-4.
- Smith, Peter (2000). Ensaiklopidia Fupi ya Dini ya Baháʼí. Oxford, Uingereza: Oneworld Press. ISBN 1-8516-8184-1.
- Smith, Peter (2008). Utangulizi wa Dini ya Baha'i. Cambridge: Cambridge University Press. ISBN 978-0-5218-6251-6.
- Stockman, Robert (2000). "Dini ya Baha'i". Katika Beversluis, Joel (mhr.). Kitabu Chanzo cha Dini za Dunia. New World Library. ISBN 1-5773-1121-3.
Usomaji zaidi
[hariri | hariri chanzo]- Vyanzo vya Kwanza
- Hyde Paine, Mabel (mhariri) (2006). Sanaa ya Kiungu ya Kuishi, na The Báb, Bahá'u'lláh, na Abdu'l-Bahá,. Bahá’í Publishing Wilmette, Illinois.
- Vyanzo vya Sekondari
- Schaefer, Udo (2007). Baháʼí Ethics in Light of Scripture, Volume 1 - Doctrinal Fundamentals. Oxford, Uingereza: George Ronald. ISBN 978-0-8539-8505-1.
- Schaefer, Udo (2009). Baháʼí Ethics in Light of Scripture, Volume 2 - Virtues and Divine Commandments. Oxford, Uingereza: George Ronald. ISBN 978-0-8539-8518-1.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- Bahai.org: Imani za Wabaháʼí
- Mkusanyo wa maandiko ya Wabaháʼí kuhusu mada mbalimbali
- The Loom of Reality, mkusanyo wa kimada wa nukuu kutoka Maandiko ya Wabaháʼí na zaidi