Nzi (kundinyota)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Nyota za kundinyota Nzi (Musca) katika sehemu yao ya angani

Nzi (kwa Kilatini na Kiingereza Musca) [1] ni jina la kundinyota kwenye nusutufe ya kusini ya dunia yetu.

Mahali pake[hariri | hariri chanzo]

Nzi iko jirani na kundinyota mashuhuri ya Salibu (Crux) iliyopo upande wa kaskazini, Mkuku (en:Carina) upande wa magharibi, Kinyonga (Chamaeleon) upande wa kusini, Ndege wa Peponi (Apus) na Bikari (Circinus) upande wa kaskazini-mashariki.

Jina[hariri | hariri chanzo]

Nzi ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa tangu mabaharia Wazungu kuzunguka Dunia yote katika karne ya 16 na kuona mara ya kwanza nyota za kusini. Haikujulikani kwa Wagiriki wa Kale au Waarabu waliojifunza kutoka kwao. Kundinyota hii ilielezwa mara ya kwanza na mabaharia Waholanzi Pieter Dirkszoon Keyser na Frederick de Houtman katika safari yao ya kuelekea Indonesia zikaonyeshwa mara ya kwanza mwaka 1598 katika globu ya nyota ya Petrus Plancius.

Keyser alitumia jina la Kiholanzi De Vlieghe (Nzi) lililotajwa baadaye kwa jina la Kilatini "Musca“. Baadaye ilipokelewa katika "Uranometria" ya Johann Bayer aliyetumia njia ya "Apis" (nyuki) na hivyo kuna vitabu vya zamani vinavyotumia jina Apis lakini baadaye "Musca" ilirudishwa.

Leo Musca ipo pia kati ya kundinyota 88 zinazoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [2] Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Mus'.[3]

Nyota[hariri | hariri chanzo]

Nyota angavu zaidi ni α Alfa Muscae yenye mwangaza unaoonekana wa 2.7 mag ikiwa umbali wa Dunia wa miakanuru 310[4] Ni rahisi kuiona maana ni nyota angavu jirani na Salibu kwa kufuata mstari wa urefu wa Salibu kuelekea kusini.

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Musca" katika lugha ya Kilatini ni "Muscae" na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Muscae, nk.
  2. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  3. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  4. Alphamus (Alpha Muscae), tovuti ya Prof. Jim Kaler, university of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]