Kishoroba cha Caprivi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kishoroba cha Caprivi ni kanda nyembamba ya eneo la Namibia inayoelekea mashariki kwenye pembe la kaskazini-mashariki kabisa ya nchi Namibia kati ya Botswana upande wa kusini na Angola pamoja na Zambia upande wa kaskazini. Kishoroba hicho kina urefu wa km 450, upana ni mara nyingi km 30 pekee.

Utawala[hariri | hariri chanzo]

Kiutawala kishoroba imegawanyika kati ya mikoa ya Caprivi and Okavango ya Jamhuri ya Namibia. Mji mkubwa ni Katima Mulilo ambao ni makao makuu ya mkoa wa Caprivi.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Jina la Caprivi limetokana na Chansella wa Ujerumani Leo von Caprivi aliyekuwa mkuu wa serikali ya Dola la Ujerumani wakati wa Mkataba wa Ujerumani na Uingereza wa 1890 unaoitwa "Mkataba wa Helgoland-Zanzibar". Ilikubaliwa ya kwamba Ujerumani inapata kishoroba cha nchi hadi mto Zambezi chenye upana "usiopungua maili 20".

Wakati ule Ujerumani ulitaka njia ya mawasiliano kati ya Namibia na mto Zambezi. Ilidhaniwa ya kwamba kuna uwezekano wa kutumia mto Zambezi kwa ajili ya usafiri na kupata njia ya maji kati ya Namibia na Bahari Hindi. Dhana hiyo ilikuwa kosa na kwa muda mrefu eneo la Caprivi lilikuwa na mawasiliano tu kupitia Zambia. Siku hizi kuna barabara ya lami hadi Katima Mulilo.

Miaka mingi wa vita ya kupigania uhuru wa Namibia na baadaye vita katika Angola eneo la kishoroba lilikuwa eneo lililofungwa kwa mawasiliano yasiyo ya kijeshi. Tangu mwisho wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Angola na kujengwa kwa barabara watu wa Caprivi wanaweza kusafiri kwa urahisi na wageni wanaweza kufika bila matatizo.

Tangu 1994 kuna "Harakati ya Ukombozi wa Caprivi", kundi kati ya Walozi wa Caprivi wanaopendelea umoja na Walozi wenzao huko Zambia wakitafuta hali ya kujitawala kwa eneo lao. Mwaka 1999 ilitokea ghasia katika mashariki ya Caprivi na mapigano kati ya wanamgambo Walozi na jeshi la serikali.