Kampeni za Kivita katika Afrika ya Mashariki (Vita ya Kwanza ya Dunia)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Ramani ya vita ya Afrika ya Mashariki mwaka 1915 (kutoka New York Times)
Historia ya Tanzania
Coat of Arms of Tanzania
This article is part of a series
Uendo
Historia ya Zanzibar
Afrika Mashariki 1800-1845
Ukoloni
Afrika ya Mashariki ya Kijerumani
Mkataba wa Zanzibar-Helgoland
Mkwawa
Vita vya Maji Maji
Vita vikuu vya kwanza Afrika Mashariki
Tanganyika
Mapambano ya uhuru Tanganyika
Uhuru
Uhuru wa Tanganyika
Mapinduzi ya Zanzibar
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
Julius Nyerere
Ujamaa
Tamko la Arusha
Vita vya Kagera
Ali Hassan Mwinyi
Benjamin Mkapa
Jakaya Kikwete
John Magufuli
Samia Suluhu Hassan

Tanzania Portal

Kampeni za Afrika ya Mashariki zilikuwa mfululizo wa mapigano ya kivita yaliyotokea Afrika ya Mashariki ya Kijerumani (Tanganyika, Rwanda na Burundi ya leo) na makoloni jirani ya Msumbiji, Rhodesia ya Kaskazini (Zambia), Afrika ya Mashariki ya Kiingereza (Kenya), Uganda, na Kongo ya Kibelgiji. Kampeni hizi zilianza mwezi wa Agosti 1914 zikaisha rasmi mnamo mwezi wa Novemba katika mwaka wa 1918.[1]

Wajerumani na mataifa ya ushirikiano

Wapiganaji katika vita hii walikuwa Schutztruppe (jeshi la kikoloni la Kijerumani) lililofanywa hasa na askari Waafrika waliosimamiwa na maafisa Wajerumani pamoja na walowezi Wajerumani na wanamaji wa manowari za Kijerumani waliokaa Afrika ya Mashariki wakati wa mwanzo wa vita 1914.

Dhidi yao walisimama jeshi dogo la kikoloni la Kiingereza katika Kenya na Rhodesia, halafu vikosi vya jeshi la kikoloni la Uhindi ya Kiingereza na vikosi kutoka Afrika Kusini na Afrika ya Magharibi. Pia walishiriki vikosi vya Force Publique ya Kibelgiji kutoka Kongo. Tangu mwaka 1916 jeshi la kikoloni la Ureno katika Msumbiji liliingia upande wa Uingereza.

Mikakati ya jeshi la kikoloni la Kijerumani lililoongozwa na Luteni Koloneli (baadaye Meja Jenerali) Paul Emil von Lettow-Vorbeck ililenga kuwalazimisha wapinzani hasa Waingereza kutumia wanajeshi wengi iwezekanavyo katika Afrika kwa shabaha ya kuwazuia wasipatikane kwenye vita ya Ulaya.

Mikakati yake ilifaulu kiasi cha kwamba Waingereza walipaswa kuleta vikosi vikubwa kutoka Uhindi ya Kiingereza na Afrika Kusini kupigania kampeni ya Afrika ya Mashariki, ingawa haikuwa na umuhimu wowote kwa mwendo wa vita Ulaya. [2][3]

Awamu ya kwanza: 1914-1915

Katika awamu ya kwanza ya vita vikosi vya Schutztruppe vilishambulia reli ya Uganda na vituo vya mpakani na Kenya. Waingereza walijibu kwa kukusanya walowezi wao katika Kenya bila kufaulu kuwazuia Wajerumani walioteka mji wa Taveta. Hiyvo Waingereza walichukua askari 12,000 Wahindi na 2 Novemba 1914 walishambulia Tanga. Lakini askari Waafrika wa jeshi la Kijerumani waliwashinda Tanga na baadaye pia Longido karibu na mlima Kilimanjaro, wengine huko Yasini.

Mapigano ya Tanga

Hapo Waingereza waliamua kuchukua wanajeshi Wazungu kutoka Afrika Kusini chini ya amri wa jenerali Jan Smuts waliofika Kenya hadi mwisho wa 1915. Wakati huohuo Wabelgiji walipanga pamoja na Uingereza kupeleka vikosi vya jeshi lake la Force Publique katika Kongo mpakani wa magharibi.

Manowari SMS Königsberg ilikuwa Dar es Salaam wakati wa Julai 1914 ikaondoka bandarini na kushambulia meli za Kiingereza kwenye Bahari Hindi. Waingereza walijaribu kuizuia walituma manowari tatu HMS Astraea, HMS Pegasus na HMS Hyacinth kutoka Afrika Kusini kuelekea Dar es Salaam. SMS Königsberg ilianza kukosa makaa kwa injini yake ikarudi Afrika ya Mashariki; ilipopita Zanzibar ikakuta HMS Pegasus bandarini na kuizamisha. Königsberg ikakimbia ikajificha katika mdomo wa mto Rufiji. Waingereza walikusanya manowari kadhaa mbele ya mto Rufiji; manowari zao zilishindwa kuingia ndani ya mdomo wa mto lakini walivamia kisiwa cha Mafia na kuanzisha kiwanja cha ndege; hatimaye walifaulu kupiga Königsberg mara kadhaa na kusababisha uharibifu mkali hadi nahodha Mjerumani aliamua kuzamisha manowari yake mwenyewe kwenye tarehe 11 Juni 1915. Mabaharia Wajerumani walitoa mizinga yao na kuipeleka kwenye nchi kavu wakajiunga na Schutztruppe.

Awamu ya pili: shambulio dhidi ya Tanganyika

Januari 1916 jeshi hili lilishambulia. Jeshi la Kijerumani lilikuwa ndogo likafuata mikakati ya kuwachelewesha maadui na kuwashambulia walipokuwa wadhaifu au walipofanya makosa.

  • Vikosi kutoka Uhindi, Afrika Kusini na Uingereza vilivamia Tanganyika kutoka upande wa Kenya
  • Wanajeshi 5,000 Waingereza na Waafrika Kusini walivamia kusini magharibi ya Tanganyika kutoka Nyassaland (Malawi) na Rhodesia (Zambia)
  • Wabelgiji waliingia Rwanda na Burundi kutoka Kongo wakafuata njia ya reli kuelekea Tabora
  • Wareno walivamia pembetatu ya Kionga (nchi ng'ambo ya mto Rufiji) na nyanda za juu za Umakonde. Lakini walishindwa hapa wakapaswa kurudi Msumbiji

Hadi Agosti 1916 mataifa ya ushirikiano yalishika miji muhimu ya Tanganyika isipokuwa Daressalaam. Moshi iltekwa mwezi wa Machi. Reli ya Kati ya Tanganyika kuanzia Tabora, Dodoma hadi Morogoro ilikuwa mkononi mwao. Walisita kuvamia Daressalaam kwa sababu waliogopa mapigano makali lakini Lettow-Vorbeck aliwahi kuondoa askari wake tayari kwa sababu hakutafuta mapigano makubwa dhidi ya maadui mwenye nguvu zaidi. Alipeleka jeshi lake katika eneo upande wa kusini wa mstari Daressalaam-Morogoro-Iringa pasipo na njia nzuri akitegemea Waingereza wasingeweza kutumia usafiri kwa malori na reli.

Hadi hapa maendeleo ya vikosi vya maungano yalikuwa na matatizo mengi. Walitegemea hasa askari Wazungu na Wahindi waliozoea kusafiri na mizigo mikubwa ya vyakula, nguo na hema na kwa hiyo walihitaji wapagazi wengi. Hivyo maendeleo yao yalikuwa polepole wakahitaji chakula kingi kulisha askari pamoja na wapagazi. Askari pamoja na sehemu ya wapagazi walikuwa wageni ambao hawakuzoea vema hali ya hewa na magonjwa hivyo walisumbuliwa kiafya. Kwa mfano kikosi cha 9th South African Infantry ilifika mwezi wa Februari 1916 chenye askari Wazungu 1,135 na hadi Oktoba ni 116 pekee waliobaki tayari kwa vita, ingawa kikosi hiki hakikuona mapigano na idadi yao ilipungua kutokana na magonjwa pekee.[4]

Kinyume chake Lettow Vorbeck aliwategemea hasa askari Waafrika waliokuwa na mahitaji madogo waliojua nchi na kuzoea magonjwa ya mazingira. Waingereza walitumia askari Waafrika hasa kwa kulinda reli ya Uganda kwa sababu mwanzoni walikosa imani katika uwezo wao.

Awamu ya tatu: vita ya msituni

Tangu mwaka 1917 Waingereza walipunguza idadi ya Wazungu na Wahindi badala yake waliunda vikosi vipya vya Waafrika vya King's African Rifles waliokuwa na uwezo wa kushindana na Waafrika wa Lettow Vorbeck.

Walifaulu kusukuma jeshi la Schutztruppe kusini zaidi. Katika Oktoba 1917 waliwalazimisha Wajerumani kusimama kwenye mapigano ya Mahiwa ambako Lettow Vorbeck aliwashinda lakini alipoteza askari mamia. Pia akiba yake ya risasi ilielekea kwisha. Kikosi kikubwa cha askari 1000 chini ya kapteni Tafel walilazimishwa kusalimisha amri baada ya kuishiwa chakula na risasi kabisa. Hata kama hakushindwa, Lettow Vorbeck hakuweza kuendelea vile akaamua kuondoka katika Tanganyika na kwenda Msumbiji alipotegemea Wareno kuwa adui mdhaifu.

Awamu ya nne: Msumbiji na mwisho

Mwisho wa Novemba 1917 Lettow aliwaacha wajeruhiwa na sehemu kubwa ya Wajerumani raia walioongozana naye nyuma akavuka mto Rovuma na askari 280 Wajerumani na Waafrika 1600.

Katika Msumbiji aliweza kuteka kambi ya kijeshi ya Wareno alipokamata bunduki na risasi pamoja na chakula. Waingereza walijaribu kumfuata laini walishindwa kumkuta katika Msumbiji. Katika miezi ya 1918 iliyofuata Lettow Vorbeck alizunguka katika Msumbiji ya kaskazini, mara nyingi kwa umbali wa matembezi ya siku 2 au tatu na Waingereza na Wareno waliomtafuta bila kumpata. Alivamia vituo mbalimbali vya Wareno na kupata risasi na vyakula mara kwa mara.

Jeshi la Kijerumani ilivyosalimisha amri 1918 (uchoraji wa siku zile)

Katika Septemba 1918 alipata habari ya kwamba Waingereza walikuwa nyuma yake kwa jeshi kubwa. Hapa aliamua kurudi Tanganyika na kuelekea Rhodesia kwa sababu habari zilimfikia ya kwamba Waingereza hawakuwa tena na jeshi huko. Tarehe 28 Septemba alivuka tena mto Rovuma akaendelea katika sehemu za kusini kupitia Songea na Mbozi. Mwezi wa Novemba aliingia Rhodesia ya Kaskazini (Zambia). Tarehe 13 Novemba kikosi chake kiliteka mji wa Kasama ambako Waingereza wachache walikimbia walipomwona. Siku iliyofuata afisa Mwingereza alikaribia kambi yake na kumletea habari ya kwamba vita ilikwisha tayari na Ujerumani iliwahi kusimamisha mapigano yote tangu 11 Novemba 1918. Lettow alipatana na Waingereza kuongoza askari hadi mji wa Abercorn (leo Mbala, Zambia) aliposalimisha amri tarehe 23 Novemba 1918.

Askari na maafisa wa Schutztruppe waliongozwa na Waingereza kutoka hapa hadi Bismarckburg (Kasanga) walipowekwa kwenye meli hadi Kigoma. Kutoka hapa walisafirishwa kwa reli ya kati hadi Tabora ambako askari Waafrika wa Schutztruppe waliweza kurudi makwao. Wajerumani waliendelea hadi Dar es Salaam. Baada kusubiri wiki kadhaa waliondoka kwenye Januari 1919 kwa meli hadi Ujerumani.[5]

Tazama pia

Tanbihi

  1. Holmes 2001, p. 361.
  2. Holmes 2001, p. 359.
  3. Strachan 2003, p. 642.
  4. Falls, Cyril. The Great War. New York: Capricorn Books. 1961, p. 253
  5. Schnee, Heinrich: Deutsch-Ostafrika im Weltkriege, Leipzig, 1919, uk. 406

Marejeo

  • Pugu Hadi Peramiho - kimehaririwa na P. Gerold Rupper, OSB, BPNP, Peramiho 1988, ISBN 9967 67 031 1
  • Abbott, Peter. Armies in East Africa 1914–1918. Osprey, 2002 ISBN 1-841-76489-2
  • Anderson, Ross. The Forgotten Front: The East African Campaign: 1914–1918. Tempus Publishing, Ltd. 2004 ISBN 0-752-42344-4
  • Crowson, Major Thomas A. When Elephants Clach: A Critical Analysis of Major General Paul Emil von lettow Vorbeck in the East African Theatre of the Great War
  • Farwell, Byron, The Great War in Africa, 1914–1918. New York: W.W. Norton & Company. 1989 ISBN 0-393-30564
  • Gardner, Brian. On to Kilimanjaro. Macrae Smith Company. 1963 ISBN 1-111-04620-4
  • Garfield, Brian. The Meinertzhagen Mystery. Washington, DC: Potomac Books. 2007 ISBN 1597970417
  • Hodges, Geoffrey, Editor. The Carrier Corps: The Story of the Military Labor Forces in the Conquest of German East Africa, 1914–1919. 2nd revised edition. Nairobi: Nairobi University Press. 2000
  • Holmes, Richard. The Oxford Campanion to Military History. Oxford University Press. 2001. ISBN 978-0198606963
  • Hoyt, Edwin P. The Germans who never lost. New York: Funk & Wagnalls. 1968, and London: Leslie Frewin. 1969. ISBN 0090964004. Note: This book is a study of Captain Max Looff and his crew of the light cruiser Königsberg
  • Hoyt, Edwin P. Guerilla: Colonel von Lettow-Vorbeck and Germany's East African Empire. New York: MacMillan Publishing Co., Inc. 1981; and London: Collier MacMillan Publishers. 1981 ISBN 0-02-555210-4
  • Miller, Charles. Battle for the Bundu: The First World War in East Africa. New York: MacMillan Publishing Co., Inc. 1974 ISBN 0-025-84930-1
  • Mosley, Leonard. Duel for Kilimanjaro. An Account of the East African Campaign 1914–1918, Ballantine Books, New York 1964
  • Paice, Edward. Tip and Run: The Untold Tragedy of the Great War in Africa, Weidenfeld & Nicolson. 2007 ISBN 0-297-84709-0
  • Rutherford, A. (ed.). Kaputala: The Diary of Arthur Beagle & The East Africa Campaign 1916–1918. Hand Over Fist Press (for Introduction [1] Archived 25 Januari 2021 at the Wayback Machine.), 2001 ISBN 0-9540517-0-X
  • Sibley, J.R. Tanganyikan Guerrilla. New York: Ballantine Books. 1973 ISBN 0345098013
  • Stapleton, Tim. The Rhodesia Native Regiment and the East Africa Campaign of the First World War. Wilfrid Laurier University Press. 2005. ISBN 9780889204980
  • Strachan, Hew. The First World War in Africa. Oxford: Oxford University Press. 2004 ISBN 0-199-25728-0
  • Strachan, Hew. The First World War, To Arms. Oxford addition. 2003. ISBN 978-0199261918
  • Stevenson, William. The Ghosts of Africa. New York: Ballantine Books. 1981 ISBN 0-345-29793-8 (fictionalized account)
  • Young, F. Brett. "Marching on Tanga." New York: E.F. Dutton & Co. 1917.(Medical officer's account of campaigning with General Smuts.)