Gideon Byamugisha

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Gideon Byamugisha ni kasisi Mwanglikana wa Uganda na mchungaji wa kwanza Mwafrika aliyetangaza wazi ya kwamba ameambukizwa UKIMWI.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa Buranga Ndorwa, Wilaya ya Kabale, Uganda wa Magharibi tarehe 29 Agosti 1959 akasomea ualimu kwenye Chuo Kikuu cha Makerere akamaliza kwa digrii mwaka 1985.

Akaendelea kusoma digrii ya theolojia huko Nairobi akapokelewa katika utumishi wa Kanisa la Kianglikana Uganda mwaka 1991. Mwaka uleule mke wake alikufa kutokana na UKIMWI.

1992 alipokea baraka ngazi ya ukasisi akapewa jukumu la kufundisha chuo cha theolojia Mukono (sasa: Chuo Kikuu cha Kikristo cha Uganda). Wakati ule alifuata ushauri kutafuta upimaji wa damu yake ahakikishe hana UKIMWI. Alipopimwa akaonekana kuwa na viini vya HIV vilevile. Aliambiwa matokeo dakika chache tu kabla ya kuwa na somo chuoni. Aliamua kuwaambia wasikilizaji wake wakiwa na walimu wenzake ya kuwa amepatikana na HIV.

Tangazo hili lilipokelewa kwa mshangao kwani katika utamaduni wa kiafrika na zaidi katika utamaduni wa kidini wa Afrika haikuwahi kutokea ya kwamba kiongozi wa kidini anasema waziwazi kuwa ameambukizwa UKIMWI. Kinyume chake mara nyingi wahubiri walitumia mfano wa UKIMWI kuonyesha ya kuwa ni adhabu kutoka Mungu na dalili ya dhambi.

Gideoni Byamugisha aliitwa na kanisa lake kuanzia mwaka 1993 kusaidia katika mradi wa UKIMWI wa kanisa. 1995 - 2002 aliongoza idara wa HIV/UKIMWI ya dayosisi ya Kianglikana ya Namirembe.

Mwaka 1995 alifunga ndoa mara ya pili akimwoa Pamela aliyekuwa mjane wakati ule kutokana na UKIMWI akipatikana mwenyewe na viini vya HIV. Wanalea watoto wao kutoka ndoa zote mbili za awali pia wakamzaa mtoto wa pamoja asiye na HIV kutokana na tibu la madawa ya ARV.

Siku hizi (2005) Byamugisha anafanya kazi na shirika la Word Vision International pia pamoja na kasisi Jape Heath kutoka Afrika Kusini ameunda "Umoja wa viongozi wa kidini wa Afrika wanaoishi na UKIMWI" (ANERELA African Network of Religious Leaders living with HIV/AIDS).

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]