Francisco Franco

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Francisco Franco Bahamonde (4 Desemba 1892 - 20 Novemba 1975) alikuwa jenerali wa Hispania ambaye aliongoza vikosi vya Wazalendo kupindua Jamhuri ya Pili ya Hispania wakati wa Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania na baadaye akatawala nchi kutoka mwaka 1939 hadi 1975 kama dikteta, akitumia cheo cha Caudillo (kiongozi). Kipindi hicho katika historia ya Hispania, kutoka ushindi hadi kifo cha Franco, inajulikana kama udikteta wa kifashisti.

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Alizaliwa huko Ferrol, Hispania katika familia ya wanajeshi. Franco alijiunga na Jeshi la Hispania kama mwanafunzi katika Chuo cha Kijeshi cha Toledo kutoka mwaka 1907 hadi 1910. Aliendelea kuhudumia katika jeshi kwenye koloni la Moroko alipopanda ngazi hadi kuwa jenerali kwenye mwaka 1926.

Miaka miwili baadaye Franco alikuwa mkuu wa Chuo Kikuu cha Kijeshi huko Zaragoza. Akiwa na imani katika ufalme, alisikitika kutangazwa kwa jamhuri na kuondoka kwa mfalme Alfonso XIII mnamo 1931. Hata hivyo, aliendelea kuhudumia jeshi la jamhuri.

Uchaguzi wa mwaka 1933 ulileta ushindi wa vyama vya kulia. Katika jimbo la Asturias wafanyakazi wasoshalisti na waanakisti walitangaza mapinduzi wakashika silaha. Franco alipewa na serikali kazi ya kukandamiza uasi huo aliyotekeleza kwa kuchukua vikosi kutoka jeshi katika Moroko. Kwa muda mfupi Franco alipandishwa ngazi kuwa mkuu wa jeshi lote.

Uchaguzi wa mwaka 1936 ulileta tena ushindi wa vyama vya kushoto (Wasoshalisti). Franco alihamishwa kwenye Visiwa vya Kanari. Katika mwezi wa Julai Franco alijiunga na kundi la maafisa wa jeshi waliopanga uasi wa kijeshi. Alipewa amri juu ya jeshi la Afrika, yaani vikosi vya Hispania katika Moroko. Kwa msaada wa Ujerumani na Italia aliweza kuhamisha wanajeshi kutoka Moroko hadi Hispania yenyewe.

Vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Hispania ilianza na Franco haraka alipanda ngazi upande wa waasi hadi kutangazwa mkuu wa jeshi upande wa wazalendo na pia mkuu wa nchi.

Mwaka 1937 aliunganisha vyama vyote vya kulia, yaani wafuasi wa mfalme, Wakatoliki na wafashisti, katika chama kimoja. Baada ya mapigano ya miaka mitatu, na kwa msaada wa silaha na wanajeshi kutoka Ujerumani na Italia, jeshi la wazalendo lilishinda serikali ya jamhuri na vyama vya kushoto.

Sasa kilianza kipindi cha udikteta wa Franco, mwanzoni kwa ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa. Matumizi yake ya udikteta yalisababisha vifo kati ya 30,000 na 50,000, wengi kwa kuua wapinzani waliojulikana wa kuwapiga kwa bunduki[6][7]. Baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, Franco alitawala kwa mamlaka kushinda kiongozi yeyote wa Hispania kabla au tangu hapo. Mwanzoni alitunga sheria zote peke yake, bila bunge wala kuuliza baraza la mawaziri. Baadaye alilegeza ukali wa udikteta lakini aliendelea kuwa mkuu wa dola hadi kifo chake na pia waziri mkuu hadi mwaka 1973. Mwaka 1947 alitangaza Hispania kuwa ufalme tena lakini hakumteua mfalme.

Katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia alikataa kuingia upande wa Hitler akaendelea na msimamo wa kutojiunga na upande wowote. Aliruhusu Wahispania kujitolea kupigania upande wa Ujerumani katika vita dhidi ya Umoja wa Kisovyeti. Alikataa pia kujiunga na siasa ya Hitler ya kutesa Wayahudi; aliruhusu maelfu ya wakimbizi Wayahudi kupitia Hispania ili kuendelea kuhamia nchi nyingine.

Wakati wa kuanza kwa Vita Baridi baina ya nchi za Kikomunisti na nchi zilizoshikamana na Marekani, Franco alichukua upande wa Marekani akatuma wanajeshi wachache katika vita ya Korea. Alifaulu kujenga uchumi wa Hispania na kuongoza nchi kutoka uchumi wa kilimo kuingia katika uchumi wa viwanda.

Tabia ya kidikteta ya utawala wake iliendelea kupungua kadri aliyozeeka. Mnamo 1973 Franco alijiuzulu kama waziri mkuu kwa sababu ya uzee na ugonjwa, lakini alibaki madarakani kama mkuu wa jeshi na mkuu wa dola. Franco alifariki mnamo 1975, akiwa na umri wa miaka 82.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Maestre, F. E., Casanova, J., Mir, C., & Gómez, F. M. (2004). Morir, matar, sobrevivir: La violencia en la dictadura de Franco. Grupo Planeta (GBS). p.8
  2. Fontana, J. (Ed.). (1986). España bajo el franquismo: coloquio celebrado en la universidad de Valencia, noviembre de 1984. Universidad; Crítica: Departamento de Historia Contemporánea. p.22
  3. Thomas, p. 900-901
  4. Preston, Paul. The Spanish Civil War. Reaction, revolution & revenge. Harper Perennial. 2006. London. p.202
  5. Beevor, Antony. The Battle for Spain; The Spanish Civil War 1936–1939. Penguin Books. 2006. London. p.94
  6. [1][2][3][4][5]
  7. Richards, Michael (1998) A Time of Silence: Civil War and the Culture of Repression in Franco's Spain, 1936–1945, Cambridge University Press. ISBN 0521594014. p. 11.