Azimio la Kimataifa juu ya Haki za Binadamu : Tofauti kati ya masahihisho

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Content deleted Content added
d roboti Nyongeza: zh-yue:世界人權宣言
d roboti Nyongeza: fo:Mannarættindayvirlýsing
Mstari 178: Mstari 178:
[[fa:اعلامیه جهانی حقوق بشر]]
[[fa:اعلامیه جهانی حقوق بشر]]
[[fi:Ihmisoikeuksien yleismaailmallinen julistus]]
[[fi:Ihmisoikeuksien yleismaailmallinen julistus]]
[[fo:Mannarættindayvirlýsing]]
[[fr:Déclaration universelle des droits de l'homme]]
[[fr:Déclaration universelle des droits de l'homme]]
[[fur:Declarazion universâl dai dirits dal om]]
[[fur:Declarazion universâl dai dirits dal om]]

Pitio la 21:42, 30 Desemba 2009

Eleanor Roosevelt na Tangazo kilimwengu la haki za binadamu (1949)

Tangazo la kilimwengu la haki za binadamu (pia: Taarifa ya ulimwengu juu ya haki za binadamu; Tamko la kimataifa kuhusu haki za binadamu; kwa Kiingereza: Universal Declaration of Human Rights) ni tamko la Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya haki za binadamu lililotolewa tarehe 10 Desemba 1948. Ilikuwa kati ya maazimio ya kwanza kabisa ya UM.

Msingi wa haki hizi uko katika kifungo cha kwanza kinachosema "Watu wote wamezaliwa huru, wakiwa na hadhi na haki sawa. Wamejaliwa akili na dhamiri na kupaswa kutendeana kwa roho ya kidugu".

Haki zinaorodheshwa katika vifungo 30 vinavyoeleza haki za msingi ambazo kila mtu anastahili kuwa nazo "bila kubaguana kwa rangi, taifa, jinsia, dini, siasa, fikara, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine yo yote".

Haki zilizomo katika tangazo hili si sheria ya kimataifa moja kwa moja jinsi zilivyo, lakini zimekubaliwa na kila taifa lililojiunga na UM. Sehemu kubwa ya vipengele vyake imeingia katika mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiraia na kisiasa ya 1966 na mapatano ya kimataifa juu ya haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ya 1976 na zimekuwa sehemu ya sheria ya kimataifa kwa njia hiyo.

Mawazo ya msingi

Mawazo ya msingi ya tangazo la haki za binadamu ni pamoja na:

  • kila mtu ana haki ya maisha, uhuru na usalama.
  • kila mtu ana haki ya elimu.
  • kila mtu ana haki ya kazi.
  • kila mtu ana haki ya kufuata utamaduni wake.
  • kila mtu ana haki ya kutotendewa kinyama au kikatili.
  • kila mtu ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake au kuchagua dini yake.

Historia

Tangazo la UM si mara ya kwanza katika historia kuorodhesha haki za binadamu. Mfano unaojulikana sana ni Tangazo la Haki za Kibinadamu na Kiraia lililotolewa na bunge la Ufaransa tarehe 26 Agosti 1789 wakati wa Mapinduzi ya Kifaransa.

Tamko la bunge la Ufaransa ulifuata katiba ya Marekani (4 Julai 1776) iliyotaja pia haki za msingi. Matangazo haya yote mawili yanasimama kwenye msingi wa juhudi za falsafa ya zama za mwangaza katika karne ya 18, lakini mizizi yake katika ustaarabu wa Ulaya unategemea hadhi ya mtu kama sura na mfano wa Mungu katika imani ya dini ya Uyahudi na Ukristo.

Kanuni za Tangazo Kilimwengu la Haki za Binadamu

Kifungu cha 1.
Watu wote wamezaliwa huru, hadhi na haki zao ni sawa. Wote wamejaliwa akili na dhamiri, hivyo yapasa watendeane kindugu.

Kifungu cha 2.
Kila mtu anastahili kuwa na haki zote na uhuru wote ambao umeelezwa katika Taarifa hii bila ubaguzi wo wote. Yaani bila kubaguana kwa rangi, taifa, wanaume kwa wanawake, dini, siasa, fikara, asili ya taifa la mtu, mali, kwa kizazi au kwa hali nyingine yo yote.

Juu ya hayo usifanye ubaguzi kwa kutegemea siasa, utawala au kwa kutegemea uhusiano wa nchi fulani na mataifa mengine au nchi ya asili ya mtu, haidhuru nchi hiyo iwe inayojitawala, ya udhamini, isiyojitawala au inayotawaliwa na nchi nyingine kwa hali ya namna yo yote.

Kifungu cha 3.
Kila mtu ana haki ya kuishi, haki ya uhuru, na haki ya kulindwa nafsi yake.

Kifungu cha 4.
Mtu ye yote asifanywe mtumwa au mtwana; utumwa na biashara yake ni marufuku kwa kila hali.

Kifungu cha 5.
Mtu ye yote asiteswe, asiadhibiwe, asidharauliwe au kutendewa kinyama au kikatili.

Kifungu cha 6.
Mbele ya sheria kila mtu ana haki ya kutambulika kama mtu.

Kifungu cha 7.
Mbele ya sheria watu wote ni sawa na wanastahili haki sawa za kulindwa. Wote wana haki sawa ya kulindwa kutokana na ubaguzi wo wote unaoweza kuvunja Taarifa hii na mambo yo yote yanayoweza kuleta ubaguzi kama huo.

Kifungu cha 8.
Kila mtu ana haki ya kutetewa na baraza la hukumu kwa makosa ya kuvunjiwa haki zake za asili anazostahili kwa mujibu wa kanuni na sheria.

Kifungu cha 9.
Mtu ye yote asikamatwe, asifungiwe au kuhamishwa kutoka nchi yake bila sheria.

Kifungu cha 10
Kila mtu ana haki kamili ya kuhukumiwa vyema hadharani na baraza la hukumu lililo huru na lisilo na upendeleo katika kutoa uamuzi wa haki zake na wajibu wake na wa makosa yo yote yanayomhusu.

Kifungu cha 11.
1. Kila mtu anaeshtakiwa kwa kosa la kuvunja sheria ana haki ya kuangaliwa kama si mkosefu mpaka imethibitishwe kwa sheria, kwa kuhukumiwa hadharani, kwamba ana hatia.
2. Mtu ye yote asitiwe hatiani kwa tendo lo lote au jambo lo lote ambalo halikupinga sheria ya taifa au ya kati ya mataifa wakati alipolitenda. Wala asipewe adhabu kali zaidi kuliko ile iliyokuwamo katika sheria wakati alipofanya kosa.

Kifungu cha 12.
Kila mtu asiingiliwe bila sheria katika mambo yake ya faragha, ya jamaa yake, ya nyumbani mwake au ya barua zake. Wala asivunjiwe heshima na sifa yake. Kila mmoja ana haki ya kulindwa na sheria kutokana na pingamizi au mambo kama hayo.

Kifungu cha 13.
1. Kila mtu ana haki ya kwenda mahali anapotaka na kuishi katika kila nchi.
2. Kila mmoja ana haki ya kuhama kutoka nchi yo yote, hata nchi yake mwenyewe, na ana haki ya kurejea katika nchi yake.

Kifungu cha 14.
1. Kila mtu ana haki ya kukimbilia na kustarehe katika nchi nyingine kwa ajili ya kuepukana na udhalimu.
2. Haki hii haiwezi kuombwa kwa udhalimu ambao hautokani na makosa ya mambo ya siasa au na makosa ya maazimio na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Kifungu cha 15.
1. Kila mtu ana haki ya utaifa.
2. Mtu ye yote asinyang'anywe utaifa wake bila sheria wala asinyimwe haki ya kujibadili taifa lake kama akitaka.

Kifungu cha 16.
1. Watu wazima, wanaume kwa wanawake wana haki ya kuoana na kuunda jamaa bila kizuio cho chote kwa sababu ya rangi, taifa au dini. Wana haki sawa za ndoa wakati wa maisha yao ya ndoa na wakati wa kutenguka ndoa.
2. Ndoa inaweza kufungwa tu kwa hiari na mapatano kamili kati ya hao wanaotaka kuoana.
3. Jamaa ni kiungo cha asili cha jamii ya watu, na inastahili kulindwa na watu pamoja na Serikali.

Kifungu cha 17.
1. Kila mtu ana haki ya kuwa na mali yake binafsi au kwa kushirikiana na watu wengine.
2. Mtu asinyang'anywe mali yake bila sheria.

Kifungu cha 18.
Kila mtu ana haki ya uhuru wa mawazo, dhamira na dini; haki hii inahusu pia uhuru wa kubadili dini yake au imani, na uhuru wa kubainisha hadharani au faraghani-akiwa peke yake au na watu wengine-dini yake kwa kufundisha, kwa vitendo, kuabudu na kwa kuadhimisha.

Kifungu cha 19.
Kila mmoja ana haki ya uhuru wa kutoa na kueleza maoni yake; haki hii inahusu pia uhuru wa kushikilia maoni yake bila kuingiliwa kati, na uhuru wa kutafuta na kutoa habari na maoni kwa njia yo yote bila kujali mipaka.

Kifungu cha 20.
1. Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika mkutano na chama kwa hali ya amani.
2. Mtu ye yote asilazimishwe kuwa manachama wa chama fulani.

Kifungu cha 21.
1. Kila mmoja anayo haki ya kushiriki katika Serikali ya nchi yake yeye mwenyewe binafsi au kwa njia ya mjumbe aliemchagua kwa hiari yake.
2. Kila mmoja anayo haki sawa ya kufanya kazi katika Serikali; matakwa hayo huonyeshwa katika uchaguzi halisi unaofanywa muda baada ya muda ambao kila mtu hupiga kura na ambao hufanywa kwa kura ya siri na kila mtu kwa hiari yake.
3. Matakwa ya watu ndiyo yatakuwa msingi wa utawala wa serikali; hali hii itajidhihirisha kwenye chaguzi za haki kwa watu wote na ambazo zinafanyika kwa siri au namna nyingine ambayo itahakikisha uchagazi kuwa huru.

Kifungu cha 22.
Kila mtu, kama raia, anayo haki ya kutunzwa na anastahili kupata hali zinazotokana na uchumi, starehe na utamaduni-ambazo ni za lazima kwa hali bora na maendeleo ya nafsi yake- kwa njia ya juhudi ya taifa na ushirikiano kati ya mataifa na kwa mujibu wa utaratibu na utajiri wa kila nchi.

Kifungu cha 23.
1. Kila mtu ana haki ya kufanya kazi, ya kuchagua kazi aipendayo, ya kuchagua kazi yenye masharti mazuri na ana haki ya kulindwa asikose kazi.
2. Kila mtu ana haki ya kupata mshahara sawa na wengine wenye kazi ya namna moja bila ubaguzi.
3. Kila mfanya kazi anayo haki ya kupata mshahara wa kufaa na unaopendeza utakao mwezesha yeye mwenyewe pamoja na jamaa yake kuishi katika hali bora, na ahifadhiwe-ikiwa lazima- maisha yake kwa njia nyingine.
4. Kila mtu anayo haki ya kuunda au kujiunga na chama cho chote cha wafanya kazi kwa ajili ya kulinda haki zake za kazi.

Kifungu cha 24.
Kila mtu ana haki ya kupumzika na kufanya kazi kwa kiasi cha saa zinazostahili. Pia ana haki ya kupata likizo, kwa vipindi, na kupokea mshahara kama vile angekuwa kazini.

Kifungu cha 25.
1. Kila mtu anayo haki ya kupata hali bora ya maisha yeye mwenyewe pamoja na jamaa yake na kupata chakula, mavazi, nyumba, matibabu na hifadhi za lazima kwa maisha yake. Pia ana haki ya kutunzwa wakati wa kazi, wakati wa ugonjwa, wa kutojiweza, ujane, uzee au anapokosa ridhiki yake kwa kutoweza kujisaidia.
2. Akina mama na watoto wanastahili kutunzwa na kupewa msaada maalum. Watoto wote- wawe wamezaliwa katika hali ya ndoa ama hapana- lazima watunzwe vyema.

Kifungu cha 26.
1. Kila mtu ana haki ya kuelimishwa. Elimu yapasa itolewe bure hasa ile ya madarasa ya chini. Elimu ya masarasa ya chini ihudhuriwe kwa lazima. Elimu ya ufundi na ustadi iwe wazi kwa wote. Na elimu ya juu iwe wazi kwa wote kwa kutegemea sifa ya mtu.
2. Elimu itolewe kwa madhumuni ya kuendeleza barabara hali ya binadamu, na kwa shabaha ya kukuza haki za binadamu na uhuru wake wa asili. Elimu ni wajibu ikuze hali ya kueleana, kuvumiliana na ya urafiki kati ya mataifa na kati ya watu wa rangi na dini mbali-mbali.Kadhalika ni wajibu iendeleze shughuli za Umoja wa Mataifa za kudumisha amani.
3. Ni haki ya wazazi kuchagua aina ya elimu ya kufunzwa watoto wao.

Kifungu cha 27.
1. Kila mtu anayo haki ya kushiriki katika maisha ya utamaduni ya jamii yo yote, na ana haki ya kufurahia ustadi wa kazi na kushiriki katika maendeleo ya mambo ya sayansi na faida zinazotokana nayo.
2. Kila mtu ana haki ya kulindwa kwa kila hali kutokana na mambo ya sayansi aliyoandika, aliyochora au aliyogundua.

Kifungu cha 28.
Ni haki kila mtu alindwe na taratibu au kanuni za jamii na zinazohusu mataifa mbalimbali ambazo ndani yake uhuru na haki zilizoelezwa katika Taarifa hii zinaweza kuhifadhiwa barabara.

Kifungu cha 29.
1. Kila mtu ana wajibu kwa watu wa jamii yo yote ambao kati yao tu ndio yanaweza kupatikana maendeleo kamili ya hali bora ya maisha yake.
2. Katika kutumia haki na uhuru wake, kila mtu itambidi kufuata kanuni zile tu zilizowekwa na sheria kwa ajili ya kulinda heshima inayotakiwa juu ya haki na uhuru wa watu wengine, na kwa ajili ya kuhifadhi kanuni za haki, usalama na hali njema ya maisha katika jamii ya kidemokrasi.
3. Uhuru huu na haki hizi kamwe visitumiwe kinyume cha maazimio na kanuni za Umoja wa Mataifa.

Kifungu cha 30.
Hakuna maneno yo yote katika Taarifa hii yanayoweza kubashiriwa kwamba yanaruhusu nchi yo yote, kikundi cha watu au mtu fulani kufanya au kushughulika na jambo lo lote ambalo nia yake ni kuharibu uhuru haki zilizoelezwa humu.


Viungo vya Nje