Kalenda ya jua-mwezi
Kalenda ya jua-mwezi (kwa Kiingereza: lunisolar calendar) ni kalenda inayotumia awamu za Mwezi pamoja na mwaka wa jua. Kalenda ya Kiyahudi na ya Kichina ni kalenda za jua-mwezi zinazotumiwa leo.
Awamu za Mwezi
[hariri | hariri chanzo]Kalenda za aina hiyo huunganisha faida ya kufuata awamu za Mwezi na mwendo wa Jua. Awamu za Mwezi zinaonekana na watu wote - tofauti na miezi katika kalenda ya kawaida (ya Gregori) ambayo haina uhusiano na mwonekano wa Mwezi. Mwezi mpya au kuonekana kwa hilali ni njia nyepesi kwa watu wote kutambua mwanzo wa mwezi.
Kalenda za mwezi, zinazofuata idadi ya miezi halisi pekee kwa kuamulia kipindi cha mwaka, huwa na kasoro kwamba majira na sikukuu havina nafasi thabiti katika mwendo wa mwaka wa mwezi. Maana miezi (vipindi) 12 kutoka hilali hadi hilali ni siku 354 pekee, ilhali mwaka wa Jua huwa na siku 365 na karibu robo.
Hivyo sikukuu zinahamahama kila mwaka kulingana na majira; vilevile vipindi ambavyo ni muhimu kwa maisha ya jamii kama vile mavuno au kuandaa mashamba hufuata mwendo wa Jua lakini havilingani na kalenda ya mwezi. Kuunganisha awamu za mwezi na mwaka wa jua kunaruhusu kutunza miezi asilia na mwendo wa majira.
Miaka ya kawaida na miaka mirefu
[hariri | hariri chanzo]Kalenda ya jua-mwezi inapaswa kusawazisha tofauti baina ya mwaka wa jua na mwaka wa mwezi. Hii inatekelezwa kwa kuingiza miaka mirefu yenye mwezi wa 13 kila baada ya miaka ya kawaida kadhaa. Kwa mfano kalenda ya Kiyahudi huingiza miaka mirefu mara saba katika kipindi cha miaka 19. Kwa njia hiyo sikukuu ya mavuno inakaa katika majira yake, hata kama tarehe yake inacheza kidogo ikilinganishwa na kalenda ya jua.
Mifano
[hariri | hariri chanzo]Kalenda za Kiyahudi, Kijain, Kibuddha, Kihindu na Kikurdi na vile vile kalenda za kimapokeo za Burma, China, Japani, Tibeti, Vietnam, Mongolia na Korea, pamoja na kalenda za kihistoria za Ugiriki ya Kale na Babeli zote ni za jua-mwezi. Pia, kalenda kadhaa zilizotumiwa kabla ya Uislamu huko Arabia Kusini zilifuata mfumo wa jua-mwezi[1].
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ F.C. De Blois, "TAʾRĪKH": I.1.iv. "Pre-Islamic and agricultural calendars of the Arabian peninsula", The Encyclopaedia of Islam, 2nd edition, X:260.
Viungo vya Nje
[hariri | hariri chanzo]- Introduction to Calendars Ilihifadhiwa 13 Juni 2019 kwenye Wayback Machine., US Naval Observatory, Astronomical Applications Department.
- Lunisolar calendar year 2017-2018 Ilihifadhiwa 2 Januari 2020 kwenye Wayback Machine. (by Serge Bièvre)
- Lunisolar Calendar
- Luni-Solar Calendar
- Calendar studies
- Model of lunisolar calendar based on observation of the Sun and Moon position