Lugha

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Lugha (kutoka Kiarabu: لغة) ni utaratibu wa kuwasiliana kati ya binadamu au pengine hata kati ya viumbe wenye akili.

Mwaka wa 2008 ulikuwa Mwaka wa Lugha wa Kimataifa.

Somo la lugha linaitwa maarifa ya lugha au isimu.

Maana ya neno "lugha"

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zilizokua katika mpango maalum na zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani ili zitumike katika mawasiliano.

Mara chache neno lugha linatumika kwa taratibu za kuwasiliana za wanyama. Lakini taratibu hizo ni tofauti sana: katika lugha za wanyama, sauti moja ina maana moja tu. Lakini katika lugha za binadamu, sauti nyingi zinaunganishwa kutengeneza maneno, na maneno mengi yanaunganishwa kutengeneza sentensi. Hivyo mnyama ambaye anaweza kutengeneza sauti ishirini tofauti anaweza "kusema" mambo ishirini tu. Kwa upande mwingine mtu ambaye anaweza kutengeneza sauti ishirini, anaweza kusema mambo zaidi ya milioni.

Tabia za lugha

  • Lugha huzaliwa
  • Lugha hukua = (kuongezeka kwa maneno, kuongezeka kwa idadi ya wazungumzaji, kuwa na mawanda mapana, kusanifiwa)
  • Lugha hufundishika
  • Lugha huathiriana
  • Lugha lazima ijitosheleze
  • Lugha hufa

Sifa za lugha

  • Lugha lazima iwe inahusu binadamu
  • Sauti-sauti hufanywa na mwanadamu
  • Lugha hufuata misingi ya fonimu, yaani, a, b, c, h, d, z
  • Lugha huwa na mpangilio maalumu wenye kubeba maana. Mpangilio huo huanza na fonimu ---> Silabi ---> Neno
  • Lugha hujitambulisha ili kuzalisha maneno mengi.

Dhima za lugha

  1. Lugha hutumika kama chombo cha mawasiliano kwa kupashiana habari.
  2. Lugha hutumika kujenga umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanajamii.
  3. Lugha hutumika kutunza, kukuza, na kuendeleza utamaduni wa jamii.
  4. Lugha hutumika katika kutetea maarifa mbalimbali (ni nyenzo ya kufundishia).
  5. Lugha hutumika kama alama ya utambulisho wa kabila/jamii au taifa fulani.

Aina za lugha kwa kigezo cha uwasilishaji

Kimsingi lugha ni moja. Uwasilishwaji wake ndio huigawa katika tanzu/aina kuu mbili:

  1. Lugha ya mazungumzo
  2. Lugha ya maandishi

Lugha ya mazungumzo

Hii ni lugha ambayo huwasilishwa kwa njia ya mazungumzo ya mdomo - na hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mazungumzo. Lugha ya mazungumzo ni kongwe, hai na halisi zaidi ya mzungumzaji na ina maana nyingi, kwani mzungumzaji na msikilizaji huwa ana kwa ana katika mazingira mamoja.

Stadi za lugha ya mazungumzo ni kuzungumza na kusikiliza.
Na. Chanzo Kikomo
1 Kuzungumza Kusikiliza
2 Mzungumzaji Msikilizaji

Lugha ya maandishi

Hii ni lugha ambayo huwasilishwa kwa njia ya maandishi. Hii ni kiwakilishi cha lugha ya mazungumzo katika mfumo wa maandishi. Lugha ya maandishi ni changa kwani imeanza milenia za hivi karibuni baada ya kuvumbuliwa kwa maandishi.

Stadi za lugha ya maandishi ni kuandika na kusoma.
Na. Chanzo Kikomo
1 Kuandika/Maandishi Kusoma
2 Mwandishi Msomaji

Kwa kawaida, lugha ni sehemu ya utamaduni wa umma fulani. Lugha ya aina hii inaitwa lugha asilia. Lakini pia kuna lugha za kuundwa.

Nyanja za lugha

Lugha ina nyanja kuu mbili, nazo ni:

  • Sarufi - hushughulikia kanuni za lugha
  • Fasihi - hushughulikia sanaa zitokanazo na lugha husika ili kuumba kazi mbalimbali za kifasihi.

Kukua na kufa kwa lugha

Tangu siku za kwanza za binadamu, lugha zimekuwa zikichipuka, kukua, kutangaa na kufa kama kiumbe yeyote mwingine. Kwa hivyo, lugha zilizopo leo ulimwenguni, huenda baada ya karne nyingi kupita zikatoweka na kuzuka nyinginezo.

Leo ulimwenguni mathalan, kuna lugha karibu 6,700, zikiwa 1,000 katika bara la kaskazini na la kusini la Amerika, 2,000 zikiwa kwenye bara la Afrika, 230 katika bara la Ulaya, 2,200 katika bara la Asia, na 1,300 katika bara la Oshania (Australia na nchi jirani nayo).

Kurasa zinazohusiana

Tazama pia

Viungo vya nje

WikiMedia Commons
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu: