Ludoviko wa Fossombrone
Ludoviko wa Fossombrone (jina asili kwa Kiitalia: Ludovico Tenaglia; 1490 hivi - 1560 hivi) alikuwa padri Mfransisko wa Dola la Papa ambaye aliongoza na kufanikisha kwa miaka 10 ya kwanza (1525-1535) juhudi za urekebisho zilizozaa tawi la Wakapuchini. Ndiye mwandishi mkuu wa katiba ya awali ambayo ilisisitiza sana ukaapweke na kupitishwa na mkutano mkuu wa Albacina (Fabriano) mwaka 1529.
Baada ya mikutano mikuu iliyofuata (1535 na 1536) kutomchagua tena kama kiongozi na kupitisha katiba mpya iliyotungwa hasa na Bernardino wa Asti, aliamua kutoka shirikani akaishi kifukara kama mkaapweke sehemu za Umbria na Marche.
Usuli
[hariri | hariri chanzo]Mwaka 1525 Mateo wa Bascio alimkimbilia Papa Klementi VII (1523-1534) ili kuruhusiwa ashike kanuni ya Ndugu Wadogo, avae kanzu asili na kuhubiri huko na huko alivyotaka. Alipokubaliwa, walijiunga naye ndugu wawili, Ludoviko na Rafaeli wa Fossombrone. Mtumishi wa kanda aliwatafuta sana, lakini walilindwa vizuri na Katerina Cibo, ndugu wa Papa. Ili kukwepa dhuluma, wakajiunga na Wakonventuali, halafu wakapewa na Klementi VII haki ya kuwa na Mtumishi wao maalumu, ingawa chini ya Mkuu wa Wakonventuali, na ya kupokea wanovisi (1528). Mapema walianza kuitwa Wakapuchini kutokana na kofia yao kubwa. Upinzani wa Mkuu wa OFM dhidi yao haukufaulu; kinyume chake, kwa kuwa alitaka kuzuia hata makao ya upwekeni ndani ya shirika, ndugu wengi wenye bidii wakakata tamaa wakajiunga na Wakapuchini. Njama nyingine za kuwakomesha zikashindikana, hivi kwamba mwaka 1535 walikuwa tayari 700. Ndipo aliposhika uongozi wao Bernardino wa Asti aliyelipatia shirika jipya sura ya kiroho ya kudumu, hasa kwa njia ya katiba iliyotungwa mwaka huo na kupitishwa mwaka uliofuata.
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- F. Canuti, L. e gli inizi dei minori cappuccini, Fano 1929 (Kiitalia)
- Lexicon Capuccinum, Romae 1951, coll. 996 s. (Kiitalia)
- Mariano d'Alatri, L. da F., in Diz. degli Istituti di perfezione, V, Roma 1978, coll. 752-754 (Kiitalia)
- Id., Bernardino d'Asti, in Santi e santità nell'Ordine cappuccino, a cura di Mariano d'Alatri, I, Roma 1980, pp. 21-24, 28 (Kiitalia)
- Id., I cappuccini: storia d'una famiglia francescana, Roma 1994, ad ind.; L. da F. e l'Ordine dei cappuccini. Atti del Convegno di Fossombrone (1993), a cura di V. Criscuolo, Roma 1994 (Kiitalia)