Lango:Sanaa/Makala iliyochaguliwa/1

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Mozaiki ya maua ya Ugiriki ya Kale, katika Uturuki ya leo

Mozaiki (au mosaiki) ni mtindo wa pekee wa uchoraji picha unaotumia vipande vidogo vya kioo cha rangi au vigae vya rangi mbalimbali vinavyounganishwa kuwa picha. Kunawezekana pia kutumia vipande vya vitu vyovyote vyenye rangi vinavyoweza kuunganishwa kuwa picha.

Mtindo huu ulionekana mara ya kwanza huko Phrygia (katika Uturuki ya leo) iliyokuwa sehemu ya ustaarabu wa Ugiriki ya Kale. Mawe ya rangi nyeupe na nyeusi yalipangwa ukutani au kwneye sakafu kuwa tarakibu. Baadaye Wagiriki na zaidi Waroma waliendelea kuongeza rangi na kutunga picha kamili si tarakibu tu kwenye kuta za nyumba. Maghofu ya Kiroma yanaonyesha mifano mingi iliyodumu hadi leo.

Sanaa ya mozaiki iliendelezwa katika ustaarabu wa Bizanti. Wabizanti walipamba makanisa, majumba ya kifalme na pia nyumba za matajiri kwa mozaiki nzuri kabisa.

Waarabu Waislamu walipotwaa shemu kubwa za milki ya Bizanti waliendelea kuwaajiri wasanii Wabizanti wakipamba misikiti kama msikiti wa Umawiya huko Dameski au majumba ya masultani.

Baadaye walikuwa mafundi Waislamu waliopamba makanisa na nyumba katika Italia ya kusini.