Nenda kwa yaliyomo

Kyrilo wa Saloniki

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Kyrilo na Methodio mitume wa Waslavoni

Mtakatifu Kyrilo (kwa Kigiriki: Κύριλλος, Kyurillos; kwa Kikyrili: Кирилъ;Thesalonike, 815; Roma, 14 Februari 869) alikuwa mmisionari, mmonaki na mtaalamu wa Kigiriki aliyeweka msingi wa utamaduni wa Kikristo kati ya mataifa ya Waslavoni.

Tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kifo chake[1].

Alipozaliwa na askari wa Kibizanti na mama Mslavoni mjini Thesaloniki (kifupi Saloniki) katika Ugiriki ya kaskazini wakati wa enzi za Dola la Bizanti alipewa jina la "Konstantino"

Jina la "Kyrilo" alilipokea baada ya kujiunga na monasteri.

Ujana na elimu

[hariri | hariri chanzo]

Alipokea mafunzo yake ya ngazi ya juu kwenye chuo kikuu cha mji wa Konstantinopoli katika masomo ya falsafa, sarufi, mahubiri, muziki, hesabu, jiografia na astronomia. Alijifunza pia lugha za Kigiriki, Kilatini, Kiaramu na Kiebrania. Baadaye aliongeza Kiarabu. Lahaja za Kislavoni alizijua tangu utotoni.

Mwaka 848 alijiunga na utumishi wa Kanisa akapokea ushemasi. Katika mapokeo ya Waorthodoksi angeruhusiwa kufunga ndoa kwanza lakini aliamua kufuata mtindo wa wamonaki. Mwaka 850 alipewa kazi ya kufundisha falsafa kwenye chuo kikuu cha Konstantinopoli.

Safari kwa Waarabu na Wakhazari

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 851 alitumwa kama balozi wa Kaisari kwenda Samarra akiwa na ujumbe kwa Khalifa Al-Mutawakkil alipoingia katika majadiliano na wataalamu Waislamu kuhusu Mungu na Utatu.

Alifanya safari nyingine kubwa kwenda kwa Wakhazari waliokuwa Waturuki waliofuata imani ya Uyahudi katika maeneo kaskazini kwa Bahari Nyeusi.

Safari kwenda Moravia kati ya Waslavoni

[hariri | hariri chanzo]

Mwaka 862 Rastislav mtawala wa Waslavoni katika Moravia alimwomba Kaisari Mikaeli III Konstantino wa Konstantinopoli kumtuma "askofu na mwalimu" atakayefundisha watu wa kawaida katika Ukristo kwa lugha ya watu. Inaaminiwa ya kwamba Ratislav alitaka kujenga Ukristo na kanisa nchini mwake bila ya kutegemea majirani Wajerumani waliowahi kujenga misingi ya Ukristo katika Moravia. Hivyo alitafuta uhusiano na Bizanti iliyofuata mtindo tofauti wa Ukristo ambayo haikuwa chini ya Papa wa Roma.

Kaisari alimtuma Kyrilo pamoja na mdogo wake Methodio kwa sababu wote wawili walikuwa watu wa kanisa wenye elimu nzuri wakijua lugha ya Kislavoni toka kwa mama yao.

Tafsiri na alfabeti mpya

[hariri | hariri chanzo]

Tangu mwaka 863 Kyrilo na Methodio waliisha na kufanya kazi kati ya makabila ya Waslavoni. Walitafsiri sehemu za Biblia hasa Agano Jipya na liturgia katika lugha ya watu. Walifaulu hata kupata kibali cha Papa kwa matumizi ya Kislavoni kanisani. Waliunda aina ya lugha inayojulikana kama "Kislavoni cha kanisa" inayoendelea kutumiwa hadi leo katika liturujia ya Wakristo Waorthodoksi Urusi, Serbia na Bulgaria.

Kwa kazi yao walianzisha aina ya mwandiko wa pekee iliyokuwa chanzo cha alfabeti inayoitwa hadi leo "Kikyrili" kwa heshima ya Kyrilo.

Kwa shughuli zao Kyrilo na Methodio walieneza Ukristo na kuweka msingi kwa utamaduni wa Kikristo kati ya mataifa ya Kislavoni ya leo.

Sala yake

[hariri | hariri chanzo]

Utakase, ulinganishe taifa lako katika imani ya kweli na ungamo sahihi, na kuangaza mioyoni neno la mafundisho yako.

Kwa kuwa ni zawadi yako kutuchagua tuihubiri Injili ya Kristo wako, kuchochea ndugu watende mema na kutimiza yanayokupendeza.

Wale ulionipa nakurudishia kama wako; uwaongoze sasa kwa mkono wako wa kuume wenye nguvu, uwalinde kivulini mwa mabawa yako, ili wote wasifu na kutukuza jina lako la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Amina.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]
Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.