Kisumwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jump to navigation Jump to search

Kisumwa ni kata ya Wilaya ya Rorya katika Mkoa wa Mara, Tanzania yenye postikodi namba 31321[1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 12,447 waishio humo.[2]

Kata ya Kisumwa ina vijiji vitano ambavyo ni: kijiji cha Nyanchabakenye, kijiji cha Nyanjagi, kijiji cha Kisumwa, kijiji cha Kwibuse na kijiji cha Marasibora, lakini pia kata hii ya Kisumwa ina vitongoji zaidi ya 35. Ifuatayo ni orodha ya vijiji vya kata ya Kisumwa na vitongoji vyake kwa mpangilio wa Wilaya ya Rorya[3].

Mipaka ya kata ya Kisumwa kwa upande wa Magharibi inapakana na kata ya Rabour, kusini inapakana na mto Mara, Kaskazini inapakana na kata ya Nyathorogo na upande wa mashariki inapakana na kata ya Manga.

40 Kijiji cha Nyanchabakenye 222 Gusuhi 223 Kyabaroti 224 Koromore 225 Nyankomogo 226 Kyabhunyonyi 227 Bugoti 228 Samo 229 Kyebe 230 Buhemba

41 Kijiji cha Nyanjagi 231 Nyangoso 232 Shuleni 233 Kosasi 234 Mkuyuni 235 Nyamahe

42 Kijiji cha Kisumwa 236 Kisumwa 237 Kyamugire 238 Byashushe 239 Kyabhunyonyi 240 Senta 241 Mwisyaga 242 Tingirime 243 Kitongo 244 Gusuhi

43 Kijiji cha Kwibuse 245 Bossi 246 Kisogoti 247 Kwibuse 248 Nyangabi 249 Kukona 250 Nyabirima

44. Kijiji cha Marasibora 251 Kamba 252 Mlimani 253 Senta 254 Karama 255 Kyangera 256 Isuti 257 Rengo

Historia[hariri | hariri chanzo]

Kata ya kisumwa ina historia yake iliyojikita katika nyanja zote za jamii, siasa, utamaduni na uchumi kama ifuatavyo.

Kisiasa jamii hii ilikuwa na watawala walioitwa "Wakama" na "Wangwana".

Miaka ya 1940 kijiji cha Nyanchabakenye kilikuwa pori: wanyama wakali waliishi humo, hususani katika mwambao wa milima ya Kyabhinyonyi na katika kijiji hiki inaaminika kuwa kuna jamii ya Wakurya waitwao Wakenye ndio waliokuwa wanaishi kwenye miteremko ya milima ya Kyabhinyonyi.

Kufikia mwaka 1962 kuliandaliwa mkakati wa kupata maji, hivyo serikali ya kipindi hicho ikaridhia kuchimba lambo katika kijiji hicho, jambo ambalo lilisababisha Wakenye wakakimbia na kupata jina la Nyanshabhakenye ambalo baadae lilitoholewa na kuwa Nyanchabakenye.

Maana ya neno Nyansha kwa mujibu wa lugha ya Kikurya ni "Ziwa" Bhakenye hawa ni jamii ya Wakurya.

Mwaka 1990 Wasimbiti waliingia kwenye vita baina ya Wajaluo kuhusu ardhi; vita hivyo vilisababisha madhara ya kijamii na ya kiuchumi na vita hivyo viliua mtu mmoja wa Wasimbiti.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Kata hii imejaliwa kuwa na mto mkubwa ambao haukauki maji yake miaka nenda rudi: mto huo ni mto Mara.

Jamii ya wakazi wa kata ya Kisumwa ni wakulima na wafugaji. Zamani mazao waliyokuwa wakilima yalikuwa ni ulezi ambao ulikuwa ukitumika kama chakula lakini pia ulitumika kama mahari kwa ajili ya kuoa. Baadae walianza kulima mazao mengine kama mtama, mahindi, mihogo na sasa mpunga. Jamii hii haikuwa na zao maalumu la biashara hapo awali mpaka zao la mpunga lilipoanzishwa ndio likawa zao la biashara. Jamii hii iliendelea kufanya biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa. Mfano mtu aliweza kubadilishana ng'ombe kwa mbuzi au kondoo. Ukiwa na kondoo au mbuzi wanne uliweza kupewa mtamba ila ulipokuwa na mbuzi au kondoo watatu uliweza kupewa ndama dume la ng'ombe.

Kwa sasa kata ya Kisumwa imeanza kujishughulisha na kilimo cha zao la alizeti kama zao la biashara: lengo kubwa la zao hili na mwanzilishi wake katani hapo ni kuweza kuondoa umaskini uliokithiri katani kwani kaulimbiu inayotumika ni "lima alizeti tokomeza kukata miti kwa uchomaji wa mkaa".

Pia kiwanda kikubwa kinajengwa katika kijiji cha Nyanchabakenye chini ya Mkurugenzi wa Zanziba & Nyihita Co. Ltd.

Utamaduni[hariri | hariri chanzo]

Utamaduni wa jamii hii ulijikita kwenye tohara na ukeketaji.

Kuhusu historia ya ukeketaji katika jamii ya watu wa kata ya Kisumwa inaaminika kuwa tangu miaka ya 1700 Wakurya walianza kuwakeketa mabinti zao. Zoezi hili liliendana na miiko ya jamii hii kwa kuamini kuwa ili binti aweze kuitwa mtu mzima lazima aweze kukeketwa. Ilipotokea binti kukeketwa tayari binti alikuwa na sifa ya kuweza kuchumbiwa, tayari kwa kuolewa.

Sambamba na hilo kulitokea ugonjwa wa kujikuna sehemu za siri hususani kwenye kinembe. Ugonjwa huo ulikuwa tishio kwa jamii ya Wakurya: ndipo wakajaribu kufanya uchunguzi wa kipi kifanyike ili kuweza kukomesha ugonjwa huo, ndipo walipojaribu kukata kinyama hicho cha kwenye sehemu za siri za mwanamke mgonjwa na ugonjwa huo ulikoma kabisa kwa mhusika. Hivyo jamii ilikubaliana ili kuondoa tatizo hili ni lazima kila mtoto wa kike aweze kukeketwa. [4]

Njia zilizotumika kuhamasisha jamii hii kukeketa watoto wao wa kike ni pamoja na majina ya kashfa kama Omosaghane na pale ilipotokea binti akajifungua bila kukeketwa ailiitwa "Irikunene". Lakini pia ilipogundulika kuwa mwanamke hajakeketwa alitakiwa kufanyiwa hivyo, hata kama angekuwa mkubwa, maana ilifikia hatua jamii ya Wakurya wakaanza kuoa kwa jamii ya Wajaluo ambao walikuwa hawakeketi. Hivyo ili kuruhusu mwanamke kufanya matambiko ya watoto wake, ikiwemo tohara kwa watoto wa kiume, alitakiwa mama afanyiwe tohara.

Katika suala zima la vita Wasimbiti walikuwa wakienda katika pango lililoko mlima wa Kyabhinyoni (pango lililokuwa maarufu kwa jina la Kyabhosongo) kwa lengo la kuchukua sumu ya kuweka kwenye mishale yao. Inaaminika kuwa mlango uliokuwa na uwezo wa kuingia katika pango hilo ni Wakehenge kwa sharti la kutotembea na binti ambaye hajakeketwa.

Ibada za jamii ya Wasimbiti waishio kata ya Kisumwa zimeendelea kuwepo kulingana na matukio. Ibada iliyohusu suala zima la kilimo walikuwa wanakuta milango yote minane (8) yaani Nyabhananta kujadili mustakabali wa mvua katika jamii hiyo.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. https://www.tcra.go.tz/images/documents/postcode/mara.pdf
  2. Sensa ya 2012, Mara - Rorya-District-Council
  3. kuanzia no 40 hadi no 44 ni majina ya vijiji vya kata ya kisumwa kulingana na mpangilio wa vijiji kiwilaya, no 222 hadi no 257 ni majina ya vitongoji vya kila kijiji kiwilaya
  4. Chanzo cha habari hiyo ni utafiti wa wanafunzi wa shule ya sekondari ya Kisumwa mwaka 2010. Mada ilikuwa "The Impact of Femal Genital Multilation".
Flag of Tanzania.svg Kata za Wilaya ya Rorya - Mkoa wa Mara - Tanzania
Flag of Tanzania.svg

Bukura * Bukwe * Goribe * Ikoma * Kigunga * Kirogo * Kisumwa * Kitembe * Komuge * Koryo * Kyang'ombe * Mirare * Mkoma * Nyahongo * Nyamagaro * Nyamtinga * Nyamunga * Nyathorogo * Rabour * Roche * Tai


Flag-map of Tanzania.svg Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Mara bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Kisumwa kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.

Usiingize majina ya viongozi au maafisa wa sasa maana wanabadilika haraka mno.