Parokia ya Kishogo

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
(Elekezwa kutoka Kishogo Parish)

Parokia ya Kishogo ni moja kati ya parokia 29 za Jimbo Katoliki la Bukoba.

Parokia hii ipo katika wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.

Kwa upande wa Mashariki inapatikana na Parokia za Itahwa na Mwemage zikitenganishwa na Mto Ngono. Upande wa Kaskazini imepakana na Parokia za Mugana na Buyango wakati inapakana na Kasambya na Ngarama kwa upande wa Magharibi. Ziwa Ikimba upande wa Kusini, linafanya mpaka kati ya Kishogo na Parokia ya Ichwandimi.

Kuanzia upande wa Mashariki kuzunguka Kaskazini hadi Magharibi Kishogo imezungukwa na tingatinga la Mto Ngono. Hivyo, kivuko cha Kansinda katika Mto Ngono kinaiunganisha Kishogo na sehemu za Kaskazini wakati kivuko cha Kyanyabasa katika mto huo Ngono ni kiunganishi kati ya Kishogo na maeneo ya Mashariki hasa Itahwa na Bujugo. Upande wa Kusini kuna barabara inayoingia Kishogo ikichepuka kutoka barabara inayoelekea Katoro.

Kishogo ilifunguliwa rasmi kama parokia tarehe 1 Mei 1934 na askofu wa Bukoba wakati huo Burchard Huwiler. Pd. Oscar Kyakaraba ndiye aliyekuwa paroko wa kwanza akiwa na msaidizi wake Pd. Melchiades Kazigo. Kwa sasa Kishogo inahudumiwa na mapadre wawili.

Kabla ya kuwa Parokia, Kishogo kilikuwa kigango cha parokia ya Bunena. Ilipopewa hadhi ya kuwa parokia, Kishogo iliunganisha pia maeneo yaliyokatwa kutoka parokia ya Kagondo yaani Mwemage na Ngarama. Wakati huo Kishogo ilikuwa na jumla ya Wakatoliki 2,138 na wakatekumeni 481. Kulingana na sensa ya mwaka 2009, Kishogo inao Wakatoliki 13,603 ambao ni asilimia 71 ya wakazi wote wapatao 19,209.

Shughuli za maendeleo za wakazi wa maeneo haya hasa ni kilimo, uvuvi, ufugaji kidogo pamoja na biashara ndogondogo.

Kwa asili mazingira ya parokiani Kishogo yanavutia sana, Kishogo ipo katika mwinuko na hivyo, utafurahia upepo mwanana wenye ubaridi kutoka mto Ngono upande wa Mashariki. Kabla hujaingia kanisani utapokewa na mandhari nzuri ya miti iliyopandwa kitaalamu kwa rula yenye vipimo vikali. Ukijani wa nyasi fupi zilizopandwa katika mazingira utakuongoza taratibu kila upande wa barabara utakayopitia kuelekea lango kuu ambapo sanamu za Watakatifu Petro na Paulo, wasimamizi wa Parokia hiyo zitakuongoza kuingia kanisani.

Ukatoliki ulifika Kishogo katika siku za mwanzoni kabisa za uinjilishaji katika Jimbo la Bukoba mwaka 1892. Imani ya Kikatoliki katika parokia ya Kishogo ililetwa na mlei Cyprian Kabyeju, mzawa wa parokia ya Itahwa. Mzee huyo alizaliwa mwaka 1883 katika kijiji cha Kitwe, Parokia ya Itahwa, alibatizwa na Pd. Nogaret tarehe 15 Machi 1913 katika kanisa la Bunena akiwa na umri wa miaka 30 na alifariki tarehe 18 Februari 1930. Huyu ndiye aliyepanda mbegu ya mwanzoni ya imani ambayo baadaye ilimwagiliwa na kupaliliwa na wamisionari na mapadre wazawa walioimarisha imani hiyo mpaka sasa.

Mpaka mwaka 1934 Kishogo ilikuwa ni kigango cha parokia ya Bunena. Wakati huo Parokia ya Bunena iliunganisha eneo lote ambalo kwa sasa ni parokia za Bukoba, Kishogo, Itahwa na Maruku, Pd. Caesar aliyekuwa paroko wa Bunena akishirikiana na shirika la White Fathers alimtuma Pd. De Wit ambaye ndiye alikuwa mmsionari wa kwanza wa White Fathers kufika Kishogo kuinjilisha.

Wakati Kishogo inaanzishwa iliunganisha eneo lote la Parokia ya Kishogo na Parokia ya Ngarama. Kabla ya hapo Ngarama ilikuwa ikihudumiwa na parokia ya Kagondo mpaka tarehe 16 Disemba 1951 ilipoanzishwa Vikarieti ya Kitume ya Kagera ya Chini ambayo baadae ilikuwa Jimbo la Rutabo likiongozwa na askofu Laurean Rugambwa. Katika kuanzishwa kwa vikarieti hiyo, eneo la Mwemage na Ngarama lilimegwa kutoka Parokia ya Kagondo na kuwa sehemu ya parokia ya Kishogo jimboni Rutabo. Parokia nyingine za Jimbo la Rutabo zilikuwa Kanyigo, Kashambya, Mugana na Rutabo.

Mwanzoni parokia ya Mwemage ilikuwa Kigango cha parokia ya Kagondo. Ilipoundwa vikarieti ya Lower Kagera, kigango hiki kikawa chini ya parokia ya Kishogo. Mwadhama alimkabidhi Pd. John Ndibalema akitayarishe kiwe parokia. Kwanza alijenga nyumba ya mapadre, waamini walimuunga mkono katika juhudi zake. Kati ya hao ni Clement Rwehikiza wa Kishonga, Benedicto Rutahiwa wa Karonge, na Patrice; pamoja na wakristo wengine wa Ibwera.

Baada ya maandalizi ya kutosha, mwaka 1955 Kishogo ikajifungua mtoto wa kwanza - parokia ya Mwemage. Baadae juhudi za ujenzi wa kanisa la parokia kwa msaada mkubwa kutoka kwa Masista Wafransisko.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  • Jubilei ya Miaka 75 ya Parokia ya Watakatifu Petro na Paulo, Kishogo, Bukoba: Rumuli Printing Press, 2009
Makala hii kuhusu Kanisa Katoliki bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Parokia ya Kishogo kama historia yake au maelezo zaidi?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.