Kilele Kiitwacho Uhuru

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kilele Kiitwacho Uhuru ni riwaya iliyoandikwa na Filipo GaoLubua (aka Filipo Lubua), mwandishi wa riwaya na mashairi kutoka Tanzania ambaye kwa sasa anaishi nchini Marekani.

Riwaya hii ni moja ya riwaya mahiri zilizoandika hali ya siasa na jamii katika nchi za Afrika, takribani miongo mitano baada ya uhuru. Katika zama hizo, bado wanasiasa wachache waliojitwalia madaraka wanaendelea kujineemesha na kufaidi mema na fanaka za nchi zao huku wakiwaacha wananchi wao wengi wakitapatapa katika umaskini na uhohehahe[1].

Riwaya hiyo ilichapishwa mwaka 2014 na jumba la uchapishaji la Jomo Kenyatta Foundation (JKF).

Muhtasari[hariri | hariri chanzo]

Faili:Bm4maoGCAAEiClY.jpg
Jalada

Riwaya ya Kilele Kiitwacho Uhuru inazungumzia nchi ya Marumere, ambayo iko katika mwambao wa Pwani ya Afika Mashariki. Hata hivyo pamoja na nchi hiyo kuwa katika mfumo wa vyama vingi, ni chama kimoja tu ambacho kimeshikilia madaraka ya nchi hiyo tangu ilipopata uhuru. Chama hicho kimekuwa kikiendeleza rushwa, ufisadi na kuneemesha wanasiasa wachache huku vikundi vingine vya kijamii vikibaki katika hali duni. Mwalimu wa shule ya sekondari nchini humo, Mwalimu Fadhili, anajitoa mhanga kutafuta mabadiliko na kuifikisha nchi yake katika 'Kilele Kiitwacho Uhuru'. Je. kazi hii itakuwa rahisi? Ataweza kutoa mnofu wa nyama nono mdomoni mwa watu wenye meno makali?

Mtunzi[hariri | hariri chanzo]

Filipo Lubua alizaliwa Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania. Baada ya kuhitimu elimu ya juu ya sekondari mwaka 2006, alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa shahada ya kwanza katika Sanaa na Elimu (B.A.Ed.) mwaka 2009, ambako alitaalamikia masomo ya Jiografia na Isimu. Mwaka 2010, alikwenda Chuo Kikuu cha Wisconsi Madison, Marekani, kama mwalimu wa Kiswahili kupitia ufadhili wa nchi ya Marekani chini ya programu maarufu ya Fulbright. Baada ya programu hiyo, mwaka 2012 alijiunga na Chuo Kikuu cha Ohio, kwa masomo ya umahiri katika Isimu Tumizi, akitaalamikia Ufundishaji na Ujifunzaji wa Lugha kwa Kompyuta (UULUKO). Baada ya masomo ya umahiri mwaka 2014, alijiunga na programu ya uzamivu na mwaka 2019 alitunukiwa digirii ya uzamivu (Ph.D.) katika masuala ya Teknolojia ya Elimu (Instructional Technology).

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. "Kiswahili novelists tackle all the relevant themes". Daily Nation (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2020-04-03. 
Makala hii kuhusu kitabu fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kilele Kiitwacho Uhuru kama Mwandishi wake, hadithi au matoleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.