Katerina wa Bologna

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Katerina wa Bologna ni jina linalotumika kwa kawaida kumtajia Katerina wa Vigri (8 Septemba 1413 - 9 Machi 1463), bikira na abesi wa monasteri ya Bologna ya Shirika la Mtakatifu Klara aliyelea kiroho wanawake wengi hata kwa maandishi bora.

Alitangazwa na Kanisa Katoliki kuwa mwenye heri tarehe 13 Novemba 1703 na mtakatifu tarehe 22 Mei 1712.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kifo chake[1].

Maisha[hariri | hariri chanzo]

Bikira Maria na mtoto Yesu walivyochorwa na Katerina wa Bologna.
Kitabu Sette armi spirituali, kilichoandikwa na Katerina mwaka 1475.

Katerina alizaliwa huko Bologna na Yohane wa ukoo wa kisharifu wa Vigri na Yohane na Benvenuta Mammolini.

Tangu utotoni alilelewa kwa bidii na kusoma hata Kilatini.

Mwaka 1424, akiwa na miaka 11, Katerina alihamia ikulu ya Ferrara na kuendelea vizuri na elimu ya wakati ule: muziki, uchoraji, dansi, ushairi, unakili.

Mwaka 1427 alihama na kujiunga na kundi la wasichana walioishi pamoja wakifuata kwanza maisha ya kiroho ya Agostino wa Hippo, lakini mwaka 1432 waliweka nadhiri ya kushika kanuni ya Klara wa Asizi, na kufuata maisha ya ndani tu katika monasteri.

Kutokana na heshima iliyomfuata kwa karama zake za pekee, mwaka 1456 ilimbidi akubali ombi la mji wake wa asili kwamba arudi na kuanzisha monasteri nyingine, ambayo akaiongoza kama abesi hadi kifo chake miaka 7 baadaye.

Abesi wa monasteri ya Ferrara, Leonarda Ordelaffi, aliwaandikia watawala wa Bologna: “Mjue kwa hakika kwamba nawapatia mtakatifu Klara wa pili”.

Katerina ni kati ya Waklara wa Observantia ambao walishika upendo kwa ustaarabu pamoja na kukazania zaidi utakatifu katika njia ya toba na unyenyekevu, kwa mfano Eustokia Calafato wa Messina na Batista Varano wa Camerino.

Kwa vipaji vyake vingi, Katerina alikuwa pia mchoraji mzuri. Kazi zake zinatunzwa sehemu mbalimbali za Italia.

Baada ya kifo[hariri | hariri chanzo]

Mwili wake ulizikwa siku ya kufa kwake, lakini baada ya wiki mbili ulitolewa kaburini ukiwa haujaoza bali unanukia; baada ya matatizo mbalimbali uliwekwa kwenye kiti ambapo umeketi hata leo karibu na kanisa lake huko Bologna (Italia).

Tazama pia[hariri | hariri chanzo]

Maandishi yake[hariri | hariri chanzo]

  • Silaha saba za roho (Le sette armi spirituali, Ed. Monastero del Corpus Domini, Bologna 1998; pia Ed. del Galluzzo 2000;);
  • Mabustani kumi na mawili (I dodici giardini, Ed. Inchiostri Associati 1999);
  • Rosari, Utenzi wa karne XV (Rosarium, Poema del XV Secolo, Ed. Barghigiani, Bologna, 1997);
  • Hotuba (I sermoni, Ed. Barghigiani, Bologna 1999);
  • Masifu, mada na barua (Laudi, Trattati e Lettere, Ed. del Galluzzo 2000);
  • Taji la Mama wa Kristo (Corona de la Madre de Christo, Ed. Digigraf 2006).

Tanbihi[hariri | hariri chanzo]

Viungo vya nje[hariri | hariri chanzo]

Makala hii bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mkristo huyu, kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Je, unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuiongezea habari.