Kamerun ya Kijerumani
Kamerun ya Kijerumani ilikuwa koloni la Dola la Ujerumani kuanzia mwaka 1884 hadi 1916. Koloni hilo lilijumuisha maeneo ya Jamhuri ya Kamerun, pamoja na sehemu zilizopo sasa katika kaskazini mwa Gabon na Jamhuri ya Kongo, pia sehemu za magharibi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na za kusini magharibi mwa Chad na maeneo mashariki mwa Nigeria.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Karne ya 19
[hariri | hariri chanzo]Utangulizi wa ukoloni
[hariri | hariri chanzo]Mnamo mwaka 1868 kampuni ya biashara C. Woermann kutoka mjini Hamburg ilianzisha kituo cha kwanza cha biashara katika eneo la Duala [1] kwenye delta ya Mto Kamerun [2] Wakala wa kampuni hiyo nchini Gabon, Johannes Thormählen, alipanua shughuli za kampuni yake akifuata mto Kamerun. Mnamo 1874, Thormählen aliungana na wakala wa Woermann huko Liberia, Wilhelm Jantzen. Kwa pamoja wafanyabiashara hao wawili walianzisha kampuni yao wenyewe, Jantzen & Thormählen huko.
Kampuni hizo mbili zilipanuka na kuwa na usafiri kwa jahazi na meli zao zenyewe na kuzindua huduma ya abiria na mizigo iliyoratibiwa kati ya Hamburg na Duala. [3] Kampuni hizo na nyingine zilipatana na watawala wenyeji waliowapatia maeneo ya kujenga vituo vya biashara na pia kulima mazao ya biashara ya nje kama mawese. Walifanya biashara hiyo pamoja na kampuni za Uingereza. Konsuli Mwingereza wa Afrika Magharibi alitembelea pwani ta Kamerun mara kadhaa akakubaliwa kama mwamuzi katika matatizo kati ya wafalme wengi wadogo wa pwani; wengine kama mfalme Bell wa Duala aliwahi kuomba malkia wa Uingereza kutangaza ulinzi juu ya nchi yake lakini serikali ya Uingereza hadi hapo ilikuwa imekataa[4].
Mnamo mwaka 1882, Uingereza na Ufaransa zilipatana kuhusu maeneo yenye maslahi zao kwenye pwani ya kaskazini ya Afrika ya Magharibi. Hapo Wajerumani walishtuka kwa sababu pande zote mbili hawakuuliza kama kuna mataifa mengine yenye maslahi na biashara huko wakaogopa kwamba watazuiliwa kwa njia ya kodi na ushuru.
Mapatano yaliyofuata mwaka 1884 kati ya Uingereza na Ureno kuhusu pwani ya Kongo yaliongeza hofu hizo. Kwa hiyo kundi la wafanyabiashara wa Hamburg walianza kumshawishi chansela Otto von Bismarck, mkuu wa serikali, kuangalia uwezekano wa tangazo la ulinzi wa Ujerumani juu ya biashara yao. Bismarck aliwahi kusema mara nyingi kwamba hakutaka koloni kwa kuwa aliziona kama njia ya kupoteza pesa. Lakini maombi ya wafanyabiashara kulinda biashara ya Kijerumani yaliweza kumshawishi akabadilika siasa yake[5] akiamini kwamba tangazo la ulinzi juu ya maeneo ya Afrika haliwezi kusababisha gharama kama kampuni za biashara zinaendesha uhusiano na watawala wenyeji ilhali serikali yake inazuia tu nchi nyingine za Ulaya kuanzisha utawala hapa[6].
Kuundwa kwa koloni la Kijerumani
[hariri | hariri chanzo]Wakati huohuo Waingereza waliandaa tayari mikataba na wafalme wa pwani ili wakubali ukuu wao, hasa kwa sababu waliogopa uenezaji wa Wafaransa waliokuwa maarufu kuzuia wafanyabiashara wa mataifa mengine. Lakini utume wa Bismarck uliwahi [7] na tarehe 14 Julai 1884 mfalme Bell wa Duala alitia sahihi mkataba alipoweka nchi yake chini ya ulinzi wa Ujerumani.
Ujerumani ilipendezwa hasa na nafasi za kilimo wa Kamerun ikaomba kampuni kubwa kuanzisha mashamba na kuuza nje uzalishaji wake. Bismarck alifafanua vipaumbele vyake: "kwanza mfanyabiashara, kisha askari". Kampuni kubwa za biashara za Ujerumani (Woermann, Jantzen und Thoermalen) na kampuni za mashamba (Sudkamerun Gesellschaft, Nord-West Kamerun Gesellschaft) zilipatiwa maeneo makubwa katika koloni. Serikali ya koloni ilisaidia kampuni kubwa kupanua mashamba na pia biashara na maeneo ya bara, mbali na pwani. Hapo jeshi la serikali liliongozana na wafanyabiashara na kupiga vita dhidi ya wenyeji ambao hawakutaka hao Wazungu wasikike kwao. Sehemu muhimu ya kazi ya serikali ilikuwa kutafuta wafanyakazi kwa ajili ya mashamba makubwa; mara kwa mara wenyeji walilazimishwa kwa nguvu kukubali mikataba ya kazi kwa vipindi vya miezi sita. Upinzani wa wenyeji ulivunjwa kwa nguvú ya kijeshi. [8]
Karne ya 20
[hariri | hariri chanzo]Uenezaji wa utawala
[hariri | hariri chanzo]Ujerumani polepole ilipanua koloni, ikikutana na upinzani mkali katika Vita ya Bafut na Vita ya Adamawa. Kwa jumla gharama za kuendesha serikali na jeshi zilizidi faida ya Ujerumani kutokana na koloni, lakini kampuni za biashara zilipata faida. [9]
Kwa ruzuku kutoka hazina ya kitaifa, serikali ya koloni ilijenga njia mbili za reli kutoka mji wa bandari wa Duala. Njia ya Kaskazini ilikuwa na urefu wa kilomita 160 hadi milima ya Manenguba, na njia kuu ilifika Makak kwenye mto Nyong kwa umbali wa kilomita 300. [10] Mfumo wa posta na telegrafu na mtandao wa meli za serikali kwenye mito mikubwa uliunganisha pwani na maeneo ya ndani.
Mwisho kwenye Vita Kuu ya Kwanza
[hariri | hariri chanzo]Wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia, majeshi ya Ufaransa, Ubelgiji na Uingereza yalivamia koloni la Kijerumani mwaka 1914 na kulitwaa. Ngome ya mwisho ya Wajerumani kujisalimisha ilikuwa ile iliyoko Mora, kaskazini mwa koloni, mnamo 1916.
Kufuatia kushindwa kwa Ujerumani, Mkataba wa Versailles uligawa eneo hilo katika mamlaka mbili za Shirikisho la Mataifa (kundi B) chini ya utawala wa Uingereza na Ufaransa. Cameroon ya Kiingereza na sehemu kubwa ya ile ya Kifaransa ziliungana tena mwaka wa 1961 kama Jamhuri ya Kamerun.
-
Mtafiti wa Ujerumani huko Kamerun, 1884
-
Polisi huko Duala kwenye siku ya kuzaliwa ya Kaiser, 1901
-
Ndizi zikipakiwa kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Ujerumani, 1912
Tanbihi
[hariri | hariri chanzo]- ↑ present-day Douala
- ↑ now the Wouri River delta
- ↑ Washausen, Hamburg und die Kolonialpolitik, p. 68
- ↑ HARRY R. RUDIN: Germans in the Cameroons 1884-1914, a case study in modern imperialism, Yale University Press 1938, uk. 23ff
- ↑ John Iliffe: Africans, The History of a Continent, Second Edition Cambridge 2007 ISBN-13 978-0-511-34916-4, uk 195
- ↑ Rudin, uk. 29f
- ↑ Haupt, Deutschlands Schutzgebiete, p. 57
- ↑ Thomas Deltombe, Manuel Domergue, Jacob Tatsita, KAMERUN !, La Découverte, 2019
- ↑ By 1911 the total volume of trade reached over 50 million gold marks [Haupt, p. 64].
- ↑ This line was later extended to the current Cameroon capital of Yaoundé.
Kujisomea
[hariri | hariri chanzo]- DeLancey, Mark W.; DeLancey, Mark D. (2000). Historical Dictionary of the Republic of Cameroon (toleo la 3rd). Lanham, Maryland: The Scarecrow Press. ISBN 0-8108-3775-7. OCLC 43324271.0-8108-3775-7
- Gorges, E. Howard (1923). Vita Kuu katika Afrika Magharibi . London: Hutchinson & Co.
- Haupt, Werner (1984). Deutschlands Schutzgebiete in Übersee 1884–1918 [Germany’s Overseas Protectorates 1884–1918]. Friedberg: Podzun-Pallas Verlag. ISBN 3-7909-0204-7.3-7909-0204-7
- Hoffmann, Florian (2007). Okkupation und Militärverwaltung in Kamerun. Etablierung und Institutionalisierung des kolonialen Gewaltmonopols. Göttingen: Cuvillier Verlag. ISBN 9783867274722.9783867274722
- "German Cameroons 1914". UniMaps. 2004. Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 4 Aprili 2013.
{{cite web}}
: CS1 maint: date auto-translated (link) Ramani ya maeneo yaliyobadilishwa kati ya Ufaransa na Ujerumani katika Mkataba wa Fez. - Schaper, Ulrike (2012). Koloniale Verhandlungen. Gerichtsbarkeit, Verwaltung und Herrschaft in Kamerun 1884-1916. Frankfurt am Main 2012: Campus Verlag. ISBN 3-593-39639-4.
{{cite book}}
: CS1 maint: location (link)3-593-39639-4 - Washausen, Helmut (1968). Hamburg und die Kolonialpolitik des Deutschen Reiches 1880 bis 1890 [Hamburg and Colonial Politics of the German Empire]. Hamburg: Hans Christians Verlag. OCLC 186017338.
Viungo vya nje
[hariri | hariri chanzo]- http://www.numismondo.net/pm/cmr/index1.htm Benknoti za Kamerun ya Kijerumani