Kalinzi

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru


Kata ya Kalinzi
Kata ya Kalinzi is located in Tanzania
Kata ya Kalinzi
Kata ya Kalinzi

Mahali pa Kalinzi katika Tanzania

Majiranukta: 4°29′42″S 29°44′58″E / 4.49500°S 29.74944°E / -4.49500; 29.74944
Nchi Tanzania
Mkoa Kigoma
Wilaya Kigoma Vijijini
Idadi ya wakazi
 - Wakazi kwa ujumla 21,904

Kalinzi ni kata ya Wilaya ya Kigoma Vijijini katika Mkoa wa Kigoma, Tanzania yenye msimbo wa posta 47206.

Jiografia[hariri | hariri chanzo]

Jiografia ya kata hii ni ya vilima na mabonde inayofanya uwepo wa hali ya ubaridi hasahasa katika msimu wa masika na maji kutiririka katika vijito vilivyopo katika mabonde.

Kalinzi ni kata katika tarafa ya Kalinzi na ina jumla ya vijiji vitatu: Kalinzi, Matyazo na Mkabogo.

Kijiji cha Kalinzi, ambacho kimebeba makao makuu ya kata na pia tarafa, ni mojawapo ya vijiji vya muda mrefu sana hata kabla ya kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa nchini Tanzania. Ndipo walipokuwepo viongozi wa kimila waliojulikanao kama Wami (machifu) kama vile Mwami Rusimbi, Ntare na George.

Wakazi[hariri | hariri chanzo]

Katika sensa ya mwaka 2022 wakazi wa kata walihesabiwa kuwa 21,904 [1]. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 27,426 waishio humo.[2]

Wenyeji wa kata hiyo ni wa kabila la Waha na makabila machache sana ya kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania na nchi jirani waliopo hapo kwa kazi, biashara au kilimo.

Uchumi[hariri | hariri chanzo]

Kata ya Kalinzi ina fursa nyingi za shughuli za kimaendeleo kutokana na hali ya hewa nzuri na tamaduni nzuri za watu wa kata hiyo ambao ni wakarimu kwa watu na wawekezaji toka sehemu mbalimbali.

Kazi kubwa ifanyikayo na wakazi wa kata hii ni kilimo hasahasa kilimo cha chakula ambapo hulima mazao ya chakula kama vile mahindi, mihogo, ndizi (pia hutumika kibiashara), maharage, njegere, nyanya, mboga za majani na viazi. Zao kuu la biashara linalolimwa na wakazi wa kata hii na kuwaingizia pesa nyingi ni kahawa. Lakini pia watu wana misitu hivyo uvunaji na utumiaji au uuzaji wa mbao japo ni kwa kiwango kidogo sana unafanyika katika hiyo kata.

Mbali na shughuli za kilimo wakazi hujishughulisha na biashara za maduka na biashara nyingine ndogondogo ambazo hufanyika sanasana katika soko kuu la Kalinzi ambalo ni mojawapo ya masoko makubwa mkoani Kigoma.

Kwa kiasi kidogo sana wakazi wa kalinzi hujishughulisha na ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku.

Miundombinu[hariri | hariri chanzo]

Usafirishaji wa bidhaa hufanyika kupitia barabara kuu ya Ram ipitayo Kalinzi toka Kigoma mjini kuelekea Manyovu, hivyo kufanya usafirishaji wa watu na bidhaa za kilimo kuwa rahisi.

Katika kata ya Kalinzi hasahasa kijijini kalinzi kilichopo barabarani kuna huduma nyingi kama vile nyumba za kulala wageni, makanisa na misikiti, shule za sekondari ambazo zipo katika vijiji vyote vitatu zenye kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha nne, shule za msingi (kwa kila kijiji ni zaidi ya moja), hospitali kubwa ya Matiazo inayomilikiwa na kanisa la Anglikani, na zahanati iliyopo katika kijiji cha Kalinzi.

Pia kuna mahakama ya mwanzo iliyopo katika kijiji cha Kalinzi. Pia katika kijiji cha Matiazo ndipo ilipo mashine kubwa ya kukoboa kahawa na hupata wateja mbalimbali kutoka sehemu mbalimbali za mkoa wa Kigoma wajao kukoboa kahawa zao.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

Kata za Wilaya ya Kigoma Vijijini - Mkoa wa Kigoma - Tanzania

Bitale | Kagongo | Kagunga | Kalinzi | Kidahwe | Mahembe | Matendo | Mkigo | Mkongoro | Mungonya | Mwamgongo | Mwandiga | Nkungwe | Nyarubanda | Simbo | Ziwani

Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Kigoma bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Kalinzi kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Tafadhali usiingize majina ya maafisa au viongozi wa sasa maana wanabadilika mno.