Kalemela

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Kalemela ni kata ya Wilaya ya Busega katika Mkoa wa Simiyu, Tanzania yenye postikodi namba 39507 [1]. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 10,928 waishio humo.[2].

Jina Kalemela linatokana na mto unaotenganisha kata hiyo na kata jirani ya Kabita. Mto huo mdogo huingia katika ziwa Viktoria kupitia kijiji cha Mayega kilichoko kata hiyo na kijiji cha Chumve kilicho katika kata ya Kabita.

Kata ya Kalemela imepakana na kata za Kabita kwa upande wa magharibi na kusini. Upande wa kusini mashariki imepakana na kata ya Mkula, na upande wa mashariki kalemela imepakana na kata ya Ramadi. Upande wa kaskazini Kalemela imepakana na mwambao wa ziwa Viktoria. Kutokana na ukaribu wa ziwa hilo, shughuli kuu ya wakazi wa kata hii ni kilimo, ufugaji na uvuvi. Kalemela inaundwa na vijiji vya Mayega, Mwabujose, Chamugasa, pamoja na Bushigwamhala.

Historia[hariri | hariri chanzo]

Wenyeji wa Kalemela ni Wasukuma wanaotokana na ukoo wa Basega. Basega ni ukoo uliotokana na mhamiaji wa Kinyamwezi aliyejulikana kwa jina la Nyalubamba. Masimulizi ya mapokeo yanaonesha kuwa Nyalubamba alifika katika eneo la Masanza akitokea Dakama yaani Unyamwezi. Baada ya kukamata Masanza, hakufanikiwa kuikamata Nasa ambayo ilikuwa imekwisha kukaliwa na Wakamba jamii ya wafanyabiashara waliokuwa wamelowea katika maeneo hayo wakitokea Ukamba katika nchi ambayo sasa inajulikana kama Kenya.

Hatimaye Nyalubamba alifanikiwa kuipata Nyaole. Eneo la Nyaole lilihusisha Kalemela, Nyatwali na Ushashi. Nyalumba baadaye alifanikiwa kuanzisha himaya nyingine katika eneo la Bwasi kule Majita. Historia inaonyesha kuwa Nyalubamba alifariki na kuzikwa huko Bwasi Majita akiacha ukoo wa Wasaga wakitawala katika eneo la Bwasi.

Wakati wa utawala wa Wajerumani, Kalemela ilikuwa chini ya Mtemi Msalika mwana wa Malulu aliyepewa na baba yake kutawala eneo hilo. Kufuatia kushindwa kwa Wajerumani katika vita vya kwanza vya dunia (1914-1918), wakoloni wa Kiingereza walimwondoa Msalika kwa tuhuma kuwa alihifadhi askari wa Kijerumani waliokuwa wakikimbia kutoka boma lao lililokuwa Ushashi. Kalemela baada ya hapo ilibaki bila utawala ikiwa chini ya uangalizi wa Mwanangwa aliyeitwa Holela Manene. Hatimaye Kalemela ilifanikiwa kusimika mtemi mpya ambaye pia alitokana na ukoo wa Basega aliyejulikana kwa jina la Bahebe.

Kabla ya uhuru wa Tanzania mwaka 1961, Kalemela ilikuwa sehemu ya utemi mdogo wa Busega uliokuwa na makao yake katika eneo la Masanza katika kata ya Kiloleli. Kipindi hicho cha ukoloni Kalemela ilijulikana kama Masanza II. Eneo hili la utemi lilihusisha eneo la Mayega, Chamugasa, Ramadi na Nyatwali. Kwa sasa eneo la Nyatwali liko katika eneo la mkoa wa Mara, wilaya ya Bunda.

Maendeleo[hariri | hariri chanzo]

Kalemela ni kata inayopitika kwa urahisi kutokana na kupitiwa na barabara kuu ya Mwanza hadi Sirari katika mkoa wa Mara. Hii huifanya iwe kata inayovutia kwa shughuli za biashara.

Kalemela inayo shule moja ya sekondari iitwayo Kalemela na katika kila kijiji kuna shule ya msingi. Mwambao wa ziwa Viktoria katika kata hii unavutia uwekezaji katika nyanja za utalii wa mazingira ya ziwa. Katika eneo hili wawekezaji wengi hivi karibuni wamevutiwa na mazingira hayo na kufanya eneo la Chamugasa lishamiri kwa ujenzi wa hoteli nzuri za kisasa.

Marejeo[hariri | hariri chanzo]

  1. Nakala iliyohifadhiwa. Jalada kutoka ya awali juu ya 2018-08-05. Iliwekwa mnamo 2018-02-01.
  2. Sensa ya 2012, Simiyu Region - Busega District Council
Kata za Wilaya ya Busega - Mkoa wa Simiyu - Tanzania

Badugu | Igalukilo | Imalamate | Kabita | Kalemela | Kiloleli | Lamadi | Lutubiga | Malili | Mkula | Mwamanyili | Ngasamo | Nyaluhande | Nyashimo | Shigala

Makala hii kuhusu maeneo ya Mkoa wa Simiyu bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu eneo hilo kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Usitaje majina ya madiwani na viongozi au maafisa wengine wa sasa maana wanabadilika haraka mno.