Jua

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Jua

Jua ni nyota iliyoko karibu na Dunia yetu kuliko nyota nyingine zote. Jua ni kitovu cha mfumo wa Jua likizungukwa na sayari nane. Dunia ni moja ya sayari hizo katika mfumo wa Jua na sayari zake.

Umbo la Jua

Umbo la Jua linakaribia kuwa tufe kamili. Maada yake ni utegili yaani gesi ya joto sana inayoshikamanishwa na nguvu ya kisumaku.

Kipenyo cha Jua ni takriban kilomita 1,392,684 ambayo ni mara 109 kipenyo cha dunia yetu. Masi yake ni mara 330,000 masi ya dunia.

Kikemia masi ya Jua ni hasa hidrojeni (73%) na heli (25%). Kiasi kinachobaki ni elementi nzito zaidi, kama vile oksijeni, kaboni, chuma na nyingine. Hata kama hizi elementi nzito ni asilimia ndogo tu za masi ya Jua, bado zinalingana na mara 5,000 masi ya dunia kutokana na ukubwa wa Jua.

Historia ya Jua

Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa Jua lilitokea takriban miaka bilioni 4.57 iliyopita kutoka wingu kubwa la molekuli lililoundwa na asilimia kubwa za hidrojeni.

Kama nyota zote Jua linapita kwenye ngazi mbalimbali za maisha yake. Wataalamu wengi hukadiria ya kwamba baada ya miaka bilioni 5 ijayo akiba ya hidrojeni katika kitovu itapungua, Jua litapanuka sana na kuwa jitu jekundu[1]; katika hali hii inaweza kuenea hadi njia ya obiti ya Zuhura na hakuna nafasi tena kwa uhai duniani kutokana na mnururisho mkali.

Wataalamu wanatofautiana katika makadirio yao kama upanuzi huu utasababisha pia kupotea kabisa kwa sayari za Utaridi, Mirihi na Dunia zikimezwa na kuingia ndani ya Jua.[2]

Baada ya miaka bilioni kadhaa ya kuwaka kama jitu jekundu, masi yake itakuwa imepungua itajikaza na kuendelea kwa muda usio mrefu kama nyota ndogo na hafifu. Kuna uwezekano mkubwa wa kwamba Jua litaendelea baadaye kama nyota kibete nyeupe (White Dwarf) itakayoendelea kuzimika polepole[3].

Mnururisho na upepo wa Jua

Jua linatoa mwanga, joto na mnururisho mwingine wa aina mbalimbali. Sehemu ya mnururisho huu unatoka kwa umbo la chembe kama protoni na elektroni ambazo kwa jumla hujulikana pia kama upepo wa Jua. Masi ya upepo wa Jua ni takriban tani moja kwa kila sekunde.[4] Asili ya nishati hii ni mchakato wa myeyungano wa kinyuklia ndani yake. Katika myeyungano huo hidrojeni inabadilishwa kuwa heliamu. Elementi nyingine zinatokea pia kwa kiasi kidogo. Badiliko kutoka hidrojeni kwenda heliamu inaachisha nishati inayotoka kwenye Jua kwa njia ya mnururisho.

Nishati ya mnururisho huu ni msingi wa maisha ya mimea na viumbe hai katika dunia. Nuru ya Jua inabadilishwa na mimea kwa njia ya usanisinuru kuwa nishati ya kikemia inayojenga miili yao itakayokuwa lishe tena ya mimea na wanyama.

Tanbihi

  1. Nola Taylor Redd, Red Giant Stars: Facts, Definition & the Future of the Sun , tovuti ya space.com, March 27, 2018, iliangaliwa Aprili 2018
  2. Klaus-Peter Schroder, Robert C. Smith , Distant future of the Sun and Earth revisited, Monthly Notices of the Royal Astronomical Society. 000, 1–10 (2008) Printed 3 February 2008
  3. Linganisha makadirio ya Schroder, Smith
  4. Carroll, Bradley W.; Ostlie, Dale A. (1995). An Introduction to Modern Astrophysics (revised 2nd ed.). Benjamin Cummings. p. 409. ISBN 0-201-54730-9.

Viungo vya Nje

Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Jua kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.