James Webb (darubini ya anga-nje)

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Darubini ya Webb jinsi inavyokaa angani baada kukunjuliwa.
Darubini ya Webb jinsi ilivyokunjwa siku chache kabla ya kurushwa mnamo Desemba 2021

Darubini ya Anga-Nje ya James Webb (kwa Kiingereza: James Webb Space Telescope; kifupi: JWST) ni darubini ya anga-nje iliyorushwa angani tarehe 25 Desemba 2021. Imepangwa kuchukua nafasi ya Darubini ya Anga ya Hubble ambayo ilizinduliwa mwaka wa 1990. [1]

Darubini hiyo imepewa jina la James E. Webb, ambaye alikuwa mkurugenzi katika NASA akaunda programu ya Apollo iliyofikisha wanaanga kwenye mwezi.

Inakusudiwa kufanya upimaji hasa kwenye nuru ya infraredi. Hapo inatumia kiakisi kikuu chenye kipenyo cha mita 6.5. Kiakisi hicho kimeundwa na vipande 18 vyenye pembe sita ambavyo vimeundwa kwa berili iliyopakwa dhahabu. Ilhali kiakisi chote kingekuwa kikubwa mno wakati wa kurusha chombo angani, kilikunjwa katika nafasi ndogo. Kupakwa kwa dhahabu ni kwa sababu dhahabu inakisi vizuri nuru ya infraredi. Tabaka la dhahabu kwenye kiakisi ni kidogo ni gramu 48 pekee lakini inatosha kupata uso wa dhahabu.

Ilhali chombo chote kinalenga kupima mnururisho hafifu wa infraredi ambayo ni mnururisho wa joto, ni muhimu darubini iwe baridi iwezekanavyo. Hivyo muundo wake ni pamoja na mwavuli mkubwa wa kinga dhidi ya Jua. Mwavuli huo unafunika takriban mita 14 x 21[2] umetengezwa na matabaka matano karatasi ya plastiki nyembamba sana yatakayoakisi nuru yote ya Jua pamoja na joto kutoka sehemu ya beteri, kompyuta na redio ya darubini.

Katika uzinduzi wa Darubini ya Webb kulikuwa na changamoto mbalimbali. Moja ni kufika kweli mahali panapotakiwa jinsi ilivyokadiriwa. Kubwa zaidi ni changamoto ya kufungua mwavuli wa kinga dhidi ya Jua halafu kukunjua "jicho" la darubini, ambayo ni kiakisi chake chenye kipenyo cha mita 6.5, kinachofanywa na vipande 18. Ilhali nafasi ndani ya chombo kilichofungwa juu ya roketi ilikuwa ndogo, vifaa hivi vyote vilipaswa kukunjwa mara kadhaa. Kwa kuvikunjua kuna vifaa vingi vidogo (injini ya umeme, magurudumu ya roda, nyaya...)  na hapo kulikuwa hatari kwamba kimoja kinaweza kukwama. Maana huko kwenye umbali huo mkubwa hakuna njia ya kukitengezea.

Obiti

Obiti ya JWST (L 1,2,3,4,5 ni nukta za Lagrange)

JWST itakuwa katika obiti kilomita 1,500,000 mbali na Dunia, ili kuepuka joto kutoka Dunia.[3] Hivyo umbali wake kutoka Dunia ni kama mara 5 umbali wa Mwezi kutoka duniani.

Darubini ya Webb itakaa sehemu inayoitwa nukta msawazo au nukta ya Lagrange. Huko iko sehemu kwenye anga-nje ambako nguvu za mvutano wa Jua na Dunia zinalingana kabisa na nguvu-nje ya mwendo wake wa obiti. Kwa wataalamu kwenye kituo cha mawasiliano duniani, darubini ya Webb itapatikana kila wakati palepale angani, hali inayorahisisha mawasiliano na kurusha kwa data za vipimo.

Hivyo haizunguki Dunia, bali huzunguka Jua kwa kasi sawa na Dunia. [4]

Marejeo

  1. James Webb Space Telescope. NASA. Iliwekwa mnamo 14 May 2013.
  2. About the Sunshield, kwenye tovuti James Webb Space Telescope ya NASA; iliangaliwa 03.01.2022
  3. Webb Telescope mirrors: Stepping stones to the cosmos. NASA. Iliwekwa mnamo 6 January 2017.
  4. Interview on JWST. NPR. Iliwekwa mnamo 14 May 2013.