Nenda kwa yaliyomo

Ijtihad

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Makala hii ni sehemu ya shindano la kuandika makala za Uislamu kupitia Wiki Loves Ramadan 2025.

Sehemu ya mfululizo wa makala juu ya

Uislamu

Imani na ibada zake

Umoja wa Mungu
Manabii
Misahafu
Malaika
Uteule
Kiyama
Nguzo za Kiislamu
ShahadaSwalahSaumu
HijaZaka

Waislamu muhimu

Muhammad

Abu BakrAli
Ukoo wa Muhammad
Maswahaba wa Muhammad
Mitume na Manabii katika Uislamu

Maandiko na Sheria

AzifQur'anSunnahHadithi
Wasifu wa Muhammad
Sharia
Elimu ya Sheria za KiislamuKalam

Historia ya Uislamu

Historia
SunniShi'aKharijiyaRashidunUkhalifaMaimamu

Tamaduni za Kiislamu

ShuleMadrasa
TauhidiFalsafaMaadili
Sayansi
SanaaUjenziMiji
KalendaSikukuu
Wanawake
ViongoziSiasa
Uchumi
UmmaItikadi mpyaSufii

Tazama pia

Uislamu na dini nyingine
Hofu ya Uislamu

Ijtihad ni dhana ya kisheria katika Uislamu[1] inayomaanisha jitihada binafsi ya kielimu na kiakili inayofanywa na mtaalamu wa sheria za Kiislamu ili kupata jawabu katika masuala ya kisheria. Ni tofauti na taqlid, ambayo ni kufuata kwa upofu au kuiga maoni ya wanazuoni waliotangulia bila kuyachunguza upya.[2]

Katika mtazamo wa kisunni wa jadi, ijtihad inahitaji mtu awe na ujuzi wa hali ya juu katika lugha ya Kiarabu, elimu ya itikadi, maandiko ya ufunuo (Qur'an na Hadith), pamoja na misingi ya sheria ya Kiislamu (usul al-fiqh). Ijtihad haifanywi ikiwa kuna maandiko wazi na yasiyo na utata au ikiwa tayari kuna makubaliano ya wanazuoni (ijma) juu ya jambo fulani. Kwa wale waliohitimu, ijtihad ni wajibu wa kidini. Mwanazuoni mwenye sifa za kufanya ijtihad huitwa mujtahid.[3][4]

Katika karne tano za mwanzo za Uislamu, ijtihad ilikuwa ikifanyika kwa dhana na kwa vitendo miongoni mwa Waislamu wa Kisunni. Hata hivyo, kuanzia karne ya 12, suala la uhalali wa ijtihad lilianza kuibua mijadala. Kufikia karne ya 14, baadhi ya wanazuoni mashuhuri wa Kisunni walidai kuwa masuala yote muhimu ya sheria yalikuwa tayari yamepatiwa majibu, hivyo wakapendekeza kupunguza matumizi ya ijtihad.

Katika nyakati za kisasa, baadhi ya wasomi wa Magharibi na sehemu ya Waislamu waliamini kuwa “mlango wa ijtihad” ulifungwa katika zama hizo za mwanzo. Hata hivyo, utafiti wa hivi karibuni unaonesha kuwa ijtihad haijawahi kusitishwa kabisa katika historia ya Kiislamu, ingawa njia na upeo wake zimekuwa zikibadilika. Tofauti miongoni mwa wanazuoni wa sheria (fuqaha) zilifanya Waislamu wa Kisunni washindwe kufikia muafaka juu ya hatima ya ijtihad na nafasi ya mujtahid. Licha ya hayo, ijtihad iliendelea kuwa sehemu muhimu ya mfumo wa sheria za Kiislamu.

Katika kipindi cha mwanzo cha zama za kisasa, bado ijtihad iliendelea kutumika, na mara kwa mara baadhi ya wanazuoni walisisitiza kuwa ijtihad ni bora zaidi kuliko taqlid.

Kuanzia karne ya 18, wanamageuzi wa Kiislamu walianza kutaka taqlid iachwe na ijtihad kupewa kipaumbele, wakiona hilo kama njia ya kurejea kwenye asili ya Uislamu. Mijadala ya umma kuhusu ijtihad bado inaendelea hadi leo, hasa katika harakati kama Salafiyya na Uislamu wa kisasa ambazo zimekuwa zikihusishwa sana na kuhimiza ijtihad. Kwa Waislamu wa Magharibi, mitazamo mipya kuhusu ijtihad imeibuka, ikisisitiza zaidi maadili na thamani za msingi kuliko mbinu za jadi za sheria.

Kwa upande wa Waislamu wa Kishia, neno ijtihad halikuanza kutumika hadi karne ya 12. Kabla ya hapo, isipokuwa kwa madhehebu ya Zaydi, wanazuoni wa Kishia wa mwanzo walipinga matumizi ya ijtihad katika masuala ya kisheria. Hali ilianza kubadilika baada ya kushirikishwa kwa mafundisho ya Mu’tazila na fiqh ya Kisunni. Kufikia karne ya 19, baada ya wanazuoni wa Kishia wa mtazamo wa Usuli—waliokuwa wakijenga sheria kwa misingi ya kiakili—kushinda dhidi ya Akhbari, waliokuwa wakiegemea zaidi kwenye mapokeo, ijtihad ikawa sehemu ya kawaida katika utendaji wa sheria za Kishia.[5]

  1. Rabb, Intisar A. (2009), "Ijtihād", The Oxford Encyclopedia of the Islamic World (kwa Kiingereza), Oxford University Press, doi:10.1093/acref/9780195305135.001.0001/acref-9780195305135-e-0354, ISBN 978-0-19-530513-5, iliwekwa mnamo 2025-03-16
  2. Rabb, Intisar A. (2009). "Ijtihād". In John L. Esposito (ed.). The Oxford Encyclopedia of the Islamic World. Oxford: Oxford University Press. ISBN 978-0-19-530513-5.
  3. John L. Esposito, ed. (2014). "Taqiyah". Ijtihad. The Oxford Dictionary of Islam. Oxford: Oxford University Press. ISBN 978-0-19-512558-0.
  4. Wakati mwingine huandikwa kama mojtahed
  5. Mohammad Farzaneh, Mateo (2015). The Iranian Constitutional Revolution and the Clerical Leadership of Khurasani. Syracuse, New York: Syracuse University Press. p. 6. ISBN 978-0-8156-3388-4.