Idrissa Ouédraogo

Idrissa Ouédraogo (1954 - 2018) alikuwa mtengenezaji wa filamu kutoka Burkina Faso. Kazi yake mara nyingi ilichunguza migongano kati ya maisha ya vijijini na mijini, pamoja na kati ya mila na usasa katika nchi yake ya asili ya Burkina Faso na maeneo mengine barani Afrika. Anajulikana zaidi kwa filamu yake ya Tilaï, ambayo ilishinda Grand Prix katika Tamasha la Filamu la Cannes la 1990 na Samba Traoré (1993), ambayo iliteuliwa kwa tuzo ya Silver Bear katika Tamasha la Filamu la Kimataifa la Berlin la 43.[1]
Maisha ya Awali na Elimu
[hariri | hariri chanzo]Idrissa Ouédraogo alizaliwa Banfora, Volta ya Juu (sasa panaitwa Burkina Faso), mnamo mwaka 1954.[2] Alikulia katika mji wa Ouahigouya katika eneo la kaskazini mwa nchi yake, na mnamo mwaka 1976 alipewa Shahada ya Awali ya Sanaa. Ili kuhakikisha anapata maisha bora, wazazi wake wakulima walimpeleka Ouagadougou kwa ajili ya masomo ya juu, ambako alisoma katika Taasisi ya Afrika ya Masomo ya Sinema (Institut Africain d’Etudes Cinématographiques) na kumaliza masomo yake mwaka 1981 na kupata shahada ya uzamili.[3] Baada ya kusoma huko Kiev katika Umoja wa Kisovieti, alihamia Paris, ambako alihitimu kutoka taasisi inayoitwa Institut des hautes études cinématographiques mwaka 1985 na kupata shahada ya Uzamili ya masomo ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Sorbonne.[2][3][4]
Maisha ya Awali
[hariri | hariri chanzo]Katika filamu yake fupi ya mwanzo, Pourquoi (1981), mwanamume anaota ya ndoto kumuua mkewe, lakini hana uhakika kama ni ndoto au hali halisi.[3] Ouédraogo aliifuata kazi hiyo kwa filamu nyingine fupi, Poko (1981), ambayo ilishinda tuzo ya filamu fupi katika Tamasha la Filamu na Televisheni la Pan-Afrika la Ouagadougou la mwaka huo. Poko anamfuata mwanamke mjamzito ambaye anafariki baada ya kushindwa kufikia vituo vya matibabu alipokuwa akisafirishwa kwa mkokoteni. Filamu hiyo iliangazia ukweli kwamba licha ya kulipa kodi zao, maskini hupata msaada mdogo wa kivitendo katika mahitaji ya kila siku kutoka kwa serikali.[3] Hii ilifuatiwa na filamu fupi nyingine kama Les Écuelles ("The Platters"; 1983), Les Funérailles du Larle Naba, ("Larle Naba's Funeral"; 1984), Ouagadougou, Ouaga deux roues ("Ouagadougou, Ouaga Two Wheels"; 1985) na Issa le tisserand ("Issa the Weaver"; 1985).[5] Filamu yake ya mwisho fupi ilikuwa Tenga (1985), ambayo inamchunguza mwanakijiji ambaye baada ya kuhamia mjini, anarudi katika mji wake wa asili. Katika filamu hizi fupi za Ouédraogo anachunguza mada na mbinu za filamu ambazo angerejea katika filamu zake za baadaye.[5]
Filamu Maalumu
[hariri | hariri chanzo]Filamu ya kwanza ya Ouédraogo, Yam Daabo ("The Choice"; 1986) ilipokelewa vyema, na inahusu uamuzi wa familia ya kijijini kubaki kutegemea misaada au kuhama eneo lingine na kujitegemea.[5] Filamu yake ya kwanza kupokea usambazaji mkubwa ilikuwa ni Yaaba ("Bibi"), ambayo ilishinda tuzo katika sherehe, ikiwa ni pamoja na Tuzo ya FIPRESCI huko Cannes, na ilionyeshwa kote ulimwenguni,ilipata umaarufu kwa sababu ya uzuri na unyenyekevu wake. Licha ya umaarufu wake, wakosoaji waliona Yaaba ilikosa ufahamu muhimu kuhusu masuala mazito yaliyoathiri maisha ya vijijini.[5]
Filamu yake iliyofuata ya Tilaï ("Swali la Heshima") ilishinda tuzo ya Grand Prix katika Tamasha la Filamu la Cannes mwaka 1990.[6] Ilijikita katika wakati wa mabadiliko katika utamaduni wa Mòoré, ambapo maisha ya watoto wa familia yanavurugika kutokana na kushikilia mila katika ulimwengu wa kisasa unaobadilika haraka.[7] Mafanikio ya Yam Daabo na Tilaï yaliweka shinikizo kwa Ouédraogo kutoa mafanikio mengine ya kimataifa, na filamu yake iliyofuata ya Karim na Sala iliharakishwa kuonyeshwa katika Tamasha la 12 la Filamu na Televisheni la Pan-Afrika la Ouagadougou na haikupokelewa vizuri, pamoja na kuwa na usambazaji duni.[7] Samba Traoré (1993) ilirudi kwenye mada za maisha ya vijijini dhidi ya mijini, mila dhidi ya mabadiliko na ilipokelewa vizuri, ikiteuliwa kwatuzo ya Silver Bear katika Tamasha la 43 la Filamu la Kimataifa la Berlin.[8] Baada ya Samba Traoré ,Ouédraogo alifuata na filamu ya Kilio cha Moyo (Le Cri du cœur, 1994), Kini na Adams mwaka 1997, Anger of the Gods (La Colère des dieux mwaka 2003) na Kato Kato mwaka 2006.
Maisha ya baadaye
[hariri | hariri chanzo]Mnamo mwaka 2015, Ouédraogo alitangaza kwa ufupi kabla ya kufunguliwa kwa Tamasha la 24 la Filamu na Televisheni la Pan-Afrika la Ouagadougou hamu yake ya kuongoza "filamu muhimu" kuhusu ukoloni wa kigeni wa bara la Afrika, mapambano dhidi ya ukoloni na watu mashuhuri wa harakati hiyo.[9] Wakati wa mahojiano ya mwaka 2015 na Le Monde, Ouédraogo alisisitiza kile alichoamini kuwa masuala matatu yanayoikabili tasnia ya filamu ya Burkina Faso. Miongoni mwa masuala hayo ni ukosefu wa maarifa na taaluma ya kutosha linapokuja suala la upigaji picha. Uhaba wa fedha na kutokuwepo kwa soko la ndani linalohitaji juhudi ni nojawapo ya matatizo mengine mawili aliyoyataja.[10] Katika miaka yake michache ya mwishoni, ndugu wa Ouédraogo walibaini ndugu yao kukatishwa tamaa katika sinema ya kisasa ya Kiafrika kutokana na kile alichokiona kama upungufu wa vipaji na pia upungufu wa rasilimali za uzalishaji.[11]
Marejeo
[hariri | hariri chanzo]- ↑ "Cinéma : le réalisateur burkinabè Idrissa Ouedraogo est mort". L'Orient-Le Jour (kwa Kifaransa). 2018-02-18. Iliwekwa mnamo 2026-04-02.
- 1 2 "Personnes | Africultures : Ouedraogo Idrissa". Africultures (kwa Kifaransa). Iliwekwa mnamo 2026-04-02.
- 1 2 3 4 Russell, Sharon A. (1998). Guide to African Cinema (kwa Kiingereza). Bloomsbury Academic. ISBN 978-0-313-29621-5.
- ↑ "Ouédraogo, Idrissa | African Film Festival, Inc" (kwa American English). Iliwekwa mnamo 2026-04-02.
- 1 2 3 4 Russell, Sharon A. (1998). Guide to African Cinema (kwa Kiingereza). Bloomsbury Academic. ISBN 978-0-313-29621-5.
- ↑ "TILAI", Festival de Cannes (kwa Kiingereza), iliwekwa mnamo 2026-04-02
- 1 2 Russell, Sharon A. (1998). Guide to African Cinema (kwa Kiingereza). Bloomsbury Academic. ISBN 978-0-313-29621-5.
- ↑ "Prizes & Honours 1993". www.berlinale.de (kwa Kiingereza). Iliwekwa mnamo 2026-04-02.
- ↑ "Checking your browser…". lesechosdufaso.net. Iliwekwa mnamo 2026-04-02.
- ↑ "Idrissa Ouedraogo : « Le cinéma low-cost ne veut rien dire »", Le Monde.fr (kwa Kifaransa), iliwekwa mnamo 2026-04-02
- ↑ https://www.lemonde.fr/afrique/article/2018/02/19/deces-d-ouedraogo-il-venait-de-terminer-un-scenario-et-nous-ferons-tout-pour-realiser-le-film_5259409_3212.html