Nenda kwa yaliyomo

Historia ya uandishi wa Kurani

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru

Historia ya uandishi wa Kurani, kwa mujibu wa Uislamu, imeteremshwa na Mwenyezi Mungu kupitia Jibrili mmojawapo wa Malaika wakubwa wenye heshima kubwa huko mbinguni. Kurani iliteremka kwa njia ya Wahyi au Ufunuo katika muda wa miaka 23 ya utume wa Muhammad.

Maneno yote yaliyomo ndani ya Kurani yanadaiwa na Waislamu kuwa ni ya Mwenyezi Mungu na kuwa Muhammad hakuwa akisema maneno haya kwa mujibu wa matamanio yake.

Kurani ilikuwa ikiteremshwa kidogokidogo katika muda huo wa miaka 23 kulingana na munasaba mbalimbali wa maisha ya Waislamu wa wakati huo ili kuwafahamisha namna bora ya kuishi ulimwenguni kwa wema na hisani na uhusiano wao baina yao wenyewe kwa wenyewe na baina yao na wasiokuwa Waislamu katika wao.

Aidha, Kurani ilikuwa ikigusia masuala mbalimbali ya maisha na mifano ya umma zilizopita ambazo hazikukubali tume za Mwenyezi Mungu kwao zikaangamizwa kwa kupinga na kwenda kinyume na Mitume na Manabii wao.

Zama za Mtume Muhammad

[hariri | hariri chanzo]

Kurani ilipoteremka kwanza iliandikwa, kwa amri ya Mtume Muhammad, kwenye vitambaa, ngozi, mifupa na majiwe. Muhammad alikuwa akiwaelekeza waandishi wake waandike kwa mujibu wa mpango na utaratibu fulani ambao unatokana na Mwenyezi Mungu mwenyewe.

Wakati wa Mtume Muhammad Kurani ilikuwa zaidi katika nyoyo za Masahaba ambao wengi wao walikuwa wameihifadhi Kurani nzima, na wengi wao walikuwa wakiiandika kwa njia mbalimbali lakini si katika msahafu mmoja.

Zama za Abubakar Siddiq

[hariri | hariri chanzo]

Abubakar Siddiq, Khalifa wa Mtume wa kwanza baada ya kufa kwake, alimtuma Zayd bin Thabit kuikusanya Kurani yote katika kitabu kimoja.

Umar bin Al-Khattab, Khalifa wa pili ndiye aliyemshauri Abubakar kuikusanya Kurani na ijapokuwa mwanzo aliona taabu kufanya jambo ambalo Mtume mwenyewe hakulifanya.

Hatimaye, Abubakar alikubali rai yake na Kurani ikakusanywa katika kitabu kimoja.

Zama za Uthman bin Affan

[hariri | hariri chanzo]

Baada ya Kurani kuandikwa kamili katika msahafu mmoja na kuwekwa katika nyumba ya Hafsa binti Umar, mmoja katika wake wa Mtume Muhammad, ulipofika wakati wa kutawala Uthman bin Affan, Khalifa wa tatu wa Mtume Muhammad, aliamrisha waandishi fulani kuuchukua huo msahafu na kunukulu nakala nyingine kwa ajili ya kupeleka sehemu mbali mbali za ulimwengu wa kiislamu ambao kwa wakati huo ulikuwa mkubwa sana na kufikia nchi nyingi za Afrika, Asia na Ulaya.

Waandishi wa Kurani Tukufu

[hariri | hariri chanzo]

Uthman bin Uffan aliwaamuru waandishi wafuatao kuandika Kurani kutokana na msahafu wa Hafsa na kutawanya nakala hizi katika sehemu mbalimbali za ulimwengu wa kiislamu:

Zayd Ibn Thabit. Abdullah Ibn Al-Zubair. Said Ibn Al-`As. Abdul-Rahman Ibn Al-Harith Ibn Hisham.

Uthman aliweka nuskha moja Madina na kupeleka nyinginezo sehemu nyinginezo za ulimwengu wa kiislamu.

Tazama pia

[hariri | hariri chanzo]

http://www.sunnah.org/history/quran_compiled.htm Ilihifadhiwa 11 Oktoba 2007 kwenye Wayback Machine.