Nenda kwa yaliyomo

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Maporomoko ya maji katika safu ya Milima ya Udzungwa

Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa ipo katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa na Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, nchini Tanzania. Sehemu kubwa ya hifadhi hii ipo ndani ya Wilaya ya Kilolo. Eneo lake lina ukubwa wa kilomita za mraba 1,990 (sawa na maili 770).[1]

Hifadhi hii ina makaazi mbalimbali ya asili yakiwemo msitu wa mvua wa kitropiki, misitu ya milimani, msitu wa miombo, nyanda za majani na maeneo ya kupandisha ngazi. Tofauti ya urefu kutoka usawa wa bahari ni kati ya mita 250 hadi 2,576 (kilele cha Lohomero), ikijumuisha sehemu ya Milima ya Udzungwa ambayo ni sehemu ya Milima ya Tao la Mashariki.[2]

Hifadhi ina zaidi ya aina 400 za ndege, mimea zaidi ya 2,500 (asilimia 25 ya hiyo ni spishi endeshi) na spishi 6 za nyani. Ni hifadhi ya pili kwa wingi wa viumbe hai barani Afrika.[1][2]

Spishi endeshi

[hariri | hariri chanzo]

Spishi sita za nyani zimeripotiwa kupatikana katika hifadhi hii, ambapo tano kati yake ni endeshi. Mbega mwekundu wa Iringa, Mbega mwekundu wa Udzungwa, na Sanje mangabey hupatikana tu katika Hifadhi ya Milima ya Udzungwa. Spishi ya mangabey hiyo haikujulikana na wanasayansi hadi mwaka 1979.[3]

Spishi mpya ya kameleoni endeshi iligunduliwa mwaka 2009 ndani ya hifadhi hii.[4]

Shughuli

[hariri | hariri chanzo]

Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Udzungwa unajikita zaidi katika kupanda milima na matembezi ya miguu, kwa kuwa hifadhi haina barabara za magari na inafikika kwa miguu tu. Njia za matembezi zinatofautiana kwa ugumu, kuanzia matembezi mafupi ya saa moja ya njia ya Sonjo hadi safari ngumu ya siku sita ya njia ya Lumemo yenye kambi.

Njia maarufu zaidi ni ile ya Maporomoko ya Sanje ambayo huchukua takribani saa nne na humwezesha mtembezaji kuona maporomoko mazuri yenye urefu wa mita 170 na kuogelea katika bwawa la maji linalotokana na maporomoko hayo.[1]

Malazi kwa wageni ndani ya hifadhi yanapatikana kwa mfumo wa kambi tu, kwani hakuna hoteli au nyumba za wageni ndani ya mipaka ya hifadhi. Katika kijiji cha jirani cha Mang'ula, kuna nyumba kadhaa za kulala wageni kwa bei nafuu.[1]

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 "Udzungwa Mountains National Park". Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania.
  2. 2.0 2.1 Lovett, Jon C., Andrew R. Marshall, and Jeff Carr. "Changes in tropical forest vegetation along an altitudinal gradient in the Udzungwa Mountains National Park, Tanzania." African Journal of Ecology 44.4 (2006): 478-490.
  3. Araldi, Alessandro, et al. "Density estimation of the endangered Udzungwa red colobus (Procolobus gordonorum) and other arboreal primates in the Udzungwa Mountains using systematic distance sampling." International Journal of Primatology 35 (2014): 941-956.
  4. Menegon, Michele, et al. "A new species of chameleon (Sanria: Chamaeleonidae: Kinyongia) from the Magombera forest and the Udzungwa Mountains National Park, Tanzania." African Journal of Herpetology 58.2 (2009): 59-70.

Viungo vya nje

[hariri | hariri chanzo]

Udzungwa Mountains National Park travel guide kutoka Wikisafiri