Gesijoto

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Hesabu ya viwango vya joto vinavyopoelewa na dunia, kuakisishwa angani na kuzunguka katika angahewa

Gesijoto (ing.greenhouse gases) ni aina za gesi katika angahewa ya dunia zenye uwezo wa kuathiri mnururisho wa infraredi yaani wa joto. Ni sababu muhimu ya kupanda kwa halijoto duniani.

Kazi ya gesijoto[hariri | hariri chanzo]

Gesijoto zinarudisha sehemu ya joto inayotoka ardhini kuelekea anga-nje na kuirudisha ardhini. Nusutufe ya dunia yetu inayoangalia jua (yaani penye mchana) inapokea kila siku kiasi cha joto kutoka jua na wakati huohuo nusutufe ya kinyume (penye usiku) inapokea tena joto kwa kuiachisha katika anga-nje.

Kuna gesijoto asilia na pia gesijoto zilizoongezwa na binadamu. Kuwepo kwa gesijoto si jambo baya maana binadamu na maumbile asilia yote vilitokea katika dunia penye gesijoto. Swali ni kuhusu kiasi chake. Gesijoto zinaunda uwezo wa angahewa ya dunia kutunza kiwango cha joto ndani yake. Bila gesijoto asilia dunia yetu ingekuwa baridi mno, kwa wastani na sentigredi -18 °C badala ya wastani ya +14 °C jinsi ilivyo sasa.

Kama kiasi cha gesi hizi kinabadilika kitaleta pia mabadiliko katika halijoto ya dunia kwa jumla; kama gesijoto zinaongezeka halijoto ya dunia inapanda na kama gesijoto zinapungua halijoto ya dunia inashuka kiwango fulani.

Tatizo linalojadiliwa tangu miaka 20 hivi ni kuongezeka kwa gesijoto katika angahewa kulikosababishwa na shughuli za kibinadamu. Kuongezeka kwa gesijoto hewani kunasababisha kupanda kwa halijoto duniani kunakoleta hasara kwa spishi nyingi. Viumbe vyote pamoja na mimea, wanyama na binadamu vilizoea hali ya joto jinsi ilivyo kwa milenia nyingi. Mabadiliko ya haraka ni hatari.

Aina za gesijoto[hariri | hariri chanzo]

Gesijoto asilia zinazopatikana katika angahewa na kutunza joto la sayari ni pamoja na mvuke wa maji, hewa ukaa (kaboni dioksidi), methani, oksidi dinitrojeni (N2O) na ozoni O2

Matatizo ya kuongezeka kwa gesijoto zinazosababishwa na binadamu[hariri | hariri chanzo]

Tatizo ni kupanda kwa halijoto katika miaka 150 iliyopita kutokana na shughuli za kibinadamu zilizosababisha kuongezeka kwa gesijoto juu ya kiwango asilia tangu kutokea kwa mapinduzi ya viwandani katika karne ya 19. Maendeleo haya yalipata nguvu ya kuendesha mashine, meli na motokaa kwa njia ya kuchoma fueli kisukuu kama makaa mawe na mafuta ya petroli. Kuchoma vile kuliachisha gesijoto nyingi kwenye angahewa.

Kati ya gesijoto zilizoongezeka tangu karne ya 19 ni hasa gesi ya ukaa (kaboni dioksidi).

Pamoja na kuchoma fueli kisukuu njia nyingine ya kuongeza gesi ya ukaa ni kukata miti kwa wingi kwa kuunda nafasi za kujenga makazi ya watu na kuanzisha mashamba. Miti ina tabia ya kujenga miili yao (shina, matawi, majani) kwa kutoa gesi ya ukaa hewani, kuipasua kwa elementi zake (kaboni na oksijeni) na kutumia kaboni kama sehemu ya seli za ubao wake. Kupunguza idadi ya miti imepunguza uwezo asilia ya mazingira ya kuondoa gesijoto hewani.

Mapatano ya kimataifa[hariri | hariri chanzo]

Tangu kuelewa hatari zinazotokana na kupanda kwa halijoto duniani kunajitihada nyingi ya viongozi wa mataifa mengi kuleta mabadaliko ya kuhifadhi mazingira. Tangu 1993 kuna Kongamano la Mfumo wa UM kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi inayolenga kupunguza kwa kupanda kwa halijoto duniani kwa kupunguza uzalishaji wa gesi ya dioksidi kabonia.

Kongamano hili lilileta mapatano ya Kyoto na Paris na tangu haya nchi nyingi zimeanza kupunguza matumizi ya makaa na mafuta katika uzalishaji wa umeme. Badala yake teknolojia za nishati mbadala zimesogea mbele kama tabo za upepo (rafadha za upepo) na kuongeza paneli za umemenuru.

Viungo vya Nje[hariri | hariri chanzo]