Friedrichstadt
Friedrichstadt (tamka Frid - rikh - stat) ni mji mdogo wa jimbo la Schleswig-Holstein nchini Ujerumani. Uko upande wa magharibi karibu na mwambao wa Bahari ya Kaskazini.
Idadi ya wakazi mwaka 2014 ilikuwa watu 2,485.
Historia
[hariri | hariri chanzo]Mji huu mdogo una historia ya kuvutia na ni kumbukumbu ya kihistoria.
Ulianzishwa mwaka 1621 na kabaila wa Holstein Friedrich III. Mtawala huyo alikuwa na mipango ya kuongeza mapato yake kwa njia ya biashara. Alilenga kufungua njia mpya ya biashara bila kutegemea Waingereza, waliokuwa na jahazi zao kati ya Uhindi na Ulaya, wala Waosmani. Kwa hiyo alilenga kuwasiliana na Uajemi kupitia Urusi akahitaji kwa mipango yake bandari upande wa magharibi wa utemi wake.
Hivyo alialika Wakristo wa jumuiya ndogo kutoka nchini Uholanzi waliokosa ustahamilivu kwao nyumbani hasa Wamenno na Waremonstranti akawaahidia uhuru wote wa kujenga makanisa yao, kufuata imani yao na ardhi, kuwa na shule na makanisa kwa lugha yao pamoja na ardhi kwa kulima na kujenga nyumba.
Kwa hiyo mji mpya ukajengwa na Waholanzi na kwa zaidi ya karne moja Kiholanzi kilikuwa lugha kikuu mjini.
Mipango ya kiuchumi haikufaulu kweli, Waholanzi wengine wakarudi kwao, na kutokana na mabadiliko ya usafiri kwa maji bandari ya Friedrichstadt ikawa ndogo kwa meli kubwa zaidi.
Hivyo umebaki mji wa kihistoria wenye nyumba zilizohifadhiwa na makanisa ya madhehebu yasiyo kawaida katika Ujerumani.