Fathia Bettahar
Fathia Bettahar (27 Agosti 1936 - 4 Agosti 2021) alikuwa mwalimu, mshauri wa sera za serikali, na mtetezi wa haki za wanawake kutoka Algeria. Baada ya kumaliza masomo yake katika chuo cha ualimu mjini Oran mwaka 1955, alianza kufundisha kuanzia mwaka 1956 hadi 1964. Baadae alifanya kazi kama msimamizi wa shule hadi mwaka 1974.
Katika kipindi hicho, alianza kujihusisha na masuala ya haki za wanawake na akajiunga na kikundi cha Umoja wa Kitaifa wa Wanawake wa Algeria . Alikuwa na nia kubwa ya kusaidia wanawake na wasichana kupata elimu.
Mwaka 1974, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Kitaifa wa Wanawake wa Algeria, na kwa wakati huo huo alikuwa Katibu Mkuu wa Shirika la Wanawake la Afrika PAWO.Alishiriki katika mikutano mingi ya wanawake duniani, ikiwemo Mkutano wa Dunia wa Wanawake wa mwaka 1975 uliofanyika Mexico City, mkutano wa Shirikisho la Kimataifa la Kidemokrasia la Wanawake (WIDF) uliofanyika Berlin Mashariki mwaka 1975, na Mkutano wa Dunia wa Wanawake wa mwaka 1985 uliofanyika Nairobi, Kenya.Kuanzia mwaka 1975 hadi 1981, alikuwa Makamu wa Rais wa WIDF, na aliendelea kuwa kiongozi wa PAWO hadi mwaka 1986.
Kati ya mwaka 2001 na 2021, Bettahar alikuwa mjumbe wa Tume ya Kitaifa ya Ushauri wa Kulinda na Kukuza haki za Binadamu CNCPPDH. Chombo hiki huru cha Algeria kilikuwa kikifuatilia sheria na hali ya haki za binadamu nchini humo.
Katika maisha yake yote, alipokea tuzo na heshima nyingi, ikiwemo Nishani ya Ana Betancourt kutoka Cuba, Nishani ya Kitaifa ya Heshima ya Guinea, na Nishani ya Kitaifa ya Mali. Pamoja na ya akina mama waanzilishi wa Shirika la Wanawake wa Afrika (PAWO), picha yake inaoneshwa katika makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, Ethiopia.